Arne Slot afunguka
Muktasari:
- Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England walishuhudia mpango wao wa kumsajili Marc Guehi kwa ada ya Pauni 35 milioni kushindwa kutiki kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili lililopita la majira ya kiangazi.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA Arne Slot amesema Liverpool kusajili beki wa kati mpya kwenye dirisha la Januari sio kipaumbele kikuu na badala yake amewekeza nguvu kwenye kuboresha maeneo mengine.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England walishuhudia mpango wao wa kumsajili Marc Guehi kwa ada ya Pauni 35 milioni kushindwa kutiki kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili lililopita la majira ya kiangazi.
Kwa sasa, Liverpool imebaki na mabeki wa kati watatu tu wa Slot kuwachagua baada ya Giovanni Leoni kupata maumivu ya goti mwezi Septemba, majeraha yatakayomweka nje kwa muda mrefu.
Liverpool imekuwa na shida nyingi kwenye safu yao ya mabeki msimu huu, ikiruhusu mabao 27 katika mechi 18 huku ikifanyikiwa kwenye mechi nne tu ambazo ilicheza bila ya nyavu zao kuguswa. Wakati huo, Ibrahima Konate, ambaye anahusika kwenye ubovu huo wa beki ya Liverpool, bado hajui hatima ya maisha yake huko Anfield kutokana na mkataba wake kutarajia kufika tamati mwishoni mwa msimu huu.
Joe Gomez naye hatima yake haijawekwa wazi, ambaye kwenye dirisha lililopita alihusishwa na mpango wa kuondoka kabla ya dili la Guehi kukwama, huku nahodha Virgil van Dijk atatimiza umri wa miaka 35 na itakapofika mwisho wa msimu atakuwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake wa kuitumikia miamba hiyo ya Anfield.
Lakini, kocha Slot amepuuzia umuhimu wa Liverpool kuwekeza kwenye kunasa beki ya kati katika dirisha la Januari. Wakati usajili wa katikati ya msimu ukiwa haupo kwenye mpango wa kipaumbele kwenye kikosi cha Liverpool, kocha Slot alisema watafikiria kuweka nguvu kwenye maeneo mengine, huku ikihusishwa na mpango wa kumsajili mshambuliaji Antoine Semenyo.
“Hili si swali nililolitarajia, kuzungumzia usajili kwenye dirisha la majira ya baridi,” alisema Slot katika mkutano wa waandishi wa habari kabla ya mechi dhidi ya Nottingham Forest.
“Nadhani kuna mechi nyingi za kucheza kabla ya kufikia dirisha la usajili. Katika hali ambayo tupo, hicho ni kitu cha mwisho kwenye akili yangu. Pengine sio kwa Richard (Hughes), lakini hicho ni kitu cha mwisho kwenye akili yangu. Sio mjadala kwa upande wangu kwa sasa.
“Kwa kipindi hiki tuna mabeki wa kati wa tatu, akiwamo Joe Gomez. Na pengine Ryan (Gravenberch) na Wata (Endo) wanaoweza kucheza kwenye eneo hilo. Pengine bado hatujalitazama hilo kwa kina, lakini kuna maeneo mengine, kwa kipindi kingine, hii ni ishu zaidi.”
Liverpool imeripotiwa kuwa moja ya timu zinazoripitiwa kuhitaji saini ya Semenyo kutoka Bournemouth kwenye dirisha la Januari, huku mkali huyo wa Ghana kwenye mkataba wake kimewekwa kipengele cha kuhitaji Pauni 65 milioni ili kuvunja mkataba wa staa huyo.