Amorim aanika mikakati yake Man United
Muktasari:
- Ripoti za hivi karibuni zimeonyesha kuwa Man United inajiandaa kuuza nusu ya kikosi chake katika dirisha moja au mawili yajayo ya uhamisho, huku mmiliki mwenza wa timu hiyo Sir Jim Ratcliffe akipanga kufanya mabadiliko makubwa.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim ameainisha mipango yake kuelekea dirisha lijalo la usajili huku taarifa zikieleza kwamba nusu ya wachezaji wa kikosi chake wanaweza kuondoka.
Ripoti za hivi karibuni zimeonyesha kuwa Man United inajiandaa kuuza nusu ya kikosi chake katika dirisha moja au mawili yajayo ya uhamisho, huku mmiliki mwenza wa timu hiyo Sir Jim Ratcliffe akipanga kufanya mabadiliko makubwa.
INEOS inaripotiwa kuwa tayari kumkabidhi Amorim jukumu la kusuka upya kikosi kuanzia Januari mwakani.
Kocha huyo raia wa Ureno, ambaye aliajiriwa mwezi uliopita baada ya kuondoka kwa Erik ten Hag, amefichua mkakati wake kuelekea dirisha lijalo akifunguka kwamba anataka kupandisha baadhi ya mastaa kutoka akademi mbali ya kusajili kutoka timu nyingine.
“Kwanza nitajikita zaidi katika kuboresha na kuendeleza vipaji vya wachezaji waliopo, kwani hiyo ni moja ya changamoto za timu yetu na pia tutaangalia wachezaji wengine wa kuwasajili. Kimsingi kuna mambo mengi ya kufanya. Lakini kabla ya kufikiria kununua lazima, ujikite kwenye kuboresha wachezaji wa ndani na baada ya hapo ndio utoke nje,” alisema Amorim.
“Tuna wachezaji wa kimataifa, ni wachezaji wazuri na tunahitaji muda kuwafundisha mfumo wetu wa uchezaji, halafu baada ya hapo tutaona. Unajua hii ni timu kubwa hivyo ikiwa mimi nitashindwa au wachezaji watashindwa mmoja wapo lazima ataondoka, hivyo inatakiwa tusaidiane ndani kwanza.”
Baada ya kupoteza mechi mbili, United ilikuwa tena uwanjani jana, katika Europa League.