Huko Man United hofu tupu

Monday January 11 2021
man pic

MANCHESTER, ENGLAND. NI hofu tupu kwa kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer baada ya Paul Pogba, Victor Lindelof na Luke Shaw kupatwa na majeraha ambayo huenda yakawafanya kukosa mechi chache zijazo.

 Baada ya mchezo wa raundi ya tatu wa Kombe la FA dhidi ya Watford walioibuka na ushindi wa bao 1-0, Solskjaer alithibitisha wachezaji hao ambao hawakucheza mechi hiyo Pogba, Lindelof na Shaw wanasumbuliwa na majeraha.

Lindelof na Shaw walitolewa kwenye kikosi muda mchache kabla ya mchezo kuanza huku Eric Bailly akipata majeraha ndani ya mechi na kuzidi kuongeza presha kuelekea mechi zijazo.

Pogba amekuwa kwenye majeraha ya mara kwa mara tangu kuanza kwa msimu wa 2019-20 akisumbuliwa zaidi na maumivu ya kifundo cha mguu na aliwahi kufanyiwa upasuaji uliosababisha akae nje kwa muda mrefu.

Msimu huu pia matatizo hayo yamezidi kumuandama na imesababisha akose mechi kadhaa baada ya kuumia akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa.

Hili ni pigo kwa sababu Man United itakuwa na michezo migumu kwa wiki ijayo katika Ligi Kuu England pale itakapoanza kuvaana na Burnley kabla ya kuangukia kwa Liverpool.

Advertisement

Hata hivyo, Solskjaer anaamini majeraha waliyoyapata wachezaji hao sio makubwa na watarejea kwenye utimamu wao wa kimwili haraka.

“Hawakucheza kwa sababu ni mejeruhi, Baily sidhani kama ameumia sana ni maumivu tu ya misuli na tuna matumaini atakuwa sawa ndani ya muda mfupi, taarifa kamili tutatoa baada ya kumfanyia vipimo zaidi,” alisema.

Akizungumzia mchezo huo alisema amefurahishwa na kitendo cha kuvuka kwenye hatua hiyo na kuelekea hatua nyingine na kiujumla walianza vizuri kwenye dakika 15 hadi 20, lakini baada ya hapo wakaanza kucheza vibaya bila kuzingatia umbo la timu na ndio maana mechi ikawa ngumu hata wakaibuka na ushindi wa bao 1-0.

Baily pia amekuwa muathirika wa tatizo la majeraha ya mara kwa mara.

Advertisement