Usiyowapenda wanakuja maze

SAHAU matokeo ya dakika moja furaha na dakika nyingine hasira ambayo kikosi cha timu ya taifa, Harambee Stars, kinawapa mafans wao na tugeukie mikikimikiki ya Ligi Kuu Kenya kurudi tena wikendi hii.

Naam! Utamu wa FKFPL ulikuwa umesimama kwa takribani wiki mbili kupisha Harambee Stars chini ya kocha Engin Firat kucheza gemu mbili za kimataifa za kirafiki yakishuhudia matokeo ‘yakustaajabisha’.

Wakiwa ugenini, Harambee Stars ilichomoza na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Qatar na juzi Jumanne wakicheza mbele ya mafans wao jijini Nairobi, walikuta wakichezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Sudan Kusini ambao siku tano kabla walifungwa mabao 4-0 na Mali mechi ya kufuzu Kombe la Afrika mwakani nchini Ivory Coast.

Hakika Firat anayedai malimbikizo ya misharaha bado anakazi kubwa kuisuka Harambee Stars ambayo inalenga kucheza kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia 2026.

Tukiyaacha hayo ya Harambee Stars, wikendi hii ni mwanzo wa mechi mbili za ‘back-to-back’ bab’ kubwa itakayohusisha washindi wa Mozzart Bet Cup Kakamega Homeboyz.

Msimu haujaanza vizuri kwa vijana wa Patrick Odhiambo wakipoteza mchezo wao wa kwanza kwa bao 1-0 mikononi mwa wageni wa ligi, Murang’a Seal ikiwa ni siku chache tu baada ya kutolewa kwenye ngarambe za Kombe la Shirikisho Afrika.

Homeboyz wikendi hii wanawakaribisha mabingwa wa zamani FKFPL Tusker FC kwenye uga wa Bukhungu, Kaunti ya Kakamega na kisha wiki ijayo kuwa wenyeji wa mabingwa watetezi Gor Mahia.

Ni mechi mbili ambazo zinatajwa kutoa mwelekeo wa uimara wa Homeboyz ikiwemo nia yao ya kutwaa ubingwa wa FKFPL kwa mara ya kwanza hususan baada ya kushinda taji la Mozzart Bet iliyowafanya kuonja mashindano ya kimataifa.

Wapo wachanganuzi wanaotabiri mmliki wa Homeboyz, Cleophas Shimanyula, huenda akafanya maamuzi magumu kwenye benchi la ufundi kama Homeboyz haitazinduka katika gemu hizo mbili ngumu hivyo kumaanisha timu itakuwa na mkufunzi mpya watakaposafiri kwenda Mombasa kuikabili Bandari FC.

Hata hivyo, kocha Odhiambo bila shaka atatarajia fomu ya vijana wake kurudi kama ilivyokuwa msimu uliyopita ambapo waliwapiga Tusker FC na kutwaa ubingwa wa Mozzart Bet Cup na kama hiyo haitoshi wakawatandika K’Ogalo kiasi cha kuwacheleweshea ubingwa wa FKFPL.