Tusker FC yajichimbia Arusha kujiwinda na Ligi Kuu Kenya

MABINGWA mara 12 wa Ligi Kuu nchini Kenya (FKF), timu ya Tusker FC inaendelea na kambi ya wiki moja jijini Arusha ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya 2023/24 unaotazamiwa kuanza Agosti 26 mwaka huu.
 
Timu hiyo inafanya mazoezi katika uwanja wa Aga Khan uliopo Ngaramtoni huku ikiwa na sura mpya kadhaa za usajili akiwemo kiungo Fabien Adikiny aliyesajiliwa kutoka Murang’a Seal, wachezaji wawili wa zamani wa Nzoia Sugar,James Kibande na Joseph Mwangi, winga kutoka nchini Uganda John ‘Tooki’ Byamukama pamoja na kipa Edwin Simiyu ambaye amepandishwa kutoka timu ya vijana.

 
Lakini pia Tusker FC inakosa nyota wake Humphrey Mieno,Jackson Macharia, beki Mtanzania Kalos Kirenge, mshambuliaji David Majak Chan kutoka Sudan Kusini pamoja na kiungo Shami Kibwana ambao wameachana na timu hiyo.
 
Katika kutesti mitambo ili kumsaidia mwalimu Robert Matano kupata kikosi cha kwanza pia kuona kuna sehemu gani za kufanyia marekebisho kabla ya Ligi kuanza Tusker FC itacheza mechi za kirafiki na Mbuni FC inayoshiriki Ligi ya Championship lakini pia Vital’O ya Burundi ambayo nayo inatazamiwa kuwasili jijini hapa muda wowote kutoka sasa.
 
Timu nyingine ya Ligi Kuu ya Kenya ,Kenya Police FC nayo iliweka kambi hapa mkoani Arusha ambapo ilicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Singida Fountain Gate na Namungo FC, katika uwanja wa Black Rhino iliyoko Karatu na zote ikitoka sare ya 1-1,kabla ya kusafiri hadi Rwanda kucheza na Rayon Sports na kushinda goli 1-0.
 
Mbali na timu hiyo pia Bandari FC nayo ilikuwa Tanzania ambapo ilicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Coastal Union FC katika uwanja wa Mkwakwani Tanga ikishinda goli 1-0,kabla ya kupokea kipigo cha goli 2-0 kutoka kwa Azam FC katika uwanja wa Azam Complex.
 
Kakamega Homeboyz nayo ni timu nyingine ya Ligi Kuu ya Kenya ambayo ilisafiri nje ya nchi kwa mechi ya kirafiki, walipoalikwa kuhudhuria sherehe za kuadhimisha siku ya kuanzishwa kwa timu ya KCCA ya Uganda iliyofanyika Ijumaa iliyopita, ambapo ilipoteza kwa wenyeji wao Kampala City Council Authority (KCCA),goli 2-0.
 
Apollo Benjamin ni mdau wa Soka Arusha anasema timu za Kenya kuja kuweka  kambi  nchini kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu ya huko kwao inamana  kubwa sana kwao na hata kwetu Tanzania kwa kuwa hivi sasa  hali ya mwamko wa soka kwa Tanzania ni mkubwa kuliko Kenya na pia hata katika suala la viwango vya soka Tanzania bado ipo juu.