Oyoo amerudi kuibua wapya

ALIYEKUWA kocha wa Thika Queens FC, Joseph Oyoo, amerudi Mombasa na kuamua kuanzisha timu ya wasichana kuanzia umri wa miaka 10 hadi 15 kwa nia ya kuwakuza na kuwafanya wawe na vipaji vya kuchezea timu ya taifa ya Harambee Starlets.

Akiongea na MWANASPOTI kwa njia ya simu, Oyoo alisema ameonelea umuhimu wa kuanzisha timu ya wasichana wadogo kwasababu ya kuwatengeneza na kuwa mastaa kama walivyokuwa wanasoka wake wa awali ambao wengine hivi sasa wanacheza soka la kulipwa majuu.

“Nimeonelea nirudi kwa timu yangu ya Mombasa Olympic Ladies FC lakini nitaanzisha timu ya wasichana wadogo niwakuze sawa nilivyofanya kina Mwanahalima Adam, Nuru Mustafa, Winnie Achieng na wengineo amabao sasa wanacheza soka nchi kadhaa za nje,” alisema.

Kocha huyo alisema timu ya wachezaji wakubwa ya Mombasa Olympic Ladies FC inayoshiriki Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza itaendelea kusimamiwa na kocha Christine Nanjala na kamwe hatataka kuingilia majukumu yake akiamini anaweza kuifanikisha.

Oyoo ni mmoja wa makocha ambao walianzisha soka la wanawake nchini na ametoa wachezaji wengi wanaoichezea Harambee Starlets japo hajapata bahati ya kutambuliwa na maofisa wa mchezo huo nchini.