Naibu Kocha Ingwe amkosoa Kocha Aussems

HAITOKEI mara nyingi kumsikia naibu kocha akimgeuzia lugha kocha mkuu. Ndivyo ilivyo kwa sasa pale AFC Leopards.
Baada ya kuanza msimu mpya wa ligi kuu kwa ushindi dhidi ya Tusker, matokeo ya Ingwe yameenda yakididimia.
Walishikwa sare tasa na KCB, kisha wakafinywa na mashemejio Gor Mahia kwenye mechi iliyofuata halafu wikendi iliyopita wakaumwa na Bandari FC.
Matokeo haya yamemwacha kocha Mbelgiji Patrick Aussems hoi huku akiwataka mashabiki wa Ingwe na uongozi kutotegemea kushindania taji la ligi kuu msimu huu.
Aussems amelazimika kukisuka kikosi kipya kwa kuwapandisha daraja wachezaji wa timu chipukizi. Hii ni baada ya kuwapoteza zaidi ya wachezaji 17 waliomuundia kikosi chake cha kwanza msimu uliopita.
Ingawaje kikosi hiki kimeonyesha mshikamano, Aussems amefunguka na kusema wanachohitaji ni mastraika lau sivyo, hamna  la maana wanaloweza kufanya msimu huu.
Baya hata zaidi ni kuwa Ingwe wana kikwazo cha kutosajili walichowekewa na FIFA baada ya kushtakiwa na makocha na wachezaji wao wa zamani kwa kukosa kuwafidia baada ya kuwavunjia mikataba yao kinyume na utaratibu ufaao.
Uongozi wa Ingwe umekuwa ukidai kuwa tayari umeanza utaratibu wa kuwafidia wanaowadai ili waweze kuondolewa marufuku hiyo na FIFA. Lakini mpaka sasa bado hawajafanikiwa ishara kuwa hamna la maana walilofanya. Kocha Aussems anasisitiza bila usajili wa wachezaji wachache wazoefu, hamna watakaloweza kufanya.
Mpaka sasa Ingwe hawajasajili mchezaji yeyote huku dirisha la usajili likiwa limesalia na siku tatu lifungwe.
Lakini licha ya mtazamo huu wa kocha Aussems, naibu wake Tom 'Gaza' Juma katofautiana nao kwa kusema kuwa kikosi chao bado tu kinaweza kutoa ushindani wa maana na hata kushinda  taji.
"Kinachotakiwa ni kuwapa wachezaji hawa chipukizi muda. Ndio watakosea lakini katika kufanya hivyo watajifunza. Ndivyo mchezaji hupata uzoefu." Juma anasema.
Kulingana na utathmini wake wa mechi mbili walizopoteza mfululizo wakilimwa 1-0 na Gor na kisha 2-1 na Bandari, kikosi chao chipukizi kilidhihirisha wazi kuwa kinazidi kuimarika.
"Dhidi ya Bandari ilikuwa kabisa ni kama tutachapa come-back katika zile dakika za mwisho wa mchezo kwa namna tulivyopambana hadi mwisho baada yao kutangulia kufunga magoli yao yote. Tuwape muda vijana, watasumbua msimu huu." Juma kasisitiza.