Mulee ampiga sapoti Wanyama

KOCHA  Jacob Ghost Mulee kampiga sapoti Victor Wanyama kuhusiana na azma yake ya kugombea wadhifa katika Shirikisho la soka nchini FKF
Mapema wiki hii nahodha huyo wa zamani wa Harambee Stars alitangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya kukosa kuitwa kikosini kwa miaka miwili.
Tangazo lake lilijiri wiki mbili baada ya kocha Mulee naye kujiondoa kama mkufunzi wa timu hiyo ikiwa ni baada ya miezi 11 toka alipoteuliwa kwa mara ya tano kuifunza Stars.
Mulee ambaye ndiye aliyemwita  Wanyama katika kikosi cha taifa kwa mara ya kwanza 2007,  kammiminia sifa baada ya kuweka wazi kwamba angependa kuingia FKF baada ya kustaafu soka kwa ujumla.
"Kwa wachezaji niliofunza, Wanyama ni moja kati ya wenye nidhamu ya hali ya juu. Lakini pia mchango wake kwa soka la Kenya ni mkubwa mno hivyo ni wazo zuri kumwona akiwa na mawazo ya kujitosa kwenye siasa ya uongozi wa  soka sababu najua, ni mwadilifu na mchapa kazi." Ghost kasema.
Licha ya kutoamua kumrejesha kikosini  alipoteuliwa kocha wa Stars Oktoba mwaka jana, Ghost anasisitiza kuwa hana tatizo kabisa na Wanyama.
Uamuzi huo wa kumtema na hata kumpokonya unahodha na kumpa Michael Olunga, ulizua minongóno kibao huku Ghost akionyesha kuchukizwa kila alipoulizwa sababu za kumwacha nje.
"Watu wanasahau kuwa ni mimi ndiye niliyempa nafasi yake ya kwanza kuichezea Stars 2007 dhidi ya Nigeria. Nilimchezesha kama striaka kwenye mechi hiyo ya kirafiki na alicheza vizuri sana." Ghost kaongeza.
Ikiwa atachukua mkondo huo, Wanyama atakuwa amefuata katika yayo za malejendi Didier Drogba na Samuel Eto'o ambao wote wamejitosa kwenye  uongozi wa Mashirikisho ya soka ya mataifa yao, wote wakiwania Urais.