MATANO: TUSKER TUSHAIVA, WALETENI SASA DJIBOUTI

KOCHA Robert Matano kadai kikosi chake sasa kimeiva baada ya kambi ya wiki moja  Mombasa, na sasa wapo tayari kuchuana na Arta Solar 7, Jumamosi wiki hii.
Baada ya kubeba taji la ligi kuu msimu wa 2020/21 mara moja Matano alianza maandalizi ya msimu ujao.
Matano alianza kwa kuwatema wachezaji 11 na kusajili wengine 11 wapya. Kisha alifunga safari hadi Mombasa na kikosi hicho kwa kambi ya wiki moja.
Sababu ya kuipeleka kambi Coast, Matano anasema alihitaji sehemu tulivu  ili aweze kuianisha kikosi chake baada ya kufanya usajili huo mkubwa uliozua gumzo miongoni mwa wakereketwa na mashabiki wa soka nchini.
"Raundi hii tuna kikosi dhabiti zaidi hasa baada ya yale mabadiliko makubwa tuliyoyafanya. Kwa wiki nzima tuliyokuwa Mombasa, tulikuwa tunaivisha timu. Nimeridhishwa kabisa na jinsi wachezaji wapya walivyoweza kuunda mwingiliano mzuri tena kwa haraka na wenzao waliowakuta kikosini." Matano anasema.
Kuhusu maandalizi ya mechi ya Jumamosi kule ugenini, Matano kasisitiza kuwa wapo tayari kukabiliana na Arta anayoichezea kiungo wa zamani wa Arsenal  Alex Song.
"Tumeiva, tupo tayari waje tu. Ndio ilikuwa sababu yetu kuweka kambi ya wiki nzima kule Mombasa. Tulihitaji sehemu tulivu  pasipo na usumbufu kwa ajili ya maandalizi yetu na ndio sababu tulikwenda Coast. Tushatimiza malengo yetu yote ya kambi hiyo, tuko tayari." Matano kachocha.
Matano na Tusker yake sasa wanajipanga kurejea Nairobi ili kujiandaa kufunga safari kuelekea Djibouti kwa ajili ya mchuano huo wa raundi ya kwanza ya mtuano. Baada ya kukipiga huko, timu hizo zitachuana tena wiki moja baadaye jijini Nairobi. Kando na kusaka mandhari tofauti ya maandalizi, uamuzi wa kukikata kambi Mombasa ulikuwa pia wa kuwawezesha wachezaji kuizoea hali ya anga  ya Coast ambayo ndiyo watakayokumbana nayo huko Djibouti.