Mabingwa Tusker FC kujengwa Ksh2 milioni

KABLA yake kutimuliwa uongozini kimabavu, Rais wa zamani wa Shirikisho la soka nchini FKF, Nick Mwendwa alikuwa ametoa ahadi ya kumzawadia bingwa wa ligi kuu msimu huu 2021/22 Ksh5 milioni.
Hii ilikuwa ni nyongeza  ya kile kiasi cha Sh3.5 milioni kilichokuwa kipewa bingwa miaka  ya hapo awali ligi ilipokuwa chini ya uongozi wa kampuni ya Kenya Premier League Limited, iliyoendesha ligi kwa niaba ya FKF.
Lakini baada ya serikali kuchukua uongozi wa soka baada ya kivunja afisi ya FKF na kumfukuza Mwendwa kwa madai ya ufisadi nauongozi mbaya, mambo yamebadilika.
Sasa bingwa wa msimu  huu uliomalizika juzi Jumamosi, Tusker FC atapokea Sh2 milioni tu.
Kamati ya Mpito  inayosimamia  soka nchini imetoa tamko kuwa itawazawadia mabingwa hao Sh2 milioni huku Sh1 milioni ikiwaendea mabingwa wa ligi kuu  ya kina dada.
Wasupa Vihiga Queens waliomaliza msimu bila ya kupotea mechi hata moja, walitawazwa mabingwa baada ya kuwafinya Bunyore FC 2-1.
Kiasi hicho cha Sh2 milioni kinatarajiwa kuzua minong'ono kutokana na kupungua kwa fedha hizo ikizingatiwa kuwa msimu uliopita Tusker walipokea Sh5 milioni kutoka kwa FKF.
Robert Matano ambaye katishia kuigura klabu hiyo akidai kukosea heshima na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo, aliwaongoza Tusker kutetea ubingwa wao kwa kuwalima Posta Rangers magoli 2-0 kwenye mechi yao ya mwisho ya msimu.
Tusker waliibuka mabingwa kutokana na tofauti ya idadi ya magoli manne mbele ya Kakamega Homboyz waliotoshana alama 63.