Kwani mabao ya Omala hayambambi Firat?

MOJA ya maswali ambayo mafans wa soka wamekuwa wakijiuliza ni vigezo vipi ambavyo kocha mkuu wa timu ya taifa, Harambee Stars, Engin Firat, anatumia katika uteuzi wa kikosi chake.

Kwa mara nyingine tena, kocha huyu raia wa Uturuki amefungua mijadala kwenye mitandao ya kijamii na vijiweni baada ya kutangaza kikosi cha Harambee Stars kinachotazamiwa kuingia kambini Jumatatu wiki ijao kwa ajiliya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Urusi.

Mechi hii itachezwa Jumatatu Oktoba 16 mwaka huu ambayo ni wiki ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na ina umuhimu wake katika kuboresha viwango vya soka vinavyotolewa na FIFA.

Harambee Stars iliondolewa gemu za kufuzu Kombe la Afrika zitakazofanyika mapema mwakani nchini Ivory Coast kutokana na kutumikia kibano cha FIFA lakini tangu warudishwe katika soka la kimataifa, Shirikisho la Soka Kenya (FKF) limekuwa likiwaandalia mechi zenye hadhi.

Tayari kwenye mechi za kalenda za FIFA zilizopita, Harambee Stars imecheza na Iran ambayo ilikipiga Kombe la Dunia mwaka jana na Qatar waliyoandaa dimba hilo la dunia na sasa wanapanga kucheza na Urusi waliyokuwa wenyeji wa Kombe la Dunia 2018.

Mechi hizi zote za kirafiki ni mahususi kwa kocha Firat kuandaa kikosi chake kwa ngarambe za kufuzu Kombe la Dunia 2026 ambapo mechi ya kwanza ya Harambee Stars itakuwa dhidi ya Gabon Novemba mwaka huu na kisha kuwavaa Ushelisheli.

Ndoto ya mafans na wadau wa soka humu nchini ni kuona Harambee Stars inaweka historia kufuzu Kombe la Dunia zitakazoandaliwa kwa ushirikiano wa nchi tatu za Marekani, Canada na Mexico.

Aidha baada ya Kenya kutunukiwa uwenyeji wa Kombe la Afrika 2027 pamoja na mataifa jirani ya Tanzania na Uganda, mafans wametaka kuona Firat anakisuka kikosi imara kilichosheheni wachezaji chipukizi wenye vipaji.

Hata hivyo, kila anapoteua kikosi cha Harambee Stars, maneno yamekuwa mengi huku mafans wakihoji kuachwa baadhi ya wachezaji ambao uwanjani wanaonekana kufanya vizuri.

Katika uteuzi wa kikosi cha Harambee Stars juzi Jumapili kwa mechi dhidi ya Urusi, Firat alimuacha straika Benson Omala ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita aliweka kambani mabao wote mawili na kuisaidia timu yake ya Gor Mahia kuibuka na ushindi kwenye Mashemeji derby.

Mabao hayo mawili ya Omala yanamfanya kufikisha mabao sita na kuongoza mbio za Kiatu cha Dhahabu msimu huu wa Ligi Kuu Kenya, lakini yanaonekana ni mabao ambayo hayajamshawishi kocha Firat kumjumuisha kikosini.

Firat aliwahi kumuita straika huyo wa K’Ogalo kwenye mechi dhidi ya Iran akiwa na wastani mzuri wa mabao kwa mechi alizocheza ila akamtema siku ya safari kwa kile watu wa karibu na kocha huo walidai alihitaji wachezaji wenye nguvu wanaoweza kuwasumbua mabeki na kutengeneza nafasi za timu kushambulia.

Inasemekana kocha Firat anataka wachezaji ambao wanaweza kuwania mipira ya hewani, kutumia nguvu na kasi kuwapita mabeki wa timu pinzani.

Straika mwingine ambaye hajajumuishwa kwenye safari ya Uturuki kwa kambi ya wiki moja kabla ya kuivaa Urusi ni Elvis Rupia ‘Machapo’ aliyeweka rekodi ya kufunga mabao mengi ndani ya msimu moja kwenye mikikimikiki ya FKFPL msimu uliyopita. Rupia anaendeleza rekodi yake tamu ya kufumania nyavu akiwa na timu yake mpya ya Singida Fountain Gate ya Bongo aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Kenya Police FC.

Mchezaji mwingine ambaye pia amekua na msimu mzuri hadi sasa ni kipa wa Posta Rangers, Samuel Njau, akiwa na cleansheet tano katika mechi sita za FKFPL.

Kipa huyo ameruhusu bao moja tu katika gemu ambayo Rangers walipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Sofapaka. 


KIKOSI CHA STARS

MAKIPA: Patrick Matasi, Brian Bwire, Bryne Odhiambo

MABEKI: Joseph Stanley Okumu, Brian Mandela, Johnstone Omurwa, Collins Sichenje, Erick Ouma, Rooney Onyango, Daniel Sakari, Vincent Harper, Amos Nondi

VIUNGO: Richard Odada, Anthony Akumu, Kenneth Muguna, Alpha Onyango, Ayub Timbe, Ovella Ochieng

MASTRAIKA: Masoud Juma, Alfred Scriven, Cliffton Miheso, Moses Shummah, Michael Olunga