K'Ogalo yabeba tena, Ingwe yapigwa nyumbani

Muktasari:

  • Bao moja la kipindi cha kwanza lililofungwa na Benson Omala na mengine ya kipindi cha pili yalitosha kuiweka bapaya Muhoroni katika janga la kushuka daraja kwani imesalia nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 28 bada ya kucheza mechi 31 hadi sasa.

HESABU zimekubali. Ndio, Gor Mahia imetwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) baada ya alasiri ya leo Jumapili kuinyuka Muhoroni Youth kwa mabao 3-0 na kufikisha pointi 67 zisizoweza kufikiwa na timu nyingine 15 za ligi hiyo iliyosaliwa na mechi za raundi tatu kabla ya kumalizika.

Bao moja la kipindi cha kwanza lililofungwa na Benson Omala na mengine ya kipindi cha pili yalitosha kuiweka bapaya Muhoroni katika janga la kushuka daraja kwani imesalia nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 28 bada ya kucheza mechi 31 hadi sasa.

Omala alifunga bao lake la 16 kwa msimu huu katika ligi hiyo na kuongoza orodha ya wafungaji sekunde chache kabla ya mapumziko kabla ya Boniface Omondi kuongeza bao la pili katika dakika ya 48 na wakati Muhoroni ikijiuliza itayarudisha vipi mabao hayo, Austine Odhimbo kapigilia chuma cha tatu dakika ya 65 na kuwakatisha tamaa wageni wa mchezo huo.

Hilo lilikuwa bao la 10 kwa Odhimbo na la 41 kwa timu hiyo inayofikisha jumla ya mataji 21 ya Ligi Kuu ya Kenya tangu mwaka 1968, ikiwa ndio kinara nchini humo. Gor Mahia imebeba ubingwa huo ikiwa na michezo mitatu mkononi, kwa kufikisha pointi 67 ambazo haziwezi kufikiwa na Tusker FC na Polisi Kenya zilizopo nafasi ya pili na tatu mtawalia, hata kama kila moja itashinda mechi tatu zilizosalia kabla ya kufungia msimu wa 2023-2024.

Huo ni ubingwa wa tatu mfululizo kwa wababe hao na kujikatia pia tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao, kwa ujumla ni ubinngwa wao wa 21.

Kipigo ilichopewa Muhoroni kimezidi kuiweka pabaya katika janga la kushuka daraja, kwani kwa sasa italazimika kushinda michezo mitatu iliyosalia ili kufikisha pointi zitakazoitoa katika janga hilo.

Kwa sasa timu hiyo ipo nafasi ya 17, juu ya Nzoia Sugar inayoburuza mkia ambayo leo imetoka suluhu na Nairobi City na kuifanya ifikishe pointi 19 na kutanguliza mguu moja katika shimo la kushuka daraja msimu huu, kwani hata ikishinda mechi tatu ilizonazo itafikisha pointi 28 ilizonazo Muhoroni na zilizopitwa na Shabana iliyopo nafasi ya 16 ikiwa na alama 29 kwa michezo 31 pia.

Katika mechi nyingine zilizopigwa pia leo, AFC Leopards ikiwa nyumbani ilifumuliwa bao 1-0 Bidco United, huku Bandari ikilazimishwa sare ya mabao 2-2 mjini Mombasa na Sofapaka na kuziacha timu hizo izikisaliwa na pointi ilizokuwazo awali kabla iya kushuka uwanjani.

Bandari imesalia nafasi ya nne na pointi 48, huku Ingwe ikishuka kwa nafasi moja kutokaa ya tano hadi ya sita ikisaliwa na pointi 47, moja zaidi na ilizonazo Nairobi City iliyobebwa na suluhu iliyopata ugenini kwani imeifanya ifikishe pointi 48 kama za Bandari ila zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Bao lililoikatili Ingwe lilifungwa Samuel Ndungu katika dakika ya 66 na kuzima matumaini ya AFC, kuing'oa Bandari  nafasi ya nne ya msimamo wa ligi hiyo.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho kwa michezo miwili, Talanta itakuwa nyumbani kuikaribisha KCB, wakati Ulinzi Stars itaialika Muranga FC, mechi zote zikipigwa kuanzia saa 9:00 alasiri ili kukamilisha mechi za raundi ya 31.