GOR MAHIA NJIA NYEUPE CAF

Tuesday April 27 2021
gor pic
By Thomas Matiko

GOR Mahia watapata fursa nyingine ya kushiriki CAF Champions League msimu ujao hata ikiwa hawatafanikiwa kushinda ligi kuu msimu huu.
Msimu huu, Gor wamekuwa kwenye fomu mbovu sana jambo ambalo halijawahi kuwatokea katika misimu mitano iliyopita.
Kwa jinsi mambo yalivyo, Gor hawajaonyesha dalili zozote za kutetea ubingwa wao msimu huu, wakiwa wanasotea katika nafasi ya 10.
Wakiwa wamecheza mechi 13, Gor wamekusanya alama 19 pekee huku vinara Tusker FC waliocheza mechi 16 wakiwa na alama 36 wakifuatia na KCB FC wenye alama 30.
Na ingawaje zimesalia zaidi ya mechi 15 msimu huu umalizike, kuna uwezekano mkubwa sana kwamba Gor hawataweza kunyakua ubingwa tena.
Lakini licha ya hilo, huenda wao ndio watapewa fursa ya kushiriki CAF Champions League msimu ujao hata endapo hawataibuka mabingwa.
Hilo linaweza kutokea ikiwa tu msimu huu wa ligi utafutiliwa mbali. Kwa sasa msimu huo umesita baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuisitisha Machi 26, kufuatia kuongezeka kwa visa vya Covid-19 nchini.
Hii ni baada ya kuweka lockdown iliyoratibiwa kumalizika mwezi ujao Mei 29. Hata hivyo tayari Waziri wa Afya Mutahi Kagwe katia wasiwasi baada ya kudai kwamba kuna uwezekano lockdown ikaongezwa hata baada ya Mei 29, jambo ambalo litatishia kuvuruga kalenda ya soka nchini endapo itatokea hivyo.
Mambo yakiishia kuwa hivyo na Shirikisho la soka FKF lilazimike kufuta msimu huu kwa mara nyingine tena basi Gor ndio watakaoiwakilisha Kenya kwenye dimba la CAF na wala sio Tusker. Haya ni kwa mujibu wa Rais wa FKF Nick Mwendwa.
“Sheria zetu zinasema kuwa bingwa wa zamani ndiye atakayeiwakilisha nchi kwenye  mashindano ya Cecafa na yale ya Bara na hivyo nafasi hiyo itapewa Gor Mahia.” Mwendwa kakata kauli.
Mwendwa alifutilia mbali msimu uliopita 2019-20 mnamo Machi baada ya Kenya kupata  kisa chake cha kwanza cha Covid-19.
Hadi wakati anaifutilia mbali msimu huo, zilikuwa zimesalia mechi 10 msimu ufikie kikomo. Baada ya kuifutilia mbali, Mwendwa aliwatangaza Gor mabingwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo safari hii Mwendwa hana nia  ya kuifuta ligi mapema. Wapo wachanganuzi wanaodai ni kwa sababu kwa sasa ni FKF ndio inayoendesha ligi kinyume na msimu uliopita ilipokuwa chini ya KPL aliyoishi kulumbana nayo Mwendwa.
Mwendwa anasisitiza kuwa msimu huu unaweza kufikia kikomo endapo Rais Uhuru ataondoa lockdown kufikia mwisho wa Mei.
“Ikiwa lockdown itaondolewa mwishoni mwa Mei, basi ligi inaweza kuendelea kuanzia Juni hadi ikafikia kikomo na bado tu tutafanikiwa  kuanisha kalenda yetu na ile ya FIFA na Ulaya. Ombi letu kwa serikali ni waondoe marufuku hii mapema ili angalau michezo irejee na wanaozitegemea waache kuumia zaidi.” Mwendwa kaongeza.
Ikiwa FKF italazimika kufuta msimu huu, basi hakutakuwa na bingwa.  Kwa mujibu wa sheria ni lazima timu zote ziwe zimecheza nusu za mechi za msimu kufikia wakati uamuzi kama huo wa kufuta msimu unapochukuliwa.
Msimu wa FKF-PL una jumla ya mechi 34 kwa kila timu kucheza na hadi kufikia sasa hamna timu hata moja iliyocheza nusu ya mechi hizo ambazo ni michuano 17.


Advertisement