Gor Mahia inahesabu saa tu, kabla ya kutangaza ubingwa

Muktasari:

  • Kikosi hicho cha Kocha Johnathan McKinstry, kinatarajiwa kushuka uwanjani leo Jumapili saa 9:00 mchana kuvaana na Muhoroni Youth kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo, jijini Nairobi ikihitaji sare moja tu au ushindi kabisa utakaoifanya ifikishe pointi 67 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine za ligi hiyo inayoshirikisha klabu 18 zikiwamo Tusker na Polisi zilizokuwa zikifukuzia kwa muda mrefu.

WATETEZI wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Gor Mahia kwa sasa wanahesabu saa tu kabla ya kubeba taji la 21 na kuzidi kuboresha rekodi iliyonayo katika ligi hiyo iliyosaliwa na mechi za raundi tatu kabla msimu huu haujamalizika.

Kikosi hicho cha Kocha Johnathan McKinstry, kinatarajiwa kushuka uwanjani leo Jumapili saa 9:00 mchana kuvaana na Muhoroni Youth kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo, jijini Nairobi ikihitaji sare moja tu au ushindi kabisa utakaoifanya ifikishe pointi 67 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine za ligi hiyo inayoshirikisha klabu 18 zikiwamo Tusker na Polisi zilizokuwa zikifukuzia kwa muda mrefu.

Huo utakuwa ni mchezo wa 31 kwa timu zote, huku Muhoroni iliyopo nafasi ya pili kutoka mkiani ikihitaji ushindi ili kujinusuru na janga la kushuka daraja wakati wenzao wakitaka kubeba taji la pili mfululizo na la 21 katika historia ya ligi hiyo na klabu hiyo kwa ujumla kwani kwa sasa ina mataji 20.

Gor Mahia iliyoanzishwa Februari 17, 1968 imetwaa mataji ya awali katika misimu ya mwaka 1968, 1974, 1976, 1979, 1983, 1984, 1985, 1987, 1990, 1991, 1993, 1995, 2013, 2014, 2015, 2017, 2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2022-2023.

Hata hivyo, rekodi zinaonyesha tangu mwaka 2018 katika mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu kwa timu hizo, Muhoroni haijawahi kupata ushindi mbele ya K'Ogalo, zidi ya kuambulia sare mbili tu na kufungwa michezo minane, ukiwamo wa duru la kwanza msimu huu ilipokubali kipigo cha mabao 2-0.

Kutokana na takwimu hizo, ni wazi Muhoroni yenye pointi 28, baada ya kushinda michezo mitano tu kati ya 30 iliyocheza hadi sasa, itakuwa na kazi ngumu mbele ya wababe hao ambao katika mechi 30 iliyoicheza imeshinda 18 na kutoka sare 10, huku ikipoteza mara mbili tu, ikiwa timu iliyopoteza michezo michache zaidi kwa msimu huu.

Awali Gor ilikuwa inaisikilizia Polisi FC iliyokuwa nafasi ya pili wakati ilipoialika Tusker Kenya jioni ya leo na kwa bahati mbaya maafande hao walikubali kipigo cha bao 1-0 na kuporomoka hadi nafasi ya tatu ikisaliwa na pointi 54 kwa michezo 31 ikiipisha Tusker iliyofikisha pointi 56.

Timu hizo mbili zimesaliwa na michezo mitatu kila moja na kama zitashinda mechi hizo, Tusker itakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 65 tu, huu Polisi itavuna alama 63, wakati Gor tayari kwa sasa imeshakusanya jumla ya pointi 64 na sare itaifanya ifiishe 65 na kubebwa na mabao iliyonayo kwa sasa na iwapo itaifumua Muhoroni itamaliza udhia kabisa kwa kutangaza ubingwa rasmi.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa jioni ya leo, Posta Rangers ilipata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Kakamega Homeboyz, huku jahazi la Shabana likizidi kuzama ikiwa ugenini baada ya kunyukwa mabao 2-1 na Kariobangi Shark katika pambano kali, ambalo wageni walitangulia kupata bao kabla ya wenyeji kupindua meza kipindi cha pili na kuibuka na ushindi huo.

Matokeo hayo yameifanya Shabana kusalia nafasi ya 16 katika msimamo wa timu 18 ikiwa na pointi 29, wakati Kariobangi ikichupa hadi nafasi ya nane ikifikisha pointi 44 sawa na Kakamega, ila ikibebwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mbali na mchezo wa K'Ogalo na Muhoroni unaosubiriwa na hamu na mashabiki wa Gor kutaka kuona timu hiyo ikitangaza ubingwa mapema ikiwa na michezo mitatu mkononi, pia kuna michezo mingine mitatu itapigwa ukiwamo wa mapema saa 7 mchana wakati vibonde, Nzoia Sugar watakapoialika Nairobi City, huku Bandari kuialika Sofapaka mjini Mombasa na Ingwe, AFC Leopards itaikaribisha Bidco United.

Kesho Jumatatu, ligi hiyo itahitimisha mechi za raundi ya 31 kwa michezo miwili yote ikipigwa saa 9 mchana, Talanta FC itaikaribisha KCB na maafande wa Jeshi la Kenya, Ulinzi Stars itakwaruzana na Muranga.