Freemason yamweka pabaya Rachier

MAFANS wa mabingwa wa kihistoria, Gor Mahia, wamemkalia kooni Mwenyekiti wao Ambrose Rachier wakitaka ajiuzulu baada ya kukiri hadharani yeye ni mwanachama wa Jumuiya ya Freemason.
Barua inayosambaa mitandaoni ikiwa na saini ya aliyekuwa Katibu Mipango wa Gor Mahia, Judith ‘Nyangi’ Anyango, imewataka mashabiki kukongamana leo jijini Nairobi kufanya maandamano ya amani kumshinikiza ajiuzulu.
Nyangi kwenye barua hiyo alisema mafans wanakusudia kufanya maandamano yao kwenye Bustani ya Uhuru kwa lengo la kujitenga na alichosema Rachier ambayo imewafanya wadhihakiwe.
Baadaye wataelekea ofisi za mwenyekiti huyo zilizopo Jumba la Mayfair na kuwasilisha ujumbe wao wakimtaka akae pembeni.
“Kama mashabiki wa Gor Mahia FC, tutashiriki maandamano ya amani ili kujitenga na kauli ya Rachier baada ya kukiri kuwa mwanachama wa Freemason. Gor Mahia FC si sehemu ya Rachier katika safari yake ya Freemason. Tunataka kulaani vikali kuendelea kwake kuhusishwa na klabu hii,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.
Mapema mwezi huu katika mahojiano na NTV, Rachier alibainisha yeye ni mwanachama wa Freemason ambacho kwa Wakenya wengi kinahusishwa na ‘utajiri wa kimizengwe’ pasipo kuegemea dini yoyote.