Buda! Usipojipanga FKFPL utapangwa tu

ETI kocha Antony ‘Modo’ Kimani ana presha Bandari FC? Labda kama utakua hauna habari alichokifanya mwishoni mwa wiki iliyopita na Nzoia Sugar wasee msiwachukulie poa.
Kimani alifanya kile ambacho makocha wengine sita msimu huu wameshindwa kukifanya nacho ni kuzipiga breki spidi kali ya Tusker FC ili kuwadhibitishia kuwa hata wao wanafungika.
Bandari FC ilianza wikendi ikiwa nafasi ya 12 lakini ushindi dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Kenya, Tusker FC, uliwafanya kupanda nafasi moja juu na kupunguza presha kwa Kimani ambaye tangu ashinde mechi ya ufunguzi dhidi ya Sofapaka, alipoteza michezo mitatu na kutoka sare mbili.
Mchezo huo wa Jumapili katika dimba la Mbaraki jijini Mombasa ulikua na matokeo ya kuridhisha kwa wenyeji ambao kabla ya kuwavaa Tusker FC walikuwa wamepoteza mabao 3-1 dhidi ya Posta Rangers kwenye uwanja huo huo.
Kupoteza mchezo huo kwa Tusker FC kunawafanya kupunguza gepu lao la pointi na Nzoia Sugar inayokimbiza ‘mwizi’ kimya kimya.
Tusker FC bado wapo kileleni na pointi 18 wakiwazidi kwa pointi moja Nzoia Sugar ambayo ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Kakamega Homeboyz kwenye Uwanja wa Sudi kaunti ya Bungoma.
Kocha wa Nzoia Sugar, Salim Babu, aliwahi kunukuliwa akisema vijana wake watakua kwenye presha pindi watakapokamata usukani wa FKFPL na kutaka kuhakikisha wanabaki hapo hapo hadi mwisho wa msimu.
Kama sio sare dhidi ya majirani zao Homeboyz basi Nzoia Sugar sasa hivi ndiyo wangekuwa kileleni laiti wangetoka Uwanja wa Sudi na pointi zote tatu.
Timu nyingine inayoonekana kuimarika ni Kenya Police FC chini ya kocha mpya Francis Baraza akirekodi ushindi wake wa pili mfululizo baada ya kuwapiga Kariobangi Sharks mabao 2-1.
Ama kwa hakika ilikuwa siku mbaya kwa makocha Robert ‘Simba’ Matano wa Tusker FC na William Muluya wa Sharks kwani ni wao pekee ambao timu zao zilikua hazijapoteza mchezo wowote wa FKFPL msimu huu.
AFC Leopards waliyoonyesha matumaini ya kuzinduka kufuatia ushindi dhidi ya Nairobi City Stars lakini mwishoni mwa wiki walipigwa na kitu kizito kufuatia kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Bidco United.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Ingwe waliwabana Bidco kwa sare ya bao 1-1 lakini walipoteana kipindi cha pili na kuruhusu mabao matatu.
“Wachezaji wangu hawakufanya vizuri na tuliruhusu mabao mepesi katika mchezo na hii haifurahishi kabisa,” alisema kocha wa Leopards, Patrick Aussems.
Wakati Ingwe wakipoteana, Gor Mahia walizinduka kutoka kichapo cha KCB na kuishindilia Rangers mabao 2-0 nyota wa mchezo akiwa straika kinda Benson Omalla akitupia mabao yote na kumfanya kufikisha mabao sita.
Wikendi imekuwa tamu kwa Vihiga Bullets wakipata ushindi wao wa kwanza msimu huu baada ya kuwafinya City Stars bao 1-0 na kuendelea kuizamisha jahazi ya kikosi cha Nicholas Muyoti ambayo pamoja na Mathare United na Wazito FC wanasaka ushindi wa kwanza msimu huu.