Buda! Aussems hacheki na mtu

KOCHA Patrick Aussems amemchuja mchezaji wa pili ndani ya wiki moja kwenye kikosi chake baada ya kumfahamisha beki Joachim Oluoch hatamhitaji msimu huu.
Aussems ambaye anajulikana kwa uwazi wake, tayari amempiga marufuku Oluoch kuhudhuria kambi yake ya mazoezi akimtaka kutafuta klabu nyingine.
“Kocha alimtimua Jumamosi baada ya mechi ya kirafiki dhidi ya APS Bomet. Alimtamkia wazi wazi kwamba hamhitaji na wala hana mipango naye hivyo akimshauri asake klabu nyingine. Ishu sasa inashughulikiwa na menejimenti kuona ni vipi mkataba wake nao uliokuwa umesalia na mwaka mmoja, utakavyositishwa,” kimeeleza chanzo chetu kutoka ndani ya klabu.
Oluoch alijiunga na Ingwe Septemba 2 mwaka jana akitokea Gor Mahia na kusaini mkataba wa miaka miwili.
Kwenye mzunguko wa kwanza wa FKFPL msimu uliopita, Oluoch alikuwa muhimili mkubwa wa timu lakini mambo yakabadilika kwenye mzunguko wa pili alipoanza kuwekwa benchi na hata kufikia wakati, kocha alimwacha nje ya kikosi chake kwa ujumla.
Inadaiwa Oluoch alizenguana na Aussems jambo ambalo limempelekea Mbelgiji huyo kuchezesha fimbo akiwa mchezaji wa pili kuonyeshwa mlango wa kutokea baada ya straika John Makwatta huku awali alipojiunga na Ingwe alishwahi kutibuana na beki Robinson Kamura na kumvua unahodha kabla ya mchezaji huyo kuomba kuondoka.