Tusker mguu ndani, nje kimataifa

Tusker mguu ndani, nje kimataifa

MUDA sio rafiki kwa mabingwa wa Ligi Kuu Kenya, Tusker FC, kuhusu ushiriki wao wa msimu huu michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

 Tusker FC wanatambulika na CAF kama mabingwa wa Kenya msimu uliopita na watakaoiwakilisha taifa katika michuano mikubwa ngazi ya klabu lakini rungu la Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) inawaweka Wanamvinyo hao njiapanda.

FIFA imeisimamisha Kenya uanachama kwa muda usiojulikana baada ya tukio la Novemba mwaka jana Serikali ilipoivunja Shirikisho la Soka Kenya (FKF) na kuteua Kamati Shikilizi kitendo ambacho kilitafsiriwa kuingilia shughuli za soka.

Tayari Kenya ishaonja machungu ya uamuzi wa FIFA kufuatia timu za taifa wanaume, wanawake na wasichana kushindwa kucheza michezo muhimu kufuzu Kombe la Afrika na Vihiga Queens kushindwa kutetea ubingwa wa Klabu Bingwa CECAFA ambayo ingewahakikishia kucheza kwa mara nyingine tena Ligi ya Mabingwa Afrika Wanawake.

Uongozi wa Tusker FC pamoja na kocha Robert ‘Simba’ Matano waliwahi kunukuliwa wakieleza imani yao suluhu itapatikana ili wacheze Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

CAF inatarajiwa kupanga ratiba kwa mechi za mchujo kutinga makundi Agosti 25 mwaka huu huku mechi za awali zikiratibiwa kuanza mapema mwezi ujao.

Tusker FC wamekuwa mazoezini kujiandaa na michuano ya kimataifa pamoja na msimu mpya wa FKFPL uliopangwa kuanza Agosti 27 mwaka huu.

Wakati Tusker FC ikiwa bado gizani ushiriki wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Tanzania itakilishwa na timu mbili ambazo ni mabingwa Ligi Kuu Bara Yanga na Simba nao Vipers wakipeperusha bendera ya Uganda huku wawakilishi wa Rwanda ni APR.