Zayd: Kurudi Bongo maamuzi magumu

KUNA wakati binadamu hujivika ujasiri na kufanya maamuzi magumu ‘kujilipua’ bila kujali nini watu wanasema.

Hata Yahya Zayd ilibidi afanye hivyo. Uvumilivu ulimshinda na kuomba kurudi nyumbani Tanzania acheze kokote kwa mkopo ili aweze kujipanga upya pengine anaweza kupiga hatua kubwa zaidi.

Miaka miwili iliyopita, Zayd alifungua ukurasa mpya kwenye safari yake ya soka baada ya kujiunga na moja ya miamba ya soka nchini Misri, Ismaily. Hata hivyo, tofauti na matarajio yake, alijikuta akigeuka mtalii kwenye nchi hiyo yenye vivutio vikubwa vya utalii ikiwamo majengo ya Pyramid.

Anasema akiwa nchini huko kwenye timu yake, hakuwa akipata nafasi ya kucheza kabla ya kupelekwa Pharco FC kwa mkopo, ingawa mambo yalikuwa yale yale, ndipo alipoamua kuchukua maamuzi magumu na mengine mengi anayoyasimulia hapa Boda 2 Boda.

“Kwangu ulikuwa uamuzi mgumu, niliamua kurudi bila ya kuangalia nani atasema nini kwa sababu sikuwa nikipata nafasi ya kucheza. Sikuona umuhimu wa kuendelea kung’ang’ania kule. Siwezi kuficha kuwa ni ndoto yangu kucheza nje ya nchi lakini mambo yanapokuwa hayaendi sio mbaya kurudi na kujipanga tena,” anasema na kuongeza;

“Mwanzoni niliona ni kipindi cha muda mfupi, nilikuwa nikipambana mazoezini lakini sikuwa nikipata nafasi ya kucheza, najua watu wanaweza kunichulia tofauti ila najua ninachofanya na siwezi kusema kila kitu kwa sababu nitakuwa nikiwakatisha moyo wengine.”

“Unajua kila mchezaji amekuwa akikumbana na changamoto za namna yake, lakini kwangu niliona imetosha na ndio maana nikaona nirudi kwanza nyumbani.”

Anasema mkataba wake na Ismaily utamalizika mwishoni mwa msimu, hivyo anaweza kujiunga moja kwa moja na Azam.

“Muda wangu wa mkopo ukimalizika itanibidi nirudi kule kwa ajili ya kuwasilikiza nao, lakini sidhani kama nitaongeza mkataba kwa sababu maisha ya kule nimeshindwa kuyaelewa. Nadhani wachezaji wa kigeni Tanzania wanainjoi sana maisha.”

“Nilikuwa nikipata nafasi ya kuongea na Himid lakini haikuwa mara kwa mara kwa sababu miji ambayo tulikuwa tukikaa ni mbalimbali, alikuwa akinishauri kama mdogo wake na maamuzi haya hayakuwa kwa shinikizo lake niliamua binafsi,” anasema winga huyo.

Akiwa Misri, Zayd alipata nafasi ya kucheza kwenye michezo mitatu tu na hakuanza alikuwa akiingia ambayo ni dhidi ya Harras El Hodoud, Wadi Degla FC na Ittihad Alexandria, kwenye michezo mingine aliishia kukaa benchi huku wakati mwingine akiachwa kabisa kikosini kwa jina lake kutokuwekwa hata kwa wachezaji wa akiba.

“Kuna muda nilikuwa nakaa ndani na kuwaza kwa nini siaminiwi na kupewa nafasi lakini nilikuwa sipati majibu. Kuna watu huwa wanaamini kufanya kazi sana ni jambo muhimu na zuri kwa mchezaji, nilikuwa nikifanya kazi kwa kujituma ila bahati nadhani haikuwa upande wangu tofauti na wachezaji wengine,” anasema.

“Kijumla sikuwa nikiona kupiga kwangu hatua nikiwa kule. Sikutaka watu kunisifia kuwa jamaa anacheza nje kila siku napanda ndege kwenda na kurudi halafu hakuna wanachoona uwanjani. Sikuwa nikipata kabisa nafasi ya kucheza, ni hatari kwa kipaji changu,” anasema.

Zayd anaamini pengine haikuwa bahati kwake kufanikiwa akiwa na miamba hiyo ya soka la Misri.

“Naweza kuwa hapa halafu nikaondoka tena na kwenda sehemu nyingine, kushindwa Misri hakuna maana naweza kufeli pia sehemu nyingine.”

Akiongelea dabi ya Cairo kati ya Al Ahly SC dhidi ya Zamalek anasema ni zaidi ya dabi kama ilivyo kwa Simba na Yanga wakikutana, kuna kipindi huwa zinatokea vurugu mitaani, watu wanakimbizana ovyo hadi vyombo vya usalama huingilia kati.

“Nimeshuhudia dabi mbili, moja zilitokea vurugu mitaani, wakikutana ushindani huwa mkubwa sana uwanjani na hata nje ya uwanja baina ya mashabiki,” anasema.

Huyo ndiye Zayd ambaye anaamini kama lilivyo ua ambalo huchanua na kusinyaa basi kitendo cha kushindwa kufikia malengo yake akiwa Misri kilikuwa ni msinyao wake hivyo yupo mbioni kuchanua na kurejea kwenye masikio ya wadau wa soka la Tanzania.