Zarika atwaa ubingwa wa Dunia wa WBF

Dar es Salaam. Bondia Fatuma Zarika wa Kenya ametwaa ubingwa wa WBF baada ya kushinda kwa pointi dhidi ya mpinzani wake Patience Mastara wa Zimbabwe.

Zarika alishinda kwa pointi 97-93 kutoka kwa jaji Anthony Rutta ambapo Jaji Pendo Njau alimpa Zarika 98-92 na jaji alitoa pointi 98-92.

Pambano hilo lilikuwa la aina yake ambapo mabondia wote hao walionyesha uwezo mkubwa na kuwapa burudani ya kutosha mashabiki.

Mashabiki wengi walidhani kuwa Mastara ni bondia dhaifu na pambano hilo litamalizika mapema zaidi, lakini Mastara ambaye ni askari aliwashangaza mashabiki na kumaliza pambano hilolililoandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sport chini ya mkurugenzi mtendaji, Kelvin Twissa.

 Zarika aliwapongeza Watanzania kwa kuhimarisha ushirikiano wa jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kumshangilia akiwa ulingoni muda wote nay eye hakuweza kuwaangusha.

Mastara ambaye alivimba kwenye paji la uso kutokana na ngumi, alipinga matokeo hayo na kusema kuwa Zarika hakustahili kushinda.