Zabamba usajili Ulaya

Muktasari:
- Kocha, Unai Emery huko Arsenal kuna dili kadhaa alikuwa akitaka kuzikamilisha ndani ya dirisha hili, huku mastaa ambao ametajwa kuwawinda kwa mkopo ni Ivan Perisic wa Inter Milan na Denis Suarez wa Barcelona.
LONDON, ENGLAND.KILA kocha anahaha. Leo, Alhamisi ikifika saa 5 usiku tu, ndio mwisho wa kufanya usajili kwenye dirisha hili la Januari huko England.
Makocha wa timu mbalimbali kwenye ligi hiyo tangu jana Jumatano walikuwa bize na leo siku ya mwisho watakuwa bize zaidi kukamilisha dili zao za usajili walipozukuwa wakizifanyia kazi kwa mwezi mzima.
Kocha, Unai Emery huko Arsenal kuna dili kadhaa alikuwa akitaka kuzikamilisha ndani ya dirisha hili, huku mastaa ambao ametajwa kuwawinda kwa mkopo ni Ivan Perisic wa Inter Milan na Denis Suarez wa Barcelona.
hao kama hadi kufika asubuhi ya leo hakuna aliyenaswa, basi mchakato utakuwa mkali kufikia kesho asubuhi ya Ijumaa, kila kitu kitakuwa kimefahamika bayana.
Kocha wa muda huko Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer alihusishwa na mpango wa kuongeza beki wa kati kwenye kikosi chake ndani ya dirisha hili, huku beki wa Napoli, Kalidou Koulibaly akidaiwa anaweza kutua Old Trafford kabla ya dirisha halijafungwa usiku.
Kuna dili nyingi zinazotajwa huenda zikatokea, Maurizio Sarri huko Chelsea anaweza akawashangaza wengi akamnasa Memphis Depay, lakini jambo hilo haliwezi kutokea kama Man United hawajasema ndio. Depay kwa sasa yupo Lyon, lakini timu hiyo ya Ufaransa haiwezi kumpeleka Mdachi huyo kwenye timu yoyote ile bila ya kuwahusisha Man United kwanza.
Chelsea inamsaka pia beki Nathan Ake, huku dirisha hili linaweza likafungwa kwa kumpoteza Mbrazili, Willian, ambaye jina lake limekuwa likitajwa na wababe wa huko Nou Camp, Barcelona.
Ishu ya Perisic na Arsenal inaweza kumhusisha Mesut Ozil akaenda Inter Milan kama tu The Gunners watakubali sharti la kulipa mshahara nusu wa Mjerumani huyo na nusu nyingine ataenda kulipwa na wababe hao wa Serie A.
Lakini Ozil amekuwa akitajwa pia na Juventus, jambo linafanya kuwapo na wasiwasi huenda akawa mmoja kati ya wachezaji wa maana watakaohama timu zao kabla ya dirisha hili kufungwa.
Nabil Fekir alihusishwa kwa mara nyingine tena na Liverpool huku kiungo Idrissa Gueye aliingia kwenye rada za Manchester City, kwamba huenda Pep Guardiola akavamia Everton fasta kabla ya dirisha kufungwa kwenda kuchukua huduma ya Msenegali huyo.
Mohamed Elneny wa Arsenal huenda akatimkia Watford huku Leicester City ikitajwa kuwa na mipango ya kumchukua Yourie Tielemans.
Hizo ni baadhi tu ya dili chache kati ya nyingi zinazoweza kukamilishwa na klabu za Ligi Kuu England kabla ya dirisha la Januari kufungwa.