Yanga yaliamsha dude Dom, Nabi asema ni mechi ya kiama

Sunday May 15 2022
Nabi PIC
By Waandishi Wetu

NI mechi ya kiama. Kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi ameweka wazi kwamba kwa namna yoyote ile lazima wahakikishe wanashinda leo dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Akizungumza na Mwanaspoti kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam wakati timu hiyo ikiondoka kwenda Dodoma alikiri mchezo huo utakuwa mgumu na wa ushindani kutokana na kila timu kuhitaji matokeo mazuri lakini wao ni muhimu mno kwani wanataka Kombe msimu huu na wako kwenye hatua nzuri.

Alisema amewaandaa vyema wachezaji wake kuelekea mchezo huo na amezungumza na mmoja mmoja na hata kambini wamesisitiza kurejea kwenye ubora wao uliozoeleka na mashabiki.

“Nimefanya kazi kubwa ya kuzungumza na wachezaji wangu wasahau matokeo yaliyopita na kuangalia yajayo, kwani pointi tulizopoteza zishapotea tunaangalia zijazo,” alisema Nabi ambaye tayari ameshaanza kusuka kikosi cha Caf. Alisema, anajua ugumu na upinzani mkubwa wa ligi uliopo katika kila timu ambayo wanakutana nayo hivyo watatumia akili za ziada kiufundi.

Kuhusu uwanja, Nabi alisema ni moja ya changamoto kubwa kuelekea mchezo huo lakini atajitahidi kuwatumia wachezaji ambao wana uwezo wa kumpa matokeo mazuri kutokana na aina hiyo ya uwanja na hawana hofu yoyote.

“Niwaombe mashabiki wetu waje kwa wingi kuisapoti timu yao kwani ina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri,” alisema.

Advertisement

Naye Injia Hersi Said aliyeambatana na kikosi hicho alisema, mchezo huo ndio utakaorejesha zaidi morali ya nyota wao kuelekea michezo ijayo na kutoa picha ya ubingwa wao msimu huu.

“Tulipoteza pointi michezo iliyopita, sisi kama viongozi tumezungumza na wachezaji wetu na kila kitu kipo sawa kuanzia bonasi hadi morali yao,” alisema Hersi ambaye pia anahusika na usajili wa Yanga.

Yanga inaongoza Ligi ikiwa na pointi 57 huku Dodoma Jiji wao wakiwa nafasi ya nane na pointi 28 ambapo nao mechi iliyopita dhidi ya Polisi Tanzania walitoka suluhu ugenini mjini Moshi.

Advertisement