Yanga yaipigabao Simba kibabe

Muktasari:
- Mabao matatu ya Simba yametokana na kushinda mechi dhidi ya Prisons bao 1-0, Mbeya City 2-0 yote yakiwekwa nyavuni na Meddie Kagere, huku wakitoka suluhu na Ndanda na kufikisha pointi saba, japo haijaruhusu bao lolote nyavuni.
YANGA inaonekana ina hesabu kali dhidi ya watani wao Simba, kwani katika mechi mbili wamewazidi kete kwa kuvuna mabao manne, tofauti na Wekundu hao ambao michezo mitatu wamepata mabao matatu licha ya kuaminika kuwa na safu matata ya ushambuliaji yenye wachezaji saba.
Mabao matatu ya Simba yametokana na kushinda mechi dhidi ya Prisons bao 1-0, Mbeya City 2-0 yote yakiwekwa nyavuni na Meddie Kagere, huku wakitoka suluhu na Ndanda na kufikisha pointi saba, japo haijaruhusu bao lolote nyavuni.
Yanga iliyocheza mechi mbili imepata mabao matano na pointi sita kwa kushinda 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar mabaoyakifungwa na Heritier Makambo na Kelvin Yondani kisha juzi kuilaza Stand United 4-3, yakifungwa na Ibrahim Ajibu, Deus Kaseke, Mrisho Ngassa na Andrew Vincent ‘Dante’, huku ikiruhusu bao nne.
Utamu unakuja hapa, Simba ilifanya usajili wa kufuru na safu kali ya ushambuliaji ikiwa na Meddie Kagere (Gor Mahia, Kenya), Adam Salamba (Lipuli ya Iringa), Rashid Mohamed (Prisons), Marcel Kaheza na kumpandisha Rashid Juma ambao wameungana na John Bocco na Emmanuel Okwi kwa usajili huo ilitoa taswira ya kuvuna mabao mengi, tofauti na kinachoendelea sasa.
Yanga, iliyo kwenye kipindi cha mpito cha ukata wakati wa usajili safu ya ushambuliaji waliwarejesha nyota wao wa zamani Ngassa, Kaseke na kuongeza mchezaji wa kigeni Makambo ambao waliungana na Ibrahim Ajib, Yusuph Mhilu, Said Mussa, Matheo Anthony, Amissi Tambwe na Juma Mahadhi.
Nyota wa zamani klabu hizo, wamezichambua timu hizo ambapo Mtwa Kihwelu alisema Wanajangwani wana timu nzuri zaidi, tatizo ni ukata na kwamba wakipata morali wana nafasi ya kufanya vizuri.
“Yanga na Simba zina ushindani wa hali ya juu, kiufundi Yanga wachezaji wao wana roho ya uzalendo licha ya hali ngumu wamekuwa wakipambana kupata matokeo, wakikaa vizuri kiuchumi wataonyesha zaidi ya hapo,” alisema Kihwelo.
Naye Mrage Kabange aliyewahi kutamba na Simba kabla ya kuzifundisha Kagera Sugar na Njombe Mji, alisema mastaa wa Simba wanapaswa kufanya vitu vinavyoendana na thamani wanayopewa kwa madai wanafanyiwa vitu vikubwa na viongozi wao, lakini wanarejesha vichache jambo alilodai wasipokuwa makini watapigwa bao na Yanga halafu litakuwa jambo la aibu.
“Wachezaji wa Simba wasipojiongeza ni aibu kwao, wenzao Yanga wanajiwekea idadi kubwa ya mabao na hilo ndilo lilitokea msimu wa 2016/17 Yanga walichukua ubingwa kwa uwingi wa mabao, unapompa mpinzani wako nafasi unakuwa unapoteza vitu vikubwa,” alisema.
Said Maulid ‘SMG’ alisema; “Simba ina kikosi kipana na timu nzuri, tofauti na Yanga ina wachezaji wazuri baadhi lakini haina kikosi kipana, ninachokiona hapa kuna wale wanaojiona wanauwezo wanajisahau na wale ambao wana kiu ya kuonyesha kitu,”.
Mkongwe Zamoyoni Mogalla alisema kunahitajika ushirikiano wa hali na mali kati ya kocha mkuu wa timu hiyo Patrick Aussem na Msaidizi wake Djuma Masoud ambaye anawafahamu wachezaji na alifanikisha ubingwa wa timu hiyo akiwa na Piere Lachantre.
“Simba sio ya kuokota bao moja moja, ina wachezaji wapambanaji nafikiri kocha mkuu akae chini na msaidizi wake wawe wanashauriana, ndipo itakaporejesha makali yake na itaanza kufunga sana, lasivyo Yanga wataendelea kutumia nafasi.”