Yanga, Simba, TRA United zimekula kibano cha TPLB
Muktasari:
- Katika taarifa iliyotolewa Juni 10, 2026, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ilitangaza adhabu hizo ambazo zimezikumba Simba, Yanga, Mtibwa Sugar, TRA United na Coastal Union pamoja na klabu za Championship za Mbuni FC na African Sports.
BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeendelea kuonyesha makali yake katika kusimamia nidhamu baada ya kutoa adhabu mbalimbali kwa wachezaji, maofisa na mashabiki pamoja na klabu za Ligi Kuu Bara na Championship kufuatia ukiukwaji wa kanuni katika mechi tofauti zilizochezwa hivi karibuni.
Katika taarifa iliyotolewa Juni 10, 2026, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ilitangaza adhabu hizo ambazo zimezikumba Simba, Yanga, Mtibwa Sugar, TRA United na Coastal Union pamoja na klabu za Championship za Mbuni FC na African Sports.
Kiungo wa Mtibwa Sugar, Fredrick Magata atakosa mechi zao zilizobaki msimu huu baada ya kufungiwa mechi tano na kutozwa faini ya Sh500,000 kwa kosa la kuwashauri maofisa wa Mtibwa Sugar kufanya mabadiliko ya mchezaji ambaye hakuwa sehemu ya kikosi kilichoruhusiwa kucheza mechi husika.
Mbali na hilo, TRA United imepigwa faini ya Sh5 milioni kutokana na kocha mkuu wa timu hiyo kutohudhuria mkutano wa waandishi wa habari kabla ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar. Klabu hiyo pia ilitozwa faini nyingine ya Sh11 milioni baada ya kocha msaidizi kutofika kwenye mkutano wa kabla ya mchezo dhidi ya Fountain Gate.
Simba yapigwa faini, shabiki afungiwa mwaka mmoja
Simba SC nayo haikusalimika baada ya kutozwa faini ya Sh5 milioni kufuatia tukio la mtoto muokota mipira kumwaga maji kwenye chupa zilizokuwa karibu na eneo la benchi la Dodoma Jiji.
Tukio hilo lilizua taharuki baada ya baadhi ya mashabiki kuanza kurusha chupa kuelekea eneo la wapinzani.
Wakati huohuo, shabiki wa Simba anayejulikana kama Omary Omary maarufu Bomba amefungiwa kuingia viwanjani kwa miezi 12 kutokana na kufanya vitendo vya fujo na kutumia lugha zisizofaa dhidi ya viongozi wa Dodoma Jiji.
Mashabiki wa Yanga wafungiwa miezi mitatu
Kwa upande wa Yanga, mashabiki wawili maarufu, Baraka Selemani (Baraka Yanga) na Abdulrahman Said (Fumau Mshairi), wamefungiwa kuingia viwanjani kwa muda wa miezi mitatu.
Mashabiki hao walibainika kutumia tiketi za watu wengine kuingia katika jukwaa la VIP A wakati wa mchezo dhidi ya Namungo FC, kitendo kilichotajwa kukiuka taratibu za viwanja.
Coastal Union yapoteza mshambuliaji
Mshambuliaji wa Coastal Union, Meshack Abraham, amefungiwa mechi tatu baada ya kucheza dhidi ya Simba SC akiwa na idadi ya kadi za njano zilizomzuia kushiriki mchezo huo.
Mbuni FC na Yunus Lema waadhibiwa
Katika Ligi ya Championship, Mbuni FC ya Arusha imetozwa faini ya Sh1 milioni kwa kushindwa kutekeleza taratibu za mtiririko wa matukio ya siku ya mechi wakati wa mchezo dhidi ya TMA.
Aidha, mchezaji wa Mbuni, Yunus Lema, ametozwa faini ya Sh500,000 kwa kukwepa kupokea mikono ya timu pinzani kabla ya mchezo kuanza, kitendo kilichoelezwa kuwa ni kinyume cha kanuni za nidhamu kwa wachezaji.
African Sports yaonywa vikali
Kwa upande wa African Sports ya Tanga, klabu hiyo imepewa onyo kali baada ya kuwakilishwa na waombaji wanne badala ya wawili kwenye kikao cha maandalizi ya mechi dhidi ya Polisi Tanzania.
Kamati ilisema kitendo hicho ni ukiukwaji wa taratibu za mashindano na kuwataka viongozi wa klabu hiyo kuzingatia kanuni katika mechi zijazo.
Kwa ujumla, adhabu hizo zinaonyesha dhamira ya TPLB ya kuimarisha nidhamu ndani na nje ya uwanja huku ikitoa ujumbe kwamba hakuna klabu, kiongozi, mchezaji au shabiki atakayekuwa juu ya sheria za soka la Tanzania.