Yanga kiroho safi

Muktasari:
YANGA imejificha mkoani Mtwara ikipiga hesabu za kuwafuata wapinzani wao Namungo ya Lindi lakini huku nyuma kocha wao Nesreddine Nabi amewasilisha ombi la kuletewa wataalam wawili zaidi.
YANGA imejificha mkoani Mtwara ikipiga hesabu za kuwafuata wapinzani wao Namungo ya Lindi lakini huku nyuma kocha wao Nesreddine Nabi amewasilisha ombi la kuletewa wataalam wawili zaidi.
Iko hivi. Mpaka sasa Nabi ametua na wataalam wawili akiwa na kocha msaidizi wa kwanza Sghir Hammad na kocha wa mazoezi ya viungo Jawad Sabri sasa kuna wengine wawili wanashushwa.
Ni kwamba kabla ya msimu ujao kuanza kuna uwezekano kwenye ufundi tu kukawa na watu sita ukiondoa wataalam wa tiba.
Akizungumza na Mwanaspoti Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, Dominic Albinius alisema mtaalam wa kwanza ambaye amesalia katika ujio wa Nabi ni mtu wa kuchambua ubora wa wapinzani.
Albinius alisema mtaalam huyo ambaye atatua nchini wakati wowote ndio raia wa kigeni aliyesalia katika benchi la Nabi. “Atakuja wakati wowote zipo taratibu anazimalizia kuzikamilisha huko aliko ili aje hapa nchini kufanya kazi,” alisema Albinius
Ingawa Albinius hakutaka kufafanua zaidi lakini Mwanaspoti linafahamu kwamba jamaa huyo ambaye jina lake halijawekwa wazi tayari anaifanya kazi hiyo mpaka sasa akitumiwa mikanda ya timu pinzani na kazi yake bora ya kwanza ilikuwa alipowachambua Prisons. Katika mchezo huo Yanga ilishinda bao 1-0 na kutinga hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Azam Shirikisho. Mtaalam huyo anaijua kazi hiyo vizuri na lengo ni kumrahisishia kazi Nabi.
Albinius aliongeza kuwa; “Kocha pia anataka atafutiwe mtu wa saikolojia kwa muda aliokaa na timu ameona kuna haja ya kuwa na mtu wa kazi hiyo. Amesema huyu mtu wa saikoloji anatamani awe raia wa Tanzania ili kuweza kuelewana na wachezaji wengi lakini atakuwa na faida ya kujua mazingira ya hapa kuliko akija mgeni.
“Tumekubaliana na ushauri wake,” alisisitiza.