Yanga haikamatiki

Mashabiki wa Yanga wakishangilia kwenye Mechi yao na Mbeya City iliyochezeka jana kwenye Uwanja wa Taifa.
Muktasari:
Yanga imeendeleza jeuri hiyo ikiwa ni siku chache baada ya kuinyuka Coastal Union mabao 8-0 huku ikiwa na kumbukumbu nzuri kimataifa baada ya kuipiga chini Platinum ya Zimbabwe na sasa inapiga kifua ikimaanisha Etoile du Sahel waje hata sasa hivi.
AFRIKA Mashariki jana kulikuwa na mechi mbili kubwa kwenye Ligi za ndani, Kenya kulikuwa na mpambano wa Mashemeji baina ya Gor Mahia na AFC Leopards ambao uliisha kwa sare ya bao 1-1. Lakini kimbembe kilikuwa Bongo, Yanga ilizidisha kiburi na jeuri kwa kuthibitisha kwamba msimu huu haikamatiki kotekote baada ya kuifumua Mbeya City mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga imeendeleza jeuri hiyo ikiwa ni siku chache baada ya kuinyuka Coastal Union mabao 8-0 huku ikiwa na kumbukumbu nzuri kimataifa baada ya kuipiga chini Platinum ya Zimbabwe na sasa inapiga kifua ikimaanisha Etoile du Sahel waje hata sasa hivi.
Vinara hao wa Ligi Kuu wamebakiza pointi tano tu kukata tiketi ya kucheza michuano ya CAF mwakani na pointi 11 kuwavua Azam ubingwa baada ya ushindi wao wa jana.
Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 46, nane zaidi ya ilizonazo Azam yenye pointi 38 baada ya juzi kung’ang’aniwa tena na sare dhidi ya Mtibwa Sugar ikiwa ni mara ya pili mfululizo.
Pointi hizo zinaifanya Yanga kubakisha pointi tano ili kupata moja ya nafasi mbili za uwakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa na kuwafungia njia Simba wenye pointi 35 na inayoweza kufikisha pointi 50 tu ikishinda mechi zake zote.
Pia Yanga imebakiza pointi 11 tu kuweza kuwavua Azam ubingwa kwani itafikisha pointi 57 ambazo haziwezi kufikiwa na watetezi hao hata wakishinda mechi zao zote kwani itaweza kufikisha pointi 56 tu.
Katika pambano hilo lililochezeshwa vema na mwamuzi Mathew Akram, Yanga ilianza kwa kasi dakika tano za kwanza kwa kulishambulia lango la wapinzani wao na dakika ya sita Amissi Tambwe aliandika bao, lakini lilikataliwa kwani kabla ya kufunga mwamuzi wa pembeni alinyoosha kibendera.
Hata hivyo walisahihisha makosa katika dakika ya 18 baada ya Kpah Sherman kufunga bao la kwanza akimalizia shuti lililotemwa la Haruna Niyonzima. Hilo likiwa bao la pili kwa Mliberia huyo msimu huu.
Vijana wa Hans vand der Pluijm waliendelea kuliandama lango la wapinzani wao na kufanikiwa kuandika bao la pili katika dakika ya 37 kupitia kwa Salum Telela aliyefunga kwa shuti kali baada ya kuanzishwa mpira wa adhabu na Niyonzima.
Mbeya City waliotoka kuwabana Azam kwa kutoka nao sare ya 1-1 Jumatano iliyopita ilicharuka na kupata bao lao dakika tano kabla ya mapumziko kupitia kwa Themi Felix ‘Mnyama’ baada ya kuwafunga tela mabeki wa Yanga kabla ya kupiga ‘chop’ iliyoshindwa kudakwa na kipa Ali Mustafa.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Mbeya City kukosa mabao ya wazi kabla ya kuruhusu bao katika dakika ya 49 baada ya nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ya Niyonzima. Mbeya ilipata pigo dakika nne baadaye baada ya Themi kulimwa kadi nyekundu na mwamuzi Mathew Akrama baada ya kumchezea madhambi Salum Telela. Telela alijikuta akishindwa kuendelea na mchezo huo na kutolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Dilunga. Licha ya kucheza pungufu, Mbeya City waliibana Yanga na hasa baada ya kufanya mabadiliko ya wachezaji kwa kuwatoa Deus Kaseke, Raphael Alpha na Paul Nonga na kuwaingiza Peter Michael, Mwegane Yeya na Abdallah Seif.
YANGA: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyi Twite, Salum Telela/Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Kpah Sherman/Mrisho Ngassa na Simon Msuva.
MBEYA CITY;Hannington Kalyesabula, Richard Peter, Hassan Mwasapili, Juma Nyosso, Christian Sembuli, Kenny Ally, Paul Nonga/Mwegane Yeya, Raphael Alpha/Abdallah Seif, Themi Felix, Peter Mwalyanzi na Deus Kaseke/Peter Mapunda.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Stand United ikiwa nyumbani ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Moro na kuzidi kujiweka katika nafasi nzuri ya kusalia msimu ujao.
Mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga ambao leo Jumatatu utashuhudiwa nyasi zake zikiwaka moto wakati Kagera Sugar na Ruvu Shooting zitakapoumana baada ya mvua kuzuia pambano lao juzi Jumamosi.
Nako nchini Kenya wapinzani wa jadi Gor Mahia na AFC Leopards zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Leopards waliokuwa nyumbani walishtukizwa na Gor baada ya kupata bao la kuongoza kupitia Ali Abondo bao lililodumu hadi mapumziko kabla ya Leopards kuchomoa dakika ya 50 kwa bao la Jacob Keli baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Gor.
Sare hiyo imeifanya Gor kuzidi kung’ang’ania kileleni mwa Ligi Kuu Kenya ikiwa na pointi 13 baada ya mechi tano. Katika mchezo mwingine ligi hiyo Sofapaka ilipata ushindi wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Nakuru Allstars. Mabao ya Collins Shivachi na John Baraza aliyefunga mawili, huku la Nakuru likifungwa na Frank Balala.
Nao wapinzani wa Yanga katika Kombe la Shirikisho Etoile du Sahel walipata ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Bades kwenye Ligi Kuu Tunisia.
Mabao ya Etoile yalifungwa na Mouihbi dakika ya 13 na Bedoui dakika ya 45 na kuifanya Etoile kuzidi kujichimbia kileleni ikiwa na pointi 49 baada ya mechi 24.