Wajue wapinzani wa Simba CAF

SIMBA jana walikuwa na jambo lao kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini wakati wa tamasha lao la Simba Day, lakini wanapaswa kujua katika michuano ya kimataifa wataanza msimu katika raundi ya kwanza dhidi ya Wabotswana.

Ndio, Jwaneng Galaxy imefuzu raundi ya kwanza baada ya kuing’oa DFC Bene Arrondissement a Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda nyumbani Gaborone kwa mabao 2-0 na kulala ugenini 1-0.

Wababe hao wa Botswana ndio watakaokuwa wenyeji wa Simba katika mechi yao ya mkondo wa kwanza inayotarajiwa kupigwa mwezi ujao kati ya Oktona 15-16 na kurudiana tena wiki moja baadaye kati ya Oktoba 22-23 jijini Dar es Salaam ili kuamua ya kwenda makundi na nyingine ya kwenda play-off

Kufanya vizuri kwa Simba msimu uliopita ambapo waliishia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika ngazi ya klabu ndio sababu ambayo iliwafanya mabingwa hao wa nchi kuanzia raundi ya pili sambamba na vigogo wengine, ikiwemo Al Ahly na Mamelodi Sundowns.

Jwaneng Galaxy inayodhaminiwa na wamiliki wa mgodi wa Dhahabu huko Botswana, imetinga hatua hiyo baada ya kuzichanga vyema karata zao kwenye mechi za raundi ya awali, kwani ushindi wa nyumbani uliwabeba licha ya kupoteza ugenini 1-0.

Ipi siri ya mafanikio ya Jwaneng Galaxy licha ya kuwa ni timu dogo ambayo ilianzishwa miaka sita iliyopita? Nguvu yao ipo wapi na je, Simba wanawezaje kuvuka kikwazo kilichopo mbele yao na kutinga tena hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa pili mfululizo, huu ni uchambuzi ambao una majibu ya maswali yote hayo.


HISTORIA YAO

Galaxy iliundwa mwaka 2015 baada ya klabu mbili kuamua kuunganisha nguvu ambazo ni Jwaneng Comets na Debswana Youngsters, hilo liliwasaidia kuwa na nguvu kubwa kwenye soka la ushindani nchini humo tofauti na miaka ya nyuma na timu hizo zilikuwa za kawaida.

Ndani ya mwaka huo, Galaxy ilionyesha ubabe wao kwenye Ligi Daraja la Kwanza Botswana na kupanda Ligi Kuu, taratibu ilikuwa ikikijenga kikosi chao hadi kuwa na timu ya ushindani mbele ya wababe wa soka la Botswana ambao ni BDF IX ambayo aliwahi kuichezea Mtanzania, Rashid Mandawa, Township Rollers na Gaborone United Sporting Club.

Ilianza kwa kuambulia nafasi ya pili kwenye ligi ya Botswana kwa miaka mitatu mfululizo ambayo ni 2017, 2018, 2019 kabla ya msimu uliopita, 2019/20 kutwaa ubingwa wa ligi hiyo ambayo kwa sasa ni maarufu kama BTC Premiership.

Mbali na kutwaa kwao mara moja ubingwa wa BTC Premiership, wanamataji mengine mawili ya Mascom Top 8 waliyotwaa 2016-17 na 2018-19.


UBABE WAO BOTSWANA

Jwaneng Galaxy ina jeuri ya fedha ikijivunia uwepo wa udhamini wa wamiliki wa mgodi wa dhahabu nchini humo kama ambavyo GSM wamekuwa wakiifanyia makubwa Yanga, ndivyo mabosi hao wamekuwa wakiipigania klabu hiyo kuleta mapinduzi ya soka.

Inaelezwa lengo la kwanza lilikuwa ni kufanya vizuri kwenye soka lao la ndani na baada ya kutimiza hilo wanataka kuwa miongoni mwa timu tishio Afrika hivyo Simba wasitegemee wepesi kwenye mchezo huo wa raundi ya pili kutokana na kujidhatiti kwa klabu hiyo.

Licha ya kwamba wapo wanaosema kufanya vizuri kwa klabu hiyo kumechangiwa na anguko la kiuchumi kwa baadhi ya klabu nchini humo kutokana na janga la virusi vya corona, Simba wanapaswa kuwapa uzito wapinzani hao maana wakiwabeza inaweza kuwatokea puani.


REKODI ZAO AFRIKA

Mwaka 2018, Jwaneng Galaxy walipata nafasi ya kushiriki kwa mara ya kwanza kombe la Shirikisho Afrika, waliishia katika hatua ya awali kwani walikumbana na kipigo cha bao 1-0 kwenye michezo yote miwili nyumbani na ugenini dhidi ya Costa do Sol ya Msumbiji.

Ushindi wao wa kwanza kwenye michuano ya kimataifa wameupata msimu huu ambapo ni dhidi ya DFC Beme Arrondissement tena wakati wakiwa nyumbani kwa mabao 2-0.Kiujumla kwenye michezo minne waliyocheza kimataifa wamepoteza mitatu na kushinda mmoja.


NYOTA WA KUCHUNGWA

Miongoni mwa wachezaji hatari kwenye kikosi cha Jwaneng Galaxy ni pamoja na Muafrika Kusini, Lucky Mokoena ambaye kwenye mchezo wa raundi ya kwanza alitupia miongoni mwa mabao ambayo yameibeba timu hiyo na kutinga raundi ya pili.

Mokoena ni mzoefu na miongoni mwa klabu ambazo aliwahi kuzichezea wakati akiwa kwao Afrika Kusini ilikuwa ni pamoja na Highlands Park.


MSIKIE MTANZANIA

Huko Botswana ambako wanatoka wapinzani wa Simba yupo Mtanzania, Abdallah Hamisi ambaye anaichezea Orapa United amewaelezea Galaxy kwa kusema ni timu nzuri ambayo inaweza kuipa changamoto Simba kwenye raundi hiyo ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Ni muda kidogo umepita tangu niwaone Galaxy maana huku Botswana ligi imesimama kwa muda mrefu kidogo kutokana na janga la virusi vya corona, nasikia wamesajili wachezaji wengine wapya lakini kwa ninavyowafahamu timu yao ni nzuri na kati ya wachezaji wao hatari ni pamoja na Mokoena,” alisema kiungo huyo.

Abdallah aliongeza kwa kusema,” Siwezi kuwaweka Galaxy kwenye daraja moja na Simba maana hii ni timu changa pamoja na kwamba wanao wachezaji wenye uzoefu.”