TSC yaivuruga Fountain Gate, Alliance Girls mambo safi

Saturday May 14 2022
tsc pic
By Damian Masyenene

Mwanza. Mbali na kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wananwake iliokuwa ikiutolea macho, timu ya Fountain Gate Princess imejikuta ikiweka rehani nafasi ya pili baada ya kusimamishwa leo jijini Mwanza.

Timu hiyo yenye maskani yake jijini Dodoma kabla ya mechi ya leo ilikuwa kwenye nafasi ya pili ikisikilizia endapo Simba Queens ingepoteza leo dhidi ya Mlandizi Queens ili izidishe matumaini yake ya kuwania ubingwa lakini hilo limekwama baada ya Simba kushinda na kutetea taji.

Fountain Gate Princess iliyokuwa ugenini katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza imejikuta ikilazimishwa suluhu (0-0) na vibonde TSC Queens na kujikuta ikishuka hadi nafasi ya tatu baada ya Yanga Princess kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Mlandizi Queens na kufikisha pointi 50 huku FGP ikifikisha 48.

Mchezo huo umepigwa saa 8 mchana uwanjani hapo huku Fountain Gate Princess ikipoteza nafasi nyingi za wazi za kupachika mabao ambao nyota wake S'arrive Bandiambila, Winfrida Gerald na Niyonkuru Sandrine walijikuta wakishindwa kufua dafu.

Licha ya sare hiyo TSC Queens ambayo imefikisha pointi saba bado inaendelea kuburuza mkia ikikamata nafasi ya 12 huku ikikamilisha tu ratiba kwani tayari imeshashuka daraja.

Katika mchezo mwingine uliopigwa leo kwenye uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza saa 10 jioni, Alliance Girls imefufuka na kurejea kwenye ushindi ikiichapa Baobab Queens ya Dodoma mabao 2-1.

Advertisement

Baobab Queens ambayo mchezo uliopita iliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya TSC Queens uwanjani hapo, ndiyo ilikuwa ya kwanza kuandika bao katika dakika ya 15 kupitia kwa Jamila Rajabu ambaye amefunga bao lake la 15 msimu huu.

Alliance Girls ambayo haijapata ushindi katika michezo mitatu mfululizo ilitulia na kuliandama lango la Baobab Queens ambapo walisawazisha mnamo dakika ya 29 kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Winfrida Charles huku bao la ushindi likifungwa na Masika Hamis dakika ya 54 kwa faulo ya moja kwa moja nje ya 18.

Advertisement