Tinoco: Bebi kanipenda na kimkulima changu hiki!
Mlinda mlango wa Yanga, Benedict Tinoco
Muktasari:
Huyu jamaa ni yule kipa mrefu aliyesajiliwa msimu huu akitokea Kagera Sugar ya Bukoma. Baada ya kuhamia Dar, Tinoco amepanga chumba kimoja katika nyumba iliyopo maeneo ya Mbagala, Kipati. Hapo anaishi peke yake.
KAMA ilivyo kawaida ya ukurasa huu ni kukuletea simulizi za maisha ya wanasoka nje ya uwanja. Leo utafahamu zaidi mlinda mlango wa Yanga, Benedict Tinoco, anavyoishi.
Huyu jamaa ni yule kipa mrefu aliyesajiliwa msimu huu akitokea Kagera Sugar ya Bukoma. Baada ya kuhamia Dar, Tinoco amepanga chumba kimoja katika nyumba iliyopo maeneo ya Mbagala, Kipati. Hapo anaishi peke yake.
Mwanaspoti lilipofika nyumbani kwake katika mishemishe za ‘Mpaka Home’, lilimkuta akiwa na jamaa zake waliofika kumtembelea, mmoja wao alikuwa kaka yake wa damu Daud. Muda huo walikuwa wakiandaa msosi na mpishi alikuwa Tinoco mwenyewe.
Kwa Dar, Tinoco ndiyo kwanza anaanza maisha, kwani tangu ahamie jijini humo baada ya kusajiliwa na Yanga, haijapita hata miezi miwili. Hivyo mshikaji anaishi kisela.
Hata hivyo, safari ya kwenda kwake ilikuwa na changamoto kadhaa ikiwamo gari alilokuwa anaendesha Mwandishi wa Makala haya kupata ajali, lakini akatoka salama.
Nyumbani
Mwanaspoti: Hodi
Tinoco: Karibu Dada mwandishi. Hapa ndipo nyumbani, nimeamua kuja kujificha huku si unajua tena maisha.
Mwanaspoti: Kwa nini uliamua kuja kukaa huku na hii ni nyumba ya ngapi tangu ulipoanza maisha ya Dar es Salaam?
Tinoco: Niliamua kuja kukaa huku kwa sababu mazingira ni mazuri na kumetulia, hakuna usumbufu ikifika saa nne tu kila mtu nyumbani kwake, pia nimepazoea kwani ninao jamaa zangu wanaoishi huku ambao nilishakuwa na mazoea ya kuja kuwatembelea tangu zamani. Hii ni nyumba ya pili mimi kuishi hapa Dar, awali nilikuwa naishi Mabibo na nilihama huko kama wiki mbili zilizopita.
Mwanaspoti: Unapokuwa nyumbani, unapendelea kufanya shughuli gani na unapomaliza huwa unajiburudisha na nini?
Tinoco: Nafanya shughuli zote kama kupika, kufua, kusafisha nyumba, kuteka maji na mambo mengine, hakuna anayenifanyia kazi za hapa nyumbani kama unavyoona sina mke wala mtumishi wa ndani.
Ninapokuwa sina shughuli, huwa nasikiliza muziki tu, napenda zaidi taarabu na msanii ninayemkubali ni Isha Mashauzi. Unaiona redio yangu? (Huku akiinyanyua) hii ni mkulima. Huwa naweka ‘Memory Card’ nasikiliza, maisha yanaendelea, siwezi kuigiza maisha, naishi maisha yangu halisi.
Mwanaspoti: Kitu gani ndani ya nyumba yako unachokipenda zaidi?
Tinocco: Aisee, ni mkulima yangu. Naipenda sana kwa sababu ndiyo huniliwaza wakati wote na kuniondolea uchovu. Kiredio hiki kinamvutia hata ‘Baby’ wangu (akimaanisha mpenzi wake), amenipenda na hii hii mkulima yangu.
Mwanaspoti: Mbali na mpira, shughuli gani nyingine unafanya?
Tinoco: Ninazo biashara tofauti ikiwamo ‘steshenari’, pia ninalima. Hayo yote yanafanyika nyumbani Mara, wapo watu nimewaajiri kwenye shughuli hizo.
Uhusiano
Mwanaspoti: Umesema hauna mke, vipi mpango wako, unaye mchumba?
Tinoco: (Anacheka) Sawa ni mambo ya kawaida. Ninaye mchumba anaitwa Mariam Samwel, ni mwanafunzi anayesomea udaktari. Ninajua nitakapoumia uwanjani, atanitibu bure. Ninampenda sana na mipango yetu ni kuja kuishi pamoja tukiwa mume na mke na tutengeneze familia bora.
Mwanaspoti: Upo naye kwa muda gani na mlikutana wapi?
Tinoco: Tuna miaka mitatu sasa. Tulikutana Musoma, wakati huo nilikuwa naichezea Polisi Mara na yeye alikuwa anacheza Netiboli. Uwanja wa Posta Mara waliokuwa wanautumia, ulikuwa karibu na tuliokuwa tukiutumia sisi hivyo ikawa rahisi kukutana.
Hata hivyo, hata nyumba tulizokuwa tunaishi zilikuwa karibu na nilisoma naye darasa moja pale Shule ya Sekondari ya Mwisenge.
Mwanaspoti: Kitu gani kinachokufanya umpende yeye na si mwingine? Pia mtakapooana utapenda muwe na watoto wangapi?
Tinoco: Ni mzuri, ana umbo zuri, mpole, mkarimu, pia anayejiheshimu. Kwa kifupi anayajua maisha. Tukifanikiwa kutimiza azma yetu ya kuoana, nataka tuzae watoto watatu tu, si unajua maisha yalivyo? Kama wataongezeka au kupungua, hiyo namwachia Mungu.
Tinoco ni nani, historia ya soka
Mwanaspoti: Tufahamishe, Tinocco ni nani?
Tinoco: Ni mtoto wa mwisho kuzaliwa katika familia yenye watoto watano; Rizika, Dickson, Daud, Asteria na Ben. Nimekulia Musoma, Mara. Tinocco ni jina halisi la baba, si la utani.
Kucheza soka ni kipaji changu cha kuzaliwa. Nilianza kucheza tangu nilipokuwa mdogo.