Tanzania Prisons yajipanga upya

Muktasari:
- Baada ya ushindi wa mabao 2-1 ilioupata mechi ya mwisho dhidi ya Coastal Union, wachezaji wa Prisons walipewa mapumziko na wanatarajia kurejea kambini Juni Mosi ili kumalizana na dakika 180 za mechi mbili za kufungia msimu.
KOCHA wa Tanzania Prisons, Amani Josiah amesema mapumziko ya wiki mbili aliyotoa kwa wachezaji anaamini yatawajenga na kupata nguvu mpya ya kufanya vizuri katika mechi mbili zilizosalia ikiwamo ile ya nyumbani dhidi ya Yanga.
Baada ya ushindi wa mabao 2-1 ilioupata mechi ya mwisho dhidi ya Coastal Union, wachezaji wa Prisons walipewa mapumziko na wanatarajia kurejea kambini Juni Mosi ili kumalizana na dakika 180 za mechi mbili za kufungia msimu.
Kocha wa Prisons aliliambia Mwanaspoti kuwa, bado hawapo eneo zuri katika msimamo, hivyo ni lazima wajipange ili kumaliza vyema msimu kwa mechi mbili zilizosalia.
“Wachezaji ni binadamu wanahitaji mapumziko ya kuziweka akili zao sawa pamoja na kukusanya nguvu mpya, ndio maana katika mapumziko ya mwezi mzima nimetoa wiki mbili, ili wakirudi wawe na nguvu mpya ya kuipigania timu,” alisema Josiah na kuongeza.
“Wanatambua tuna mechi mbili ngumu mbele yetu, tunacheza na Yanga nyumbani, tutaifuata Singida Black Stars, timu zote zinapambania nafasi, ndiyo maana niliona kuna haja ya kuwapumzisha ili kujipanga kulingana na mechi halisi ambazo tutacheza.”
Kocha huyo alisema katika mapumziko hayo aliwapa programu maalumu na ratiba za mechi, lengo ni kuhakikisha wasijisahau na kutoka mchezoni kwa kula bata badala ya kujiweka fiti kwa kazi ya mwisho.
“Kwa aina ya mazoezi niliyonayo siwezi kumzuia mchezaji kula bata, kwani hadi tunaachana waliona ushindani wa namba ulivyo kila mmoja anatamani kuingia kikosi cha kwanza,” alisema Josiah aliyepewa timu baada ya Mbwana Makata kuachana na klabu hiyo katikati ya msimu akitokea Geita Gold iliyopo Ligi ya Championship.
Kwa sasa Prisons ipo nafasi ya 12 ikicheza mechi 28 ikishinda nane, sare sita na kupoteza 14, huku ikifunga mabao 23 ya kufungwa 38 na kukusanya pointi 30 ikiwa kwenye janga la kuangukia katika play-off ya kushuka daraja kuzifuata KenGold na Kagera Sugar zilizotangulia mapema.