Sserunkuma aitetemesha Yanga

Muktasari:
Kwa upande wake, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema: “Ni mchezaji mzuri, lakini tunasubiria ili aweze kuonyesha ufundi wake uwanjani kama mchezaji wa kigeni ili wazawa tujifunze kitu kutoka kwake.”
MABEKI wa Yanga, wamesema endapo watani wao wa jadi, Simba, wakimsainisha Dan Sserunkuma, watakuwa wamepata kifaa na mambo yatakuwa si mchezo kwenye mechi ya Mtani Jembe Desemba 13.
Beki mzoefu kwenye kikosi cha Yanga na Taifa Stars, Oscar Joshua, alikiri kuwa kwa jinsi anavyomfahamu Sserunkuma ni mchezaji anayesumbua sana safu za ulinzi na pia ana kasi ya kutaka kuzifuma nyavu za wapinzani wao mara kwa mara.
“Kwa upande wangu kama beki napenda kukutana na washambuliaji wasumbufu kama Sserunkuma ambaye ataifanya akili yangu ijishughulishe muda wote ili kumdhibiti,” alisema.
Aliongeza: “Atawasumbua wengine, mimi najipanga kukabiliana na aina zote za mikikimikiki ili niweze kutoa msaada kwenye kikosi changu hasa kutwaa ubingwa msimu huu na kufanya vizuri kwenye mechi ya Mtani Jembe.”
Kwa upande wake, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema: “Ni mchezaji mzuri, lakini tunasubiria ili aweze kuonyesha ufundi wake uwanjani kama mchezaji wa kigeni ili wazawa tujifunze kitu kutoka kwake.”
Cannavaro alisema kwa mechi alizowahi kumuona Sserunkuma akicheza, Mganda huyo alionyesha uwezo mkubwa, hivyo anaamini kama akipata kombinesheni nzuri, Simba watakuwa wameongeza kitu cha tofauti.
Sserunkuma anatarajia kusaini Simba leo Jumanne au kesho akitokea Gor Mahia ya Kenya.