Singida BS ilivyoipitisha tanuru la moto Mbeya City
Muktasari:
- Singida Black Stars msimu huu imeonekana kuwa ‘adui’ wa Mbeya City na kuiweka katika presha kubwa ya kushuka daraja baada ya kuvuna ushindi kwenye mechi zote walizokutana nje na ndani.
PAMOJA na kubaki na pointi tatu nyumbani, Singida Black Stars imeweka rekodi na historia kwa Mbeya City kwa kuvuna mabao 13 katika michezo mitatu waliyokutana msimu huu.
Singida Black Stars msimu huu imeonekana kuwa ‘adui’ wa Mbeya City na kuiweka katika presha kubwa ya kushuka daraja baada ya kuvuna ushindi kwenye mechi zote walizokutana nje na ndani.
Mbeya City ambayo imerejea Ligi Kuu msimu huu, haijawa na matokeo mazuri ikiwa nafasi ya 14 kwa pointi 22, ambapo imebakiza michezo mitano ya jasho na damu kujua mustakabali wake Ligi Kuu.
Mechi zilizobaki kwa timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya, ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba na TRA United itakazocheza nyumbani, huku ikisafiri mechi mbili dhidi ya Pamba Jiji na Dodoma Jiji.
Katika mchezo wa kwanza kukutana timu hizo katika uwanja wa Kwaraa mjini Babati, Mbeya City ilichakazwa mabao 4-1 kisha kukutana mchezo wa kombe la shirikisho huko mjini Singida na kulambiswa 5-1 na juzi wakazibwa 4-1.
Matokeo hayo yaliifanya Singida Black Stars kufikisha pointi 41 na kujitanua zaidi nafasi nne za juu, huku ushindi mwingine ukiipeleka robo fainali ya shirikisho licha ya kwamba baadaye waliondoshwa na Coastal Union kwa penalti 4-2 huko Mkwakwani Tanga.
Ofisa Habari wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota amesema licha ya matokeo ya timu hiyo lakini bado hawajakata tamaa na wanaenda kujipanga upya na michezo iliyobaki wakiwa na matumaini ya kufanya vizuri.
“Tuna mechi mbili nyumbani za bandika bandua, tukianza na Mtibwa Sugar kisha Simba, hizi na nyingine tunaenda kuziwekea mkakati kuhakikisha Mbeya City haishuki daraja”
“Kwa kuwa ligi inasimama kwa muda tukirejea jijini Mbeya tutaangalia ratiba na mahitaji ya timu kuhusu wachezaji kwenda likizo fupi, kimsingi mashabiki na wadau ni muda sasa tuendelee kushirikiana,” alisema Mwankota.