Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sinema nzima ya Ihefu, Singida Big Stars

Muktasari:

  • Kwa tafsiri isiyo rasmi muswada huo unalenga kufanya hali ya baadaye ya soka nchini humo kuwa imara kwa kufanya mageuzi katika usimamizi wa mpira wa miguu katika ngazi ya klabu.

MACHI 19, mwaka huu, serikali ya Uingereza iliwasilisha bungeni muswada unaotarajiwa kudhibiti uendeshaji wa klabu za soka kiuchumi, kijamii na kimichezo baada ya mwongozo wa maoni (white paper) unaoitwa “A Sustainable Future- Reforming Club Football Governance” kuchapishwa kwenye tovuti yake tangu Februari.

Kwa tafsiri isiyo rasmi muswada huo unalenga kufanya hali ya baadaye ya soka nchini humo kuwa imara kwa kufanya mageuzi katika usimamizi wa mpira wa miguu katika ngazi ya klabu.
Muswada huo, ambao utaanzisha ofisi ya Mratibu Huru wa Mpira wa Miguu (Independent Football Regulator, IFR) ambayo, haitakuwa ikiingiliwa na serikali wala mamlaka za soka, unalenga kulinda na kuendeleza uimara wa kifedha kwa klabu zinazoshiriki ligi tano za juu, kuimarisha mfumo bora wa mgawanyo wa mapato kama ule unaozingatia ukubwa wa timu na mwisho unalenga kulinda utamaduni wa mpira wa miguu wa Uingereza ambao ni muhimu kwa mashabiki na jamii iliyo katika maeneo ambayo klabu zinatoka.

Nimeupenda muswada huu kwa kuwa una mambo mengi ya kulinda uimara na uhai wa klabu za soka na hasa mashabiki wake, ukizingatia kuwa mpira wetu unapitia katika wakati ambao baadhi ya mambo ambayo Waingereza wanataka kuyadhibiti, huku ndio tunayafanya kwa kasi.

Katika muhtasari wa muswada huo, serikali ya Uingereza inasema, “mpira wa miguu Uingereza ni zaidi ya mchezo - ni sehemu ya historia yetu, urithi wetu, kitambulisho chetu cha taifa na utamaduni wetu wa pamoja. Ni habari ya mafanikio makubwa duniani, ikiruhusu mashabiki kuwaona baadhi ya wachezaji bora duniani wakicheza England kila wiki. Mafanikio haya yanajengwa juu ya ukuaji imara wa kibiashara, sehemu fulani ikitokana na uwekezaji kwenye klabu.

“Hii ndio sababu ofisi ya IFR itaanzishwa kwa njia ambayo inalinda mpira wa miguu wa Uingereza kama uwekezaji unaovutia na mashindano mazuri ya kimichezo, lakini pia kuhakikisha kuwa ukuaji unaoendelea wa mchezo huu, haufanyiki kwa klabu kupoteana na jamii zake au maslahi ya mashabiki.”

Najua baadhi ya watu huwa hawapendi kulinganisha mambo yanayofanyika Tanzania na ya nchi zilizoendelea kisoka ‘eti’ kwa sababu zilishapiga hatua kubwa, lakini najua hakuna mwanariadha anayekimbia akimuangalia aliye nyuma yake, bali aliye mbele. Hata kama aliye mbele amemzidi kwa mbali sana, jitihada zake za kutaka kumfikia zinaboresha muda wake binafsi hata kama hashindi mbio hizo.

Tunajua kuwa mpira wa miguu wa Uingereza uko mbali sana kiuendeshaji na kibiashara, lakini hiyo haitufanyi tubweteke na kuridhika kwamba ‘eti’ hatuwezi kufanya jitihada zozote kuiga wanachokifanya. Ni lazima tupige hatua kwa uwezo wetu ili angalau tufikie theluthi moja ya wanachokifanya kwa kuwa hiyo itatunufaisha hata kama hatutalingana nao.

Nitaendelea kutumia muswada huo katika safu zangu mbalimbali kuonyesha wenzetu wanavyopiga hatua kisayansi kila kukicha ili tuone wapi tunaweza kufanyia marekebisho hata kama si kwa kiwango kinacholingana na Waingereza pamoja na nchi nyingine zilizotuzidi kimaendeleo.

Jambo ambalo leo nimependa kulichomoa kwenye muswada huo ni suala linalohusu kuheshimu mashabiki na mabadiliko ya umiliki wa klabu. Inaelekea kama huku tumeamua mwenye fedha afanye anachotaka, klabu zijiamulie zinachotaka na chochote kifanyike ilimradi klabu zitimize wajibu wake wa kucheza mechi za ligi hata kama zitahamia sehemu ambayo hazikubaliki kwa mashabiki.

Klabu zinatangaza kuhama viwanja kana kwamba zina uhakika wa kupata mashabiki kokote ziendako. Klabu zinabadilisha umiliki kana kwamba si suala zito na mambo mengine mengi. Leo hii, mfano mdogo tu kuna ile sinema ya Ihefu Sports Club kubadilishwa jina na kuwa Singida Black Stars Football Club na imehamishia makao yake mkoani Singida ikitokea Mbeya, ambako ilijenga jina na kuanza kuvutia mashabiki.

Na wamiliki wanaosadikika kuwa walikuwa wanaimiliki Singida Fountain Gate, ambayo msimu huu mwanzoni ilikuwa ikijulikana kama Singida Big Stars (SBS), ndio wanaosadikiwa kuwa wamiliki wa Singida Black Stars (SBS).

Ile Singida Fountain Gate inatarajiwa kuhamia mkoani Mwanza ambako muda si mrefu nayo huenda ikabadilishwa jina. Si rahisi timu yenye jina la mkoa mwingine icheze Mwanza kama ndio makao yake makuu.

Kwa maneno mengine, ile Ihefu Sports Club, ambayo kwa misimu miwili imetingisha soka kwa kuwa klabu ya kwanza kuifunga Yanga, imefarakana na dunia kama ilivyokuwa ile Singida United na Singida Big Stars. Jamii ya Singida inayumbishwa isijue ifanye nini.

Bila shaka mashabiki wamechanganywa na mabadiliko hayo na ni ngumu kuona mantiki ya wamiliki kuachana na Singida Fountain Gate na kuinunua Ihefu, ikichukua baadhi ya wachezaji muhimu na baadaye ikaibadili jina na kuwa Singida Black Stars. Hizi ni sinema ambazo hatujui zinalenga nini huko mwishoni, huku mamlaka za soka zikisema hazijui hata wamiliki wa baadhi ya klabu.

Kwa mujibu wa muswada huo wa serikali ya Uingereza ambao utaanzisha utoaji wa leseni kwa klabu tofauti na ule mfumo wa Chama cha Soka (FA), wamiliki na wakurugenzi watafanyiwa tathmini kubwa zaidi kuziepusha klabu kuingia kwenye mikono isiyo sahihi na wakionekana hawakidhi vigezo, wanaweza kuondolewa na kuzuiwa kumiliki klabu.

Maana yake hapo hakutakuwa na mmiliki “asiyejulikana” kama ilivyo hapa kwetu na hivyo uwezo wake wa kustahimili mikiki ya kiuchumi utakuwa bayana. Tabia ya kuuzauza klabu imetawala sana kwenye klabu nyingi za Championship, Ligi Daraja la Kwanza na hata hili la Ligi Kuu kutokana na kutokuwepo na vigezo vya wamiliki na hata wakurugenzi wanaopewa majukumu ya kusimamia klabu.

Na kwa sababu biashara ya klabu haijawa kubwa, basi tunaona ni jambo la kawaida tu kwa wamiliki wa klabu kuiuza kila wanapofikiria kufanya hivyo, bila ya kujali maslahi mapana ya mchezo wa mpira wa miguu, na hasa mashabiki.
Muswada huo pia utawapa mashabiki sauti kubwa zaidi katika uendeshaji wa klabu na kuzuia wamiliki kubadilisha majina ya klabu kwa utashi wao binafsi. Pia mashabiki watakuwa na sauti kubwa zaidi katika masuala ya kubadilisha jezi za nyumbani na nembo.

Kwa hiyo ushirikishwa wa mashabiki (fans engagement) unaonekana ndio suala kuu katika kufanikisha mambo hayo.
Hii inamaanisha klabu zitatakiwa zianzishe bodi ya ushauri ya mashabiki ili wahusishwe katika maamuzi makubwa ya klabu yanayowahusu au kuanzisha mtandao mpana wa mawasiliano kwa ajili ya kuomba ridhaa ya mashabiki iwapo zitataka kubadilisha jezi za nyumbani za timu, kubadili uwanja na nembo na zitatakiwa ziwasilishe ushahidi wa ridhaa ya mashabiki kwa Mdhibiti wa Klabu za Mpira wa Miguu, ambaye anahusika na utoaji wa leseni kwa klabu, nje ya ule utaratibu wa mchezo wenyewe.

Kwa maana hiyo, leo Ihefu Football Club ingekuwa inasubiri ridhaa ya mashabiki (si wanachama) kubadili jina na kuwa Singida Black Stars, jambo ambalo lisingefanyika kwa wepesi kwa sababu mashabiki wana mchango wao wa kuiwezesha Ihefu kufikia mafanikio yaliyotamaniwa na wawekezaji wapya.

Leo Singida Big Stars ingebidi isubiri mashabiki wakubali klabu yao kuitwa Singida Fountain Gate na kubadili hata jezi inazotumia nyumbani, ikizingatiwa kuwa baadhi wameshanunua mfano wa jezi hizo (replica) kwa ajili ya mechi za nyumbani.
Lakini kwa kuwa limeshafanyika, ni dhahiri kuwa mashabiki wa Singida na Ihefu hawajashirikishwa kwa lolote, au maana ya moja kwa moja ni kwamba wamepuuzwa.

Nchini Uingereza serikali ilistushwa na uamuzi wa klabu za Manchester United, Arsenal, Liverpool, Tottenham Hotspur na Manchester City kuwepo kwenye mpango wa mashindano mapya ya European Super League, ambayo wengi waliona klabu hizo zilipuuza utashi wa mashabiki wake kutokana na kuwa na wamiliki wasiojali masuala hayo. Na ikatoa maelekezo na baadaye mpango wa ligi hiyo ukafa.
Ndio maana muswada huo unazizuia klabu za Uingereza kujiunga na mashindano maasi yoyote hadi ijue utashi wa mashabiki wake (si wanachama).

Kuhusu hali ya kiuchumi ya klabu, serikali iliona tatizo hilo kwa upana zaidi wakati klabu ya League Two, ya nne kwa ngazi kutoka Ligi Kuu, ya Bury ilipoanguka kifedha ghafla mwaka 2019. Mwaka huo, yaani msimu wa 2018-19, Bury ilishika nafasi ya pili ya League Two na hivyo kupanda kwenda League One. Lakini ikashindwa kuanza msimu kutokana na matatizo ya muda mrefu ya kifedha na kusababisha itimuliwe League One.

Serikali ilianza kufikiria jinsi ya kuzinusuru ligi baada ya tukio hilo na ndipo ilipoahidi kuja na muswada utakaodhibiti hali hiyo.
Kwa hiyo hizi sinema za Singida Fountain Gate, Singida Big Stars, Singida Black Stars na Ihefu Football Club hazina budi kuangaliwa katika upana wake kabla ya ligi kuja kupata tatizo la timu kulazimika kujiondoa kwenye ligi baada ya raundi kadhaa na hivyo kubadilisha kabisa msimamo. Naelewa kuwa Arusha Football Club ilijitoa Ligi Daraja la Kwanza na kulilazimisha Shirikisho la Soka (TFF) kufanya kazi ya ziada kuhakikisha inamaliza majukumu yake badala ya kufuta matokeo.

TFF na Bodi ya Ligi Kuu hazina budi kufikiria jinsi ya kudhibiti mabadiliko haya na kuyapa kipa umbele maslahi ya mashabiki ili klabu zisijifanyie mambo kiholela kutokana na utashi wa wamiliki. Na athari yake ni kwamba ukubwa wa Simba na Yanga unaongezeka maradufu kwa kuwa mashabiki wa klabu nyingine hawazalishwi na hao waliopo wanachanganywa na maamuzi ya wamiliki kuhamisha mechi hovyo, kubadili majina na kubadili hadi makao makuu.

Na TFF isipoona kwa jicho la kijanja sinema hii ya Singida Fountain Gate, Singida Black Stars na Ihefu Football Club, nani anajua kinachofuata?
Labda serikali itaona umuhimu wa mashabiki na kuingilia kati kama Uingereza ilivyofanya. Na hapo hakutakuwa na  ile dhana ya eti “serikali inaingilia kati” kwa kuwa usajili na umiliki ni mambo yaliyo ndani ya nchi. Mwandishi wa uchambuzi huu ni Katibu wa zamani wa TFF. Maoni: +255 658 376 417