Simba yapiga mkwara mzito

Friday October 02 2020
simba pic

BENCHI la ufundi la Simba limewapiga mkwara mzito na kuwakumbusha wachezaji wake mechi saba za Ligi Kuu msimu uliopita na kuwataka kuzikumbuka kwa jicho la pili kabla ya kushusha mguu uwanjani dhidi ya JKT Tanzania, Jumapili hii kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Mechi hizo ni zile ambazo Simba ilipata ushindi katika viwanja vya mikoani ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa kwa kutokuwa na eneo zuri la kuchezea kulinganisha na vile vilivyopo jijini Dar es Salaam ambavyo ni Benjamin Mkapa, Uhuru na Azam Complex.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu ameiambia Mwanaspoti kuwa wachezaji wa timu hiyo wanapaswa kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo kwani hakuna sababu itakayoeleweka kutoka kwao ikiwa hawatopata ushindi.

“Kiuhalisia ni viwanja vichache tu hapa nchini ambavyo vina eneo zuri la kuchezea na ukivihesabu havizidi vitano sasa huwezi kuwa bingwa kwa kutegemea ushindi katika kiwanja kimoja tu au viwili ni lazima upate matokeo mazuri katika viwanja hivyo vinavyoonekana havina ubora kwa sababu ndio mazingira tuliyonayo.

“Msimu uliopita, hapo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa tulipoteza dhidi ya Yanga, Mbao na tukatoka sare na Ruvu Shooting lakini pia kwenye Uwanja wa Uhuru, tulifungwa na JKT Tanzania na tukatoka sare na Prisons. Hata hivyo, tulipata ushindi katika viwanja vingi mikoani.

“Hivyo tunaenda kucheza na JKT Tanzania katika Uwanja wa Jamhuri tukiwa tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunaibuka na ushindi lakini suala la ubovu wa eneo la kuchezea sio la kulitumia kama utetezi hivyo wachezaji wanatakiwa kupambana ili tuweze kuibuka na ushindi,” alisema Rweyemamu ambaye ni mzoefu ndani ya Simba.

Advertisement

Rweyemamu alisema kuwa Simba inaelekea Dodoma leo ikiwa na kikosi cha wachezaji 27 na watamkosa mmoja tu ambaye ni Gerson Fraga aliye majeruhi.

“Simba tuna wachezaji 29, ukimuondoa Cyprian Kipenye ambaye ameenda kwa mkopo Ihefu, wanabakia 28 ambao kati ya hao, ni Fraga tu ambaye hatosafiri kwa sababu ya kuuguza majeraha yake, wanabakia 27 ambao wote wako fiti na watasafiri na kocha anaweza kumtumia yeyote kulingana na mipango na mahitaji yake.

“Kubwa tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti ili tuibuke na ushindi katika mchezo huo lakini kwa maana ya morali na hamasa viko juu na wachezaji wana hamu ya kuipatia timu ushindi,” alisema Rweyemamu

Simba itacheza na JKT Tanzania ikiwa na kumbukumbu ya kuvuna pointi nne katika mechi zake mbili za mwanzo ilizocheza ugenini katika viwanja vya Sokoine (Mbeya) na Jamhuri (Morogoro) dhidi ya timu za Ihefu na Mtibwa Sugar ambazo hata hivyo haikuonyesha kiwango cha kuvutia, ikifunga mabao matatu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.

Hata hivyo, katika mechi mbili zilizofuata iliyocheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Biashara United na Gwambina FC, ilipata ushindi katika mechi zote huku ikifunga mabao saba pasipo kuruhusu nyavu zao kutikiswa.

Msimu uliopita, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Biashara United katika Uwanja wa Karume Musoma, ikaifunga Mbao FC mabao 2-1 na Alliance kwa mabao 4-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Lakini pia iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Jamhuri, ikawapia mabao 2-0 Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya na ilishinda bao 1-0 dhidi ya Lipuli katika Uwanja wa Samora, Iringa huku pia ikishinda mabao 2-1 mbele ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi.

Hata hivyo, Simba ilifungwa bao 1-0 na Mwadui kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na ilitoka sare dhidi ya Prisons, Ndanda, Namungo FC na Coastal Union.

 

Advertisement