Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yapata dawa ya Asec, wenyewe waingia ubaridi Dar

MTOTO hatumwi dukani, ndivyo unavyoweza kusema kwa pambano leo kati ya Simba na Asec Mimosas ya Ivory Coast zitakapokutana kwenye mechi ya kwanza ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwani wenyeji wamepata dawa.

Simba itakuwa wenyeji wa Asec katika pambano hilo litakalopigwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, huku kocha wake, Pablo Franco akiipata dawa ya wapinzani wao ambao sio wa kubezwa.

Hii ni awamu ya sita kwa Simba kushiriki Kombe la Shirikisho, japo ni mara ya kwanza kwao kucheza makundi, huku katika awamu yao ya kwanza 2007 iliishia hatua ya awali, 2020 waliishia raundi ya kwanza, 2011 waliishia hatua ya mchujo, 2012 na 2018 waliishia raundi ya pili na ya kwanza.

Kwa upande wa ASEC hii itakuwa mara yao ya tisa kushiriki Kombe la Shirikisho na ndani ya awamu hizo wametinga hatua ya makundi mara tatu ambapo ni kwenye miaka ya 2011, 2014 na 2018.

Katika kuhakikisha inafanya vizuri kwenye mchezo huo wa kwanza hatua hiyo ya makundi kwa msimu huu wa 2021/22 ambao ni wa 19 tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo, kocha Pablo ameamua kuyapiga msasa majembe yake yatakayoanza kikosi cha kwanza.

Pablo amethibitisha hilo kwenye mazoezi ya timu hiyo na alianza kufanyia kazi mbinu zake kwa kugawa wachezaji wake kwenye makundi tofauti kulingana na nafasi ya mchezaji, kundi la makipa liliongozwa na Aishi Manula, mabeki wa kati na pembeni, viungo wa kati, viungo wa pembeni na washambuliaji wa kati.

Kwa upande wa makipa, Ally Salum na Aishi Manula walitakiwa kukaa langoni kila mmoja, kisha Pablo akiwa na ubao mdogo mkononi mwake wa kufundishia, akaanza kugawa wachezaji hao katika idara tofauti na kisha kuanza kuwaelekeza njia ambazo mpira unatakiwa kupita wakati wakishambulia.

Hilo lililikuwa funzo la kawaida ambalo wachezaji hakuna aliyekuwa akipewa presha kubwa ya kutekeleza kile ambacho alikuwa akielekezwa, mpira ulikuwa ukianzishwa kwa mabeki wa pembeni, ambao nao walitakiwa kwa uharaka kupiga pasi kwa mabeki wa kati au viungo muda mwingine ambao pua zao zilitakiwa kwa haraka kunusa na kupiga mipira mirefu kwenye maeneo ya pembeni.

Upande wa pembeni ambao mpira utapigwa ni tofauti kabisa na ule ambao shambulio lilianzia kwa haraka beki wa upande huo au winga muda mwingine anatakiwa kupanda kwa haraka na kupiga pasi chonganishi ndani, viungo wanatakiwa kusogea eneo hilo ili kuongeza namba ya washambuliaji.

Baada ya kumaliza jaribio la namna ya kushambulia, Pablo aligawanya vikosi viwili cha kwanza kiliundwa na Ally, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Hennock Innonga, Joash Onyango, Erasto Nyoni, Sadio Kanoute, Rally Bwalya, Pape Sakho, John Bocco na Mzamiru Yassin.

Kikosi cha pili, Manula, Israel Patrick, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Clatous Chama, Pater Banda, Jimmyson Mwinuke, Meddie Kagere na Yusuph Mhilu.

Vikosi hivyo vilipambanishwa, kikubwa Paplo alikuwa akisisitiza ile staili yao ya kushambulia ambao awali walikuwa wakiifanyia kazi, kila baada ya muda fulani alikuwa akimtoa machezaji fulani upande huu na kumpeleka upande mwingine.

Kocha huyo raia wa Hispania ni kama kuna kitu alikuwa akikitengeneza pale na aliona mchezaji huyu anashindwa kufanya vizuri kwenye mfumo huo akicheza na fulani kadri muda ulivyokuwa ukienda ndipo mazoezi yalivyokuwa yakichanganya na morali kwa wachezaji ikionekana kuwa kubwa.

Kuna muda kila mpira ukitoka, Pablo alikuwa anauweka mwingine uwanjani kwa haraka na kuwapa timu aipendayo faida ya kuanza mashambulizi yake, hilo liliwafanya wachezaji wa Simba mawazo na fikra zao kuwa mchezoni kwani upande ulioonekana kuzembea walijikuta ikiwagharimu.

Aliyeonekana lulu kwenye mazoezi hayo ni Sakho ambaye alitupia mabao mawili na kutengeneza nafasi kadhaa ambazo hata hivyo hazikutumika, wengine mbali na Msenegal huyo ni Gadiel, Mhilu, Banda na Kapombe ambao kila mmoja alitupia bao, Bwalya na Mzamiru walikuwa hatari kwenye eneo la kiungo.

Viungo hao walikuwa wakiachia mipira kwa haraka na kusogea kwenye maeneo mengine kutafuta tena nafasi kwa upande wa mabeki, Joash na Innonga walifanya vizuri nao kwenye mazoezi hayo ambayo yalifanywa kwenye uwanja wa Mo Simba Arena.


ASEC WATAKA POINTI MOJA

Kabla ya mabingwa hao wa Ivory Coast kuanza safari Jumatano ya kuja Tanzania kwa mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Simba, nahodha wa kikosi hicho, Cisse Abdoul Karim alihojiwa na chombo cha habari nchini humo na kusema si mbaya kama wataambulia pointi moja kwa Mkapa.

“Tunajiamini na tutafanya kila kitu kurudisha angalau pointi 1 kutoka kwa safari hii ya Dar Es Salam,” alisema nahodha huyo katika mahojiano ambayo alihojiwa Jumatano na Sports Ivoire muda mchache kabla ya kuanza kwa safari.

Kwa upande wa Kocha wa ASEC Mimosas, Julien Chevalier raia wa Ufaransa alisema; “Tumejiandaa vyema kwa mchezo huu. Hatuna majeruhi wala wachezaji walio na maambukizi ya virusi vya corona. Tutajitolea kwa kila kitu ili kupata matokeo mazuri huko Tanzania.”

ASEC waliondoka Abidjan asubuhi ya Jumatano kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Felix Houphouet Boigny saa 11:15, ikisimama kwa muda mfupi mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, saa 8:30 mchana kabla ya Alhamisi kutua kwenye ardhi ya Tanzania wakiwa wapole wakisikilizia pambano hilo la tatu kukutana na Simba baada ya ile miwili ya mwaka 2003 katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kila moja ikishinda nyumbani. Simba ikishinda Dar kwa bao 1-0 na kupasuka ugenini mjini Abidjan kwa mabao 4-3.


MACHO YA FEDHA

Ni mchezo ambao utakuwa na maana kubwa kwa timu zote katika kutengeneza mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Zawadi nono ya fedha ambayo kila timu inayotinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho inakuwa imejihakikishia, hapana shaka ndio inazidi kunogesha na kufanya pambano la Simba na Asec Mimosas leo kuwa la aina yake.

Kila timu itakayotinga hatua ya robo fainali itajihakikishia kitita cha Dola 350,000 (Sh809 milioni) lakini kinaweza kuzidi kwa timu zitakazofika nusu fainali, fainali au kutwaa taji.

Ikumbukwe bingwa wa mashindano hayo anavuna kiasi cha Dola 1.25 milioni (Sh2.9 bilioni), mshindi wa pili akipata kiasi cha Dola 625,000 (Sh1.4 bilioni) huku kwa zile zinazoishia nusu fainali kila moja inapata Dola 450,000 (Sh1 bilioni).


HASIRA ZA 1993

Hapana shaka mbali na kufanya vizuri kwenye kundi na kusaka fedha za hatua ya robo fainali, Simba wanaingia katika mchezo wa leo wakiwa na kumbukumbu mbaya dhidi ya timu kutoka Ivory Coast.

Mwaka 1993, Stela Abidjan ya Ivory Coast ilitia mchanga pilau la Simba baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 jijini Dar es Salaam katika mechi ya marudiano ya fainali ya lililokuwa Kombe la Caf (sasa kombe la Shirikisho) licha ya timu hizo kutoka sare katika mechi ya kwanza huko Ivory Coast.