Simba yaiwahi Yanga Kigoma, Barbara asema kazi imeisha

SIMBA imekuwa ya kwanza kutua kwa kishindo na mikwara ya aina yake mjini Kigoma. Juzi na jana vigogo wasiopungua 20 wa Simba wakiongozwa na wajumbe wa Bodi walitua Kigoma kwa ajili ya kuweka mambo sawa, huku wakitupia picha kibao mtandaoni kama tambo kwa watani zao ambao wanaonekana kwenda kwa tahadhari kubwa.
Mwanaspoti linajua mbali na wazito hao, tayari wazee wa klabu hiyo kutoka mikoa mbalimbali wakiongozwa na Hassan Dalali wapo huko kuhakikisha morali ya mashabiki na wanachama iko juu.
Yanga wao mpaka jana hawakuwa na tambo yoyote, lakini habari zinasema wataanza kuwasili kesho usiku na wanafanya mambo mengi kimyakimya.
Kikosi cha Simba kitatua Kigoma kesho Alhamisi kwa ndege huku Yanga wakitazamiwa kutua kesho hiyohiyo ila watakuwa mbali na mji. Kumbukumbu za mechi iliyopita ambayo Simba ililala 1-0 zimechagiza umakini wa mchezo huo wa fainali ya FA.
Yanga waliingia kambini Jumatano mara baada ya kutoka Dodoma walikokuwa kwenye mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Dodoma Jiji wakati Simba wameingia kambini jana Jumanne.
Kwenye msafara utakaoanza asubuhi, Simba hawatakuwa na wachezaji Ibrahim Ajibu, Jonas Mkude na Perfect Chikwende ambao hawapo kwa sababu mbalimbali, lakini wengine wote watakuwa sehemu ya kikosi hicho, wakati Yanga hawatakuwa na Michael Sarpong. Benchi la ufundi la Simba likiongozwa na kocha Didier Gomes katika kuhakikisha wanafanya vizuri lilitoa mapumziko ya siku moja kwa wachezaji.
Baada ya maandalizi ya siku mbili watakapofika Kigoma jioni yake watafanya mazoezi kwenye uwanja ambao utaendana na mazingira ya uwanja utakaochezwa mechi kwa siku tatu.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema: “Nasubiri kupatiwa ratiba na viongozi muda na siku ya kusafiri, nami jukumu langu ni kufikisha kwa wachezaji na benchi la ufundi, ila tunaingia kambini moja kwa moja leo (jana Jumanne),” alisema.
Kocha Gomes alisema: “Tunatamani kukamilisha msimu kwa kuchukua tena ubingwa wa ASFC mfululizo, lakini jambo zuri litakuwa tumewafunga wapinzani, tutafanya maandalizi ya kutosha na hilo tuna imani linawezekana.”
Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez alisema kama uongozi wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi hiyo.
Alisema jambo jema wamefanikiwa lengo la kutwaa ubingwa wa ligi.
“Ubingwa wa ligi ni kwa ajili ya wote ambao wanahusika na Simba, lakini kama uongozi bado tunashirikiana na benchi la ufundi na wachezaji kuona tunashinda fainali ya ASFC.
“Mechi ngumu lakini tutapambana viongozi kuwawezesha wachezaji na benchi la ufundi kutupa ushindi ambao ndio tunatamani kuupata.
“Kiujumla maandalizi yanaendelea kuona tunaishi katika malengo yetu ya kutetea ubingwa wa ASFC ambao tuliuchukua msimu uliopita,” alisema Barbara
Barbara aliwahi kuliambia Mwanaspoti kuwa kabla ya kupewa kazi hiyo Bodi ya Wakurugenzi ilimpa malengo matatu ndani ya msimu huu ametakiwa kuyatimiza, ikiwa ni kutetea ubingwa wa ligi, kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutetea ubingwa wa ASFC.