Simba nyumbani, Yanga ugenini

Wednesday August 03 2022
simba pic
By Eliya Solomon

RATIBA ya Ligi Kuu Tanzania Bara imetangazwa leo, Jumatano Agosti 3 na Bodi ya Ligi  kwenye wiki ya kwanza itashuhudiwa Yanga ikianza kampeni za kutetea ubingwa wake ikiwa ugenini kucheza dhidi ya Polisi Tanzania huku Simba ikiwa nyumbani kucheza dhidi ya Geita Gold.

Katika utoaji huo wa ratiba ya msimu ujao ambao pazia lake linatarajiwa kufunguliwa Agosti 13 kwa mchezo wa watani wa jadi, Simba dhidi ya Yanga, mtendaji mkuu wa bodi, Almasi Kasongo alisema imezingatia mambo kadha wa kadha ikiwemo kalenda ya CAF na FIFA.

"Msimu wa 2022/23 utakuwa na jumla ya michezo  240 kwa maana ya kuwa 120 nyumbani na  120 ugenini," alisema Kasongo n  kuendele,

"Tumezingatia ushiriki wa timu zetu kwenye mashindano ya CAF kwa maana ya kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa lakini pia tumengalia Ushiriki wa timu yetu ya taifa kwenye michuano ya CHAN na kufuzu kwa Afcon 2023."

Hakuishia hapo, Kasongo aliendelea kwa kutoa ufafanuzi kuhusu ratiba hiyo kwa kusema imezingatia uwepo wa michuano ya Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) na Ile ya Mapinduzi ambayo hufanyika Januari.

"Wakati wa Kombe la Dunia Ligi yetu itaendelea kwa sababu hakuna timu inayotoa wachezaji kuanzia watatu kwa mujibu wa kanuni," alisema.

Advertisement

Mchezo wa kwanza wa msimu baada ya pazia kufunguliwa Agosti 13, utakuwa Agosti  15 kati ya Ihefu dhidi Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Highland Estate huko Mbeya.

Agosti 16, Polisi Tanzania itaikaribisha Yanga kwenye uwanja wa Shekh Amri Abeid, Arusha, Simba itacheza dhidi ya Geita Gold, Agosti 17 kwa Mkapa.

Mchezo wa kwanza wa watani ya jadi msimu ujao achana na ule wa ufunguzi, utachezwa, Oktoba 23 ambapo Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye raundi ya nane.

Advertisement