Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shaibu Ninja : Jamani huku Marekani kila mtu kivyake tu

Muktasari:

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalum na Ninja ambaye amezungumzia maisha mapya ya Marekani hasa ya klabu ya LA Galaxy miundombinu yao na staili ya jinsi wanavyoishi.

MWENYE bahati habahatishi, hilo limejidhihirisha kwenye maisha ya beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye alijiunga na Wanajangwani kwa mara ya kwanza 2017, akitokea Taifa Jang’ombe ya Zanzibar.

Baada ya mwaka huu kumaliza mkataba wake Yanga, ambao ulikuwa wa miaka miwili, Ninja alipata dili nono la kusaini miaka minne katika timu ya Jamhuri ya Czech ya Ligi Daraja la Tatu inayojulikana kama MFK Karvina.

Bado bahati iliendelea kumfuata kwani timu hiyo iliamua kumpeleka kwa mkopo wa mwaka mmoja katika klabu ya LA Galaxy ya Ligi Kuu ya Marekani ambako alikwenda kuanza kwenye kikosi B.

Ninja wakati anajiunga na Yanga alifanyiwa sherehe na timu yake ya Taifa Jang’ombe, bado utaratibu huo uliendelea alipopata dili la nje pia Zanzibar ambapo walimuaga kwa kumuandalia mechi.

Lakini pia alipata bahati ya kupewa jezi aliyokuwa anaitumia nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ baada ya kustaafu ambaye aliukubali uwezo wa Ninja akisema atajisikia raha akiendelea kuiona jezi hiyo uwanjani.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalum na Ninja ambaye amezungumzia maisha mapya ya Marekani hasa ya klabu ya LA Galaxy miundombinu yao na staili ya jinsi wanavyoishi.

KILA MTU KIVYAKE

Ujamaa uliopo Tanzania ambapo utakuta wachezaji wanaishi kama ndugu wa kutoka familia moja, Ninja anasema kwa Marekani ni tofauti ukaribu wao ni wakati wa mazoezi na mechi.

Ninja anasema wameshapewa nyumba ya kuishi yeye na wachezaji wenzake, lakini hakuna mtu aliye na muda na mwenzake, kila mtu anafanya mambo yake isipokuwa wakiwa mazoezi na mechi ndipo wanapoweza kupiga stori mbili, tatu.

“Hakuna mtu aliye na muda na mwenzake, tukirejea kutoka mazoezini kila mtu anaingia chumbani kwake, hakuna cha kupiga stori wala kukaa pamoja kucheka. Hata TV iliyopo sebuleni katika nyumba ya kushea tunayoishi wachezaji haijafungwa maana haina mtazamaji (iko kwenye maboksi yake tu),” anasema.

MAISHA YA MAREKANI

Anasema miundombinu yao ni mizuri kuanzia mitaa hadi namna wanavyoendesha soka lao kisasa, jambo analoona linawarahisishia wachezaji wenye vipaji kufika mbali.

Ninja anasema Marekaniwameendelea katika mambo mengi, licha ya kuwa kila mtu anafanya mambo yake na hakuna anayefuatilia maisha ya mwingine na kwamba miundo mbinu ya soka ni imara.

“Kwanza viwanja vya mazoezi vipo vingi, timu moja inaweza kuwa na viwanja 10 ama zaidi, nakumbuka wakati natambulishwa nilipelekwa kuona viwanja vingi sana.

“Viwanja vyao ni bora hata mchezaji ukicheza unakuwa huru. Yale mawazo ya kuumia hovyo yanakuwa hakuna,” anasema.

MWENDO NI NDEGE TU

Anasema kwa kuwa usafiri wao ni ndege tu kila waendapo kwenye mechi za ugenini, inawasaidia wasijisikie uchovu licha ya ratiba ngumu ya mechi. “Ndio maana nimesema miundo mbinu yao ni mizuri, wachezaji wa huku wanafanikiwa kirahisi kwa sababu mengi wamerahisishiwa,”

“Hatutumii muda mwingi njiani ni saa chache ama dakika kadhaa tu tunakuwa tumefika sehemu husika ya kucheza mechi,” anasema.

UTARATIBU WA TIMU YAO

Anasema kuna kitu cha tofauti alichokiona kwenye timu hiyo kwamba wakati wanakwenda mazoezini wanaandaliwa kifungua kinywa, uwanjani baada ya mazoezi wanapikiwa chakula.

“Baada ya mazoezi ama mechi tunapikiwa chakula, ukiamua kubeba unabeba kwenda kula unakoishi, usipopenda basi unakwenda kupika unachokipenda, yaani wachezaji wa huku kwa sehemu wana raha yake,” anasema.

WATAALAMU WA SAIKOLOJIA

Anasema mchezaji anapokosea, makocha na viongozi wa timu hiyo wanakuwa karibu naye kumjenga kwa upendo na kumwambia ndio mwanzo wa kufanya kitu bora zaidi.

“Wapo tofauti kidogo namna ambavyo wanakurekebisha kosa. Yaani ni kama vile hujakosea. Wakimaliza kuzungumza na wewe unapata hamu ya kujituma na umakini unakuwa unaongezeka zaidi,” anasema.

KIKOSI CHA KWANZA

Bado hajaanza kucheza kikosi cha kwanza, anacheza timu B ya LA Galaxy.

Lakini anasema atapandishwa siku za usoni kwamba ndivyo alivyoambiwa na kocha wake.

“Nilikuwa naangaliwa. Hii ni klabu kubwa. Nisingeweza kuanza kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja. Nilikuwa napewa maelekezo mengi ya namna ya kuendana na mazingira.

“Jambo ambalo kocha ananisisitiza mpaka sasa, ni kwamba ananitaka kuzungumza na wachezaji wenzangu niwapo uwanjani. Nimeanza kulifanya hilo ndipo ameniambia atanipandisha kucheza kikosi cha kwanza muda wowote kuanzia sasa.

“Pia aliniambia asingeweza kunianzisha moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza kwa sababu alikuwa anakisoma kipaji changu na kwamba tayari ameishanielewa.”

ZLATAN IBRAHIMOVIC NI WA AINA GANI

Anasema kwa ustaa alionao straika Ibrahimovic hakutegemea kama angekuwa mchezaji anayependa waliochini wafike juu, akimsifu kwamba ni mshauri mzuri na anayependa kujituma.

Anasema alipata wasaa wa kupiga naye stori mbili tatu kuhusiana na maisha ya soka, jambo kubwa alilomuambia ni nidhamu na juhudi anaamini atashangaza ulimwengu.

“Ameona baadhi ya mechi ambazo nimecheza, kaniambia nijitume nina kitu kikubwa mguuni kwangu, ana moyo wa tofauti wa kutaka waliochini waweze kuishi ndoto kubwa, sio pekee yangu anayenishauri. Wengi huwaambia hilo,” anasema.

ALIVYODHIBITI UPWEKE

Ninja anasema licha ya kila mchezaji kutokuwa na muda na mwingine, akijiona anasikia upweke ananyanyua simu kuwapigia rafiki zake wa Tanzania na baada ya kuzungumza nao, hali hiyo hutoweka. Pia anasaidiwa na uwapo wa mitandao ya kijamii kama WhatsApp, ambayo unaweza kuwa katika ‘magrupu’ yanayowaleta pamoja watu kutoka kokote waliko duniani.

“Naongea sana na marafiki zangu wa Tanzania kupitia simu, hivyo najikuta hali ya kuwa mpweke inanitoka. Nakuwa najihisi kama nipo pamoja nao, hilo halinisumbui kabisa,” anasema.

HAJAANZA KUTEMBELEWA

Sio kwamba Ninja ndiye Mtanzania pekee anayeishi Marekani, wapo wengi na hata yeye amekiri kuwasikia kuwepo lakini wapo mbali na sehemu anapoishi.

“Bado sijaanza kutembelewa na Watanzania wenzangu, wapo na baadhi yao nimewasaliana nao, wanaishi mbali na sehemu nilipo. Naamini ukipatikana muda nitakuwa na watu wengi wa kunitembelea na kuwatembelea,” anasema.

UPATIKANAJI WA CHAKULA

Ingawa vyakula vya Marekani ni tofauti na vya Tanzania anasema upatikanaji wake ni supamaketi. “Kuna supamaketi kubwa ambazo zinauza vyakula vya nchi zote, lakini ndio mpaka uzoee mazingira,” anasema.

ANAFANYAJE KUHUSU IBADA

Ninja ametokea Zanzibar ambako dini ya Kiislamu imetawala, alipoulizwa staili ya Marekani kila mtu na mambo yake je anafanyaje kuhusu kuswali. Alijibu Mungu yupo popote. Na anaswali alipo.