Sasii apewa mambo matano ya kuzingatia

Mwamuzi, Herry Sasii

MWAMUZI Herry Sasii amepewa mambo matano ili kuhakikisha anahitimisha salama ngwe ya dakika 90 ya dabi ya watani wa jadi Simba na Yanga hii leo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Sasii anachezesha kwa mara ya tatu dabi hiyo, awali ilikuwa ni ile ya Ngao ya Jamii ya msimu wa 2017/18 na kisha mechi ya Ligi ambazo zote zilimalizika kwa sare. Jana asubuhi, mwamuzi huyo alikuwa darasani kujiweka fiti zaidi kabla ya mchezo huo ambao waamuzi wenzake wamemtakia kheri, wakimuombea aukamilishe salama na kumpa mambo matano ambayo akiyazingatia yatanogesha dabi hiyo ya tatu kwa Sasii kuwa pilato.
“Kikubwa ni wote kumuombea na kumuamini, lakini sana sana asiingie na matokeo mfukoni,” alisema Abdulkadir Omary mmoja wa waamuzi waliowahi kuchezesha fainali za Afcon.
“Tunaamini waamuzi wote ni waaminifu, japo tofauti yao ni elimu na ufahamu sheria, kwa Sasii hadi kuwa na beji ya Fifa ana sifa zote na nasisitiza tena tumuombee atoe uamuzi wa halali bila upendeleo, mechi za dabi ni ngumu
Mwamuzi mwingine, Ibrahim Kidiwa alisema kikubwa ni umakini na uaminifu pia ahakikishe anadili na wachezaji uwanjani.
“Hakuna kazi ngumu kama ya kuchezesha dabi na mechi za Simba na Yanga zinakuwa na maneno mengi, kikubwa tumuombee Sasii na wasaidizi wake, awe watulivu na atoe uamuzi bila kuhofia upande wowote.
“Kama ni mahali pa faulo iwe ni faulo kweli, penalti au kadi basi afanye hivyo bila kuhofia hiyo ni dabi wala kujali mashabiki wanasema nini,” alisema.
Katika mchezo huo ambao Simba atakuwa mwenyeji, Sasii atasaidiwa na Kassim Mpanga na Hamdani Said wote kutoka Dar es Salaam na mwamuzi wa akiba ni Ahmada Simba wa Kagera.
Mtathimini wa waamuzi ni Soud Abdi wa Arusha na mechi Kamishna ni Hosea Lugano wa Lindi.
Afisa itifaki ni Jacqueline Kamwamu wa Dar es Salaam, Hashim Abdallah amepewa majukumu ya ulinzi, Afisa Masoko wa mchezo huo ni Fredrick Masolwa na Ofisa Habari ni Clifford Ndimbo.
Dawati la matibabu litaongozwa na Dk Norman Sabuni, msimamizi wa kati wa kituo ni Msanifu Kondo na Baraka Kizuguto atakuwa mratibu mkuu wa mchezo akisaidiana na Jonathan Kassano na Herieth Gilla.