Refa Yanga, Belouizdad shilingi itasimama

Mwamuzi Traore katika moja ya mechi za michuano ya CAF.

Muktasari:

  • Yanga inasaka rekodi ya kutinga robo fainali kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwani mwaka 1998 iliposhiriki makundi kwa mara ya kwanza iliishia kumaliza mkiani.

HISTORIA ya refa Boubou Traore (34) kutoka Mali, inazilazimisha Yanga na CR Belouizdad ya Algeria kila moja inapaswa kujipanga vilivyo wakati zitakapokutana Jumamosi kuanzia Saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Timu hizo zitavaana kwenye pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Kundi D, ikiwa ni marudiano baada ya awali Cr Belouizdad kushinda ikiwa nyumbani kwa mabao 3-0, huku zote zikiwa na pointi tano baada ya mechi nne kwa kila moja, nyuma ya vinara Al Ahly ya Misri yenye pointi sita ambayo yenyewe wikiendi hii itaumana na Medema ya Ghana.

Picha ya mechi ya awali kati ya Yanga na CR Belouizdad iliyochezwa Algeria na wenyeji kushinda mabao 3-0.

Refa Traore ndiye amepangwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kushika kipyenga katika mechi hiyo akisaidiwa na Sydou Tiama (Burkina Faso), Nodibo Samake (Mali) na refa wa mezani Ousmane Diakate kutoka Mali.

Refa huyo ameonekana kuwa na historia ya bahati kwa timu za kutoka ukanda wa nchi zinazozungumza lugha ya Kiarabu, lakini amekuwa na kumbukumbu mbaya kwa CR Belouizdad katika mechi ambazo amewahi kuichezesha dhidi ya wapinzani wake.

Katika mechi 10 zilizopita ambazo timu za Kiarabu zilicheza, huku refa akiwa Traore, ziliibuka na ushindi mara tisa na moja ikitoka sare, hata hivyo pamoja na timu nyingi kutoka Uarabuni kuwa na historia ya kufanya vyema ikichezewa na mwamuzi huyo, refa huyo amekuwa na nuksi kwa Belouizdad kwani haijawahi kupata ushindi au hata sare pale alipowachezesha.

Traore amechezesha mechi mbili za Belouizdad ambazo ya kwanza ni ile waliyocheza Februari 28, 2021 na Mamelodi Sundowns kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambayo timu hiyo kutoka Algeria ilichapwa mabao 5-1.

Februari 24, 2023, CR Belouizdad ilipoteza kwa bao 1-0 mbele ya Al Merrikh ya Sudan, huku refa wa mchezo akiwa ni Boubou Traore.

Yanga inayoshika nafasi ya tatu kwenye kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika, inahitaji ushindi katika mechi hiyo dhidi ya Belouizdad ili ifikishe pointi nane na kuweka hai matumaini yake ya kuingia hatua ya robo fainali kabla ya kumalizana na Al Ahly mechi itakayopigwa mapema mwezi ujao jijini Cairo.

Kwa mujibu wa msimamo ulivyo kwa sasa, Al Ahly ndio inayoongoza, ikiwa na pointi sita ikifuatiwa na Belouizdad yenye tano kama ilivyo kwa Yanga, ila zinatofautia kwa mabao ya kufunga na kufungwa, kisha Medeana inashika mkia ikivuna pointi nne, huku kila kitu ikicheza mechi nne.

Hii ni mara ya pili kwa Yanga kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya awali kutinga mwaka 1998 na kuishia kuburuza mkia katika Kundi B.

Matokeo yoyote mazuri kwa Yanga kwenye mechi hiyo ya Jumamosi inaweza kuiweka kwenye nafasi nzuri ya kuandika rekodi ya kutinga robo fainali kwa mara ya kwanza tangu michuano hiyo ilipobadilishwa mfumo wake mwaka 1997.