Rainford Kalaba mahututi ajali ya lori

Muktasari:

Kalaba, 37, amejeruhiwa baada ya gari ndogo aina ya Mercedes Benz aliyokuwamo ikiendeshwa na mwanamke ambaye hajafahamika kugongana uso kwa uso na lori.

ALIYEKUWA nahodha wa TP Mazembe na timu ya taifa ya Zambia, Rainford Kalaba yupo katika wodi ya wagonjwa mahututi huko Zambia baada ya kupata ajali ya gari iliyotokea katikati ya Kafwe na Lusaka, Zambia, leo.

Kalaba, 37, amepata ajali hiyo baada ya gari ndogo aina ya Mercedes Benz aliyokuwamo ikiendeshwa na mwanamke ambaye hajafahamika kugongana uso kwa uso na lori la mafuta.

Awali, staa huyu aliripotiwa kuwa amefariki kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TP Mazembe katika ukurasa wao wa mtandao wa Facebook kabla ya baadaye miamba hao wa Afrika kutoa taarifa nyingine iliyoeleza kwamba gwiji wao huyo hajafa bali yupo kwenye hali mbaya.

Kwa mujibu wa Polisi wa Zambia, “uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba ajali ilitokea baada ya gari aina ya Benz kujaribu kuipita gari nyingine bila ya tahadhari, na kusababisha kwenda kulivamia lori lililokuwa linakuja.”

Kabla ya kustaafu soka Julai mwaka jana akiwa na Mazembe, Kalaba alikuwa mmoja kati ya mastaa tegemeo wa timu hiyo akiisaidia kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2015 ambalo nyota mwenzake wa wakati huo Mbwana Samatta alimaliza mfungaji bora wa michuano hiyo na kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wanaocheza soka ndani ya bara hili.

Akiwa na Mazembe amewahi kucheza mara mbili dhidi ya Simba. Ya kwanza ni mwaka 2011, kwenye Ligi ya Mabingwa katika hatua za awali ambapo walishinda mechi zote mbili, pia wakakutana mwaka 2019 katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ambapo Mazembe ilipita kwa ushindi wa mabao 4-1 walioupata DR Congo baada ya mchezo wa mkondo wa kwanza hapa Dar es Salaam kumalizika kwa suluhu. Katika ushindi huo Kalaba alitoa asisti moja.

Kwa sasa anahudumu kama kocha msaidizi wa Mazembe, kibarua ambacho alipewa baada ya kutundika daruga.

Mbali ya mchango wake kwa Mazembe ambako kiujumla alicheza mechi 97 za michuano ya kimataifa katika miaka 12 aliyohudumu akishinda mataji 17 tofauti, pia alikuwa tegemeo katika timu ya taifa ya Zambia.

Kalaba alikuwepo katika kikosi cha taifa hilo kilichochukua ubingwa wa AFCON mwaka 2012, ambayo yeye alicheza mechi saba kwa dakika 90 na hadi anastaafu kuichezea timu ya taifa mwaka 2018, alishaichezea Chipolopolo mechi 108 na kufunga mabao 14.

Kabla ya kutua Mazembe mwaka 2010, Kalaba aliwahi kupita timu mbalimbali barani Ulaya akianzia timu ya vijana ya Nice ya Ufaransa kisha Braga, Gil Vicente FC na Leiria zote za Ureno. Pale Zambia aliwahi kuzichezea Kitwe United na Zesco.