Pep kabadili mfumo ghafla
Muktasari:
- Katika maandalizi ya mechi alizimulika kanuni zake tano kwa kuziandika ubaoni na kutengeneza mbinu zake za uchezaji kupitia kanuni hizo, baadaye mpango mzima ukawa akilini mwake ambazo aliendelea kuzifanyia kazi uwanjani kabla ya mechi kuanza
TOLEO lililopita kwenye kitabu cha Pep Confidential, mwandishi Marti Perarnau alianza kwa kuzungumzia mfumo na wachezaji ambao Pep angewapanga katika mechi yake na Dortmund pamoja na mazinira mengine ya mechi hiyo. Sasa endelea…
Wakati huo huo watakuwa wakimtumia kiungo aliye mbele ya mabeki wawili wa kati ambaye jukumu lake litakuwa ni kudhibiti mashambulizi ya kushitukiza ya timu pinzani na ambaye pia atakuwa tayari kurudi nyuma kuwasaidia mabeki wa kati pale atakapohitajika.
Pia atakuwa na mshambuliaji wa kati mwenye uwezo wa kuwafanya mabeki wanne wa timu pinzani wakae nyuma zaidi pamoja na mshambuliaji wa pili au kiungo mshambuliaji mwenye kuweza kucheza katika maeneo lakini pia atakuwa na ushirikiano mzuri na kiunganishi wa mshambuliaji wa kati.
Katika maandalizi ya mechi alizimulika kanuni zake tano kwa kuziandika ubaoni na kutengeneza mbinu zake za uchezaji kupitia kanuni hizo, baadaye mpango mzima ukawa akilini mwake ambazo aliendelea kuzifanyia kazi uwanjani kabla ya mechi kuanza. Msingi wake ni mfumo wa 3-6-1 ambao baadaye ungebadilika na kuwa 5-4-1 wanapokuwa katika harakati za kujihami na kisha kucheza katika mfumo wa 3-4-3 wanapokuwa katika harakati za kushambulia.
Mwisho wa yote Hojbjerg akapangwa upande wa kulia nyuma, Rafinha kushoto na Lahm na Kroos wakapangwa viungo wakiwa mbele ya mabeki wawili wa kati, Gotze alianzia mbele kushoto, Muller mbele kulia huku, Robben akawa ndiye mtu muhimu mbele linapokuja suala la mashambulizi katika pande hizo tatu.
Pindi Dortmund wanapokuwa na mpira, Robben alikuwa na uhuru wa kuwakabili kwa nguvu zote kadri ilivyoona ana uwezo, lakini mbali na hilo, Gotze na Muller nao walikuwa na jukumu la kuwazibia njia Dortmund huku Lahm na Kroos wakiwa nyuma, yote hiyo ikuwa ni kuwapa presha wapinzani wao.
Bayern watakiwa wakicheza kimtego zaidi, watakuwa wenye kuwasubiri Dortmund na safu ya ulinzi itakuwa ikiziba njia nyuma zaidi kuliko ilivyo kawaida yao kwa kipindi chote cha msimu, hawakutaka kuipa timu ya Klopp (Dortmund, Klopp kwa sasa anainoa Liverpool) nafasi yoyote.
Rangi ya njano ya Dortmund ilitawala Uwanja wa Olympic mjini Berlin, ilikuwa hivyo hivyo kwa nyimbo ambazo ziliimbwa mwanzo mwisho na mashabiki wa timu hiyo.
Kuanzia dakika ya kwanza, Klopp na kikosi chake walichanganywa na Bayern mpya, hiki si kile kikosi ambacho kingewafanya wakurupuke na kuwashambulia na kuacha nyuma kukiwa wazi.
Ghafla kukawa na kitu tofauti, na hata kabla ya kubaini mabadiliko, Muller nusura aandike bao, mpira ulimgonga kipa Weidenfeller na Robben, ambaye hakuwa mbali alipatiwa nafasi ya pili iliyotokana na pasi ya uhakika uliyomfikia mguu iliyopigwa na Lahm.
Dortmund ni kama vile walipoteana, kwa kawaida ni wataalam katika kutengeneza mitego ya kuotea, wanawaacha wapinzani wao wasogee hadi eneo lao la goli kwa raha zao, ni kama vile muwindwaji aliyeachwa ajipange lakini hajakaa vizuri anastukia anayemuwinda kamvaa na kumgawanya vipande vipande.
Na kama ilivyo ada kwa Pep nguvu na uimara wa timu yake aliuweka katika eneo la kiungo, katikati ya uwanja, aliwaacha wachezaji watatu katika eneo la katikati nyuma na wengine sita wakijimwaga na kupambana eneo la kati.
Kaika mazingira hayo ya kushangaza, Dortmund walijikuta wakishindwa kujibu mapigo, presha waliyojaribu kuitengeneza kwa Bayern wakitumia washambuliaji wao haikuwa na madhara kwa Bayern kutokana na wingi wa wachezaji wa Bayern katika eneo la kati.
Kwa hali hiyo Pep akawa na mashambulizi kidogo ingawa yote yalikuwa hatari. Alichofanya ni kupendelea na staili hiyo huku akimiliki zaidi mpira, Robben alikuwa peke yake mbele, lakini aliwaweka roho juu mabeki watatu, mabeki wote wa kati pamoja na beki mmoja wa pembeni.
Ilipotokea Muller akawa huru na kumpa msaada wawili hao walitengeneza kitu hatari, hilo lilipojitokeza washambuliaji wawili wa Bayern walikuwa wakiwasumbua mabeki wote wanne wa Dortmund.
Maana yake ni kwamba viungo watano wa Pep wakati wote walikuwa bora kuwazidi wanne wa Dortmund katika mpambano wa eneo la kati ya uwanja.
Itaendelea Jumamosi