Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NYUMA YA PAZIA : Tatizo la Xhaka ni rula ya Vieira na Petit

Muktasari:

Miguu ya Petit ilikupa nini? Kila kitu ambacho Vieira angekupa. Lakini zaidi ni mguu wa kushoto ambao ulimzidi Vieira kwa kupiga pasi ndefu. Mwishowe kabisa mguu wake ungekupa mabao ya mbali. Lakini pia alikuwa mtu wa kadi nyekundu kama Vieira.

MWANDISHI wa Kiingereza aliyeitwa Will Sharp aliwahi kuandika. Alisema “Patrick Vieira na Emmanuel Petit wataendelea kuwa rula ya kupimia viungo wao wajao wa Arsenal”. Nadhani hakukosea sana. Ndio hakukosea.

Wakati mwingine hii rula ambayo Sharp anaizungumzia huwa inaitwa kwa lugha nyingine ya Kiingereza kama ‘To set the standard’. Yaani kazi ya mtu inapimwa zaidi kupitia kwa watu walioweka viwango fulani siku za nyuma. Miguu ya mirefu ya Vieira ingekupa nini? Kwanza kabisa tackling. Halafu pasi fupi. Halafu kukukokota mpira kwa ufasaha. Halafu wakati mwingine mabao. Halafu wakati mwingine kule uswahilini walipenda ‘kanzu’ zake.

Zaidi ya kila kitu, miguu yake ilikupa utawala wa mpira, kifua chake kikajaa ubabe. Haishangazi aliondoka katika Ligi Kuu ya England akiwa mchezaji aliyepewa kadi nyingi zaidi nyekundu kando ya kina Duncan Ferguson ‘Big Dan’.

Miguu ya Petit ilikupa nini? Kila kitu ambacho Vieira angekupa. Lakini zaidi ni mguu wa kushoto ambao ulimzidi Vieira kwa kupiga pasi ndefu. Mwishowe kabisa mguu wake ungekupa mabao ya mbali. Lakini pia alikuwa mtu wa kadi nyekundu kama Vieira. Nilimtazama Granit Xhaka akiondoka uwanjani wikiendi iliyopita akiwa amevua kitambaa cha unahodha na kukitupa chini. Nikawaza. Tatizo ni rula ya Will Sharp. Mashabiki walikuwa wanamzomea. Akatoa ishara ya kuwataka waendelee kumzomea. Akakinga mkono wake wa kushoto katika sikio akidai anataka kuwasikia zaidi.

Katika mstari wa kutokea, akampa mkono wa hasira kinda, Bukaya Saka, akamkwepa Unai Emery, akavua jezi yake na kutokomea katika vyumba vya kubadilishia nguo. Nadhani historia yake na Arsenal imeishia hapo. Hakuna kitakachoendelea tena.

Arsenal hawajawahi kumzomea nahodha wao. Sio Arsenal tu, ni ngumu kwa wazungu kuzomea wachezaji wao, hasa linapokuja suala la nahodha. Nini kinatokea kwa Xhaka? Kwanza kabisa ameshindwa kukaa katika rula ya kina Vieira na Petit.

Hutaweza kujua Xhaka ni kiungo wa aina gani. Anacheza rafu katika maeneo ya hatari na kusababisha penalti au faulo za nje ya lango ambazo zinaigharimu Arsenal. Amepata kadi nyekundu nyingi zaidi ya mchezaji yeyote tangu atue Arsenal.

Xhaka ni nani? Hana umahiri katika ukabaji wala ushambuliaji. Xhaka ni nani? Hana mabao mengi wala pasi nyingi za mwisho za mabao. Arsenal ililipa Pauni 36 milioni zaidi ya miaka mitatu iliyopita kwenda Borussia Monchegladbach kwa ajili ya Xhaka. Tatizo rula ya Vieira na Petit haijamtosha Xhaka pekee. Kina Abou Diaby, Denilson na wengineo pia haikuwatosha. Tatizo ni kwamba, kwa Xhaka rula haijamtosha na makosa yake yanayoigharimu Arsenal mabao ya wapinzani yanaonekana wazi.

Labda Diaby hakuwa Vieira wala Petit lakini hakuwa anacheza rafu zisizo za msingi katika boksi kama ile ambayo Xhaka alimchezea Son Heung-Min na kuzalisha penalti pambano dhidi ya Tottenham. Labda ndio maana hakuwahi kuzomewa. Xhaka amegoma kuomba radhi, amekejeli mashabiki wanaomzomea. Kabla ya haya angeweza kuomba mikanda yake ya video na kujitazama tena. Na kabla ya hapo pia angeweza kuomba mikanda ya Vieira na Petit. Angejiweka katika rula ya Will Sharp.

Mwishowe angegundua kitu. Angegundua kuwa analipwa zaidi ya Pauni 100,000 kwa wiki kutoka katika pesa ambazo zinatoka katika mashabiki waliomzoea ambao huwa wanalipa viingilio na kununua jezi za klabu.Zaidi ya yote, hao mashabiki wanalijua eneo lao la kiungo. Hata kama kina Diaby halikuwatosha, lakini kulikuwa na watu liliwatosha nje ya Vieira na Petit. Kina Gilberto Silva, Edu na Cesc Fabregas walilitendea haki. Na hata kabla ya Vieira na Petit basi David Platt na Paul Merson walilitendea haki eneo hilo.

Mashabiki wa Arsenal wanapomzomea Xhaka sio kwa sababu wanamuonea. Ni kwa sababu wanajua jinsi ambavyo kuna watu walilitendea haki eneo hilo. Xhaka asingekasirika. Angejitafakari.