Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyuma ya Pazia: Eden Hazard anaacha machozi nyuma yake

Muktasari:

Hazard anakwenda Santiago akiwa anavaa jezi namba 7 na anakwenda kucheza upande wa kushoto aliokuwa anacheza Cristiano Ronaldo. Hazard sio Ronaldo, lakini Hazard sio Alex Iwobi wala Marcus Rashford. Machozi lazima yawatoke mashabiki wa Ligi Kuu ya England. Sio Chelsea peke yake.

WAKATI dunia ikisheherekea Sikukuu ya wajinga Aprili Mosi, 2010, Mwandishi wa Gazeti la Marca la Hispania, Carlos Carpio alikuwa akimhoji Zinedine Zidane kuhusu kinda anayemvutia kwa wakati huo. Alimtaja Eden Hazard wa Lille.
“Ni swali gumu ngoja nifikirie,” alisema Zidane mbele ya meza ya Carpio, kisha akaendelea: “Ohh nimempata. Naweza kukuambia ni mzuri sana.Ni Mbelgiji, anachezea Lille ya Ufaransa na anaitwa Eden Hazard. Ni mwepesi, anakimbia zaidi kushoto, lakini anaweza kubadilika kwenda kulia. Ana akili sana na atakuwa mchezaji mkubwa. Naweza kumchukua kwenda Madrid huku nimefumba macho.”
Baadaye Hazard alikwenda kuzurura England na wiki hii ametua rasmi Real Madrid. Hazard kwa Kiingereza maana yake majanga. Na alikuwa majanga kweli. Florentino Perez amelipa Pauni 115 milioni kwa mchezaji aliyebakiza miezi 12 tu katika mkataba wake. Haijawahi kutokea.
Hazard anakwenda Santiago akiwa anavaa jezi namba 7 na anakwenda kucheza upande wa kushoto aliokuwa anacheza Cristiano Ronaldo. Hazard sio Ronaldo, lakini Hazard sio Alex Iwobi wala Marcus Rashford. Machozi lazima yawatoke mashabiki wa Ligi Kuu ya England. Sio Chelsea peke yake.
Hazard alipendwa na kila shabiki wa Ligi Kuu ya England. ungemchukia katika mechi moja tu, Chelsea dhidi ya timu yako. Mechi nyingine zote ungependa Hazard awakomeshe adui zako. Shoo ya mwisho ya kibabe alipiga dhidi ya Arsenal pale Baku.
Hazard anajua kumiliki mpira, kukaa nao muda mrefu, kuufanyia matokeo ya uhakika. Hazard akicheza dhidi ya timu yako hauna raha. Kwanza unacheza na Hazard, kisha unacheza na Chelsea. Ina maana unaweza kuikamata Chelsea, lakini usimkamate Hazard. Ina maana Chelsea wanaweza kucheza ujinga lakini Hazard akaamua mechi. Anaitia mfukoni kisha anaondoka zake kwenda nyumbani kulala.
Hauwezi kumchukia Hazard. Hana tabia za maudhi. Hajirushi, sio mgomvi, yuko bize na kazi yake ya kupiga chenga kule kushoto na kufunga. Miaka yote Hazard yupo katika ubora uleule wa siku zote mpaka pambano lake la mwisho dhidi ya Arsenal Baku. Hazard sio Ronaldo wala Messi. hawezi kufunga mabao 50 ya msimu. Lakini ndio maana pia Messi na Ronaldo ni wachezaji wa kipekee. Hata hivyo, Hazard atakupa usumbufu mwingi ambao pia unawafungulia njia wenzake.
Usumbufu wa Hazard una mambo matatu. Kwanza atakupa mabao. Pili atatengeneza nafasi za wenzake kufunga, lakini tatu anawapa Chelsea umiliki wa mpira ambao unawapa hofu wapinzani na kujikuta muda mwingi wakipanga mipango ya kuikabili Chelsea na Hazard kuliko kupanga mipango yao ya kwenda mbele. Kifupi ni kwamba Waingereza wanaita kitu hiki kama ‘Fear Factor’. Hakuna kocha ambaye atakwenda Stamford Bridge au atakuwa uwanja wake wa nyumbani bila ya kutengeneza mipango mizuri ya kumdhibiti Hazard.
Kuondoka kwake kuna maana nyingi tofauti. Kwanza kabisa La Liga imepora kipaji chake bora zaidi katika Ligi Kuu ya England. Mohamed Salah ametupa misimu miwili mizuri, Sadio Mane ametupa misimu mitatu mizuri, Eden Hazard ametupa misimu saba ya kusisimua.
Watu  wanaopenda utamu wa mpira na mambo yake, kule Hispania wameletewa ongezeko la Hazard kando ya Lionel Messi, Luis Suarez na wachache wengineo. Kama Barcelona Itamrudisha Neymar mwaka huu au mwakani itakuwa hatari zaidi. Kama Real Madrid itamchukua Kylian Mbappe mwaka huu au mwakani, itaongeza utamu zaidi.
Chini ya Ronaldo na Messi kulikuwa na kundi lililokuwa linaongozwa na Neymar sambamba ya Hazard.
Halafu ghafla akaibuka Mbappe. Wote hawa wakicheza La Liga nadhani litakuwa pigo kubwa kwa Ligi Kuu ya England.
Nilikuwa namsoma John Cross, Mwandishi wa Gazeti la Mirror la Uingereza. Alikuwa akilalamika kwamba Hazard ni pigo kubwa kwa Ligi Kuu ya England tangu Cristiano Ronaldo aondoke Julai 2009. Ndio, alikuwa anasema kweli. Mbaya zaidi kaenda Hispania kuongeza nguvu upande ule. Afadhali angeenda Italia. Hapo hapo unaanza kuwaza maisha ya Chelsea bila ya Hazard. Yatakuaje? Msimu uliopita huku ikiwa na Hazard ndani lakini bado ilishika nafasi ya tatu, tena baada ya Spurs kuzubaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa. Vipi kama baada ya Hazard kuondoka?
Soka la leo pale England usimpoteze mchezaji wako mahiri. Ushindani umekwenda juu zaidi tofauti na zile zama za Sir Alex Ferguson na Arsene Wenger pekee. Siku hizi unashindana na watu wengi. Unashindana hata na Tottenham Hotspurs, achilia mbali matumizi ya pesa ya Cty na kuibuka upya kwa Liverpool.