Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nani anampisha Mpanzu Simba?

Mp Pict
Mp Pict

Muktasari:

  • Ujio wa Mpanzu ni taarifa njema kwa mashabiki na makocha wa timu hiyo wanaoongozwa na Fadlu Davids, lakini fundi huyo lazima apangue mziki wa Wekundu

SWALI kubwa ambalo mashabiki wa Simba wanajiuliza kwa sasa ni kwamba ujio wa winga mpya, Elie Mpanzu pale kikosini ni mchezaji gani anakwenda kumpisha? Hiyo inatokana na namna ambavyo walivyokiona kikosi chao mpaka sasa.

Simba ambayo katika usajili wa dirisha kubwa msimu huu imeshusha wachezaji wapya 15 wakiwemo wazawa sita na wa kimataifa wanane, hivi karibuni imemuongeza Mpanzu ambaye ni raia wa DR Congo.
 
Mpanzu ambaye alihitajika ndani ya Simba tangu dirisha kubwa la usajili, hivi sasa amebakiza utambulisho tu huku tayari akiwa ameshavalishwa mavazi rasmi yenye nembo ya timu hiyo akiwa amefichwa kwenye hoteli moja kubwa jijini Dar es Salaam.

Ujio wa Mpanzu ni taarifa njema kwa mashabiki na makocha wa timu hiyo wanaoongozwa na Fadlu Davids, lakini fundi huyo lazima apangue mziki wa Wekundu hao kama sio kuondosha mtu kitu ambacho baadhi ya mastaa wanaocheza nafasi moja wanapaswa kuanza kujipanga mapema ili kuepuka kufyekwa mara baada ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa Desemba, mwaka huu.

UCHEZAJI WAKE
Mpanzu ni mshambuliaji wa pembeni mwenye ubunifu ambao umekuwa ukimsaidia kufungua ngome za wapinzani, akiwa anajua kutumia vizuri ufundi wa miguu na kupangua mabeki huku pia ana kasi, lakini anafunga mabao na kutengeneza. Pia anajua kupiga mipira ya adhabu ndogo mambo ambayo ndani ya Simba anatakiwa kuyaendeleza kama alivyofanya akiwa na AS Vita.

Katika hilo, amethibitisha akiwa na AS Vita ya DR Congo na hapa mchambuzi wa soka nchini humo, Masamba Mboya anamchambua.

Mboya anaamini Simba imefanya uchaguzi bora akisema: "Mpanzu anaweza kucheza winga zote mbili kwa ufanisi mkubwa, lakini hasa amekuwa akifurahia kulia. Sijaitazama Simba ya msimu huu katika mechi zake zote, lakini kwa ubora wa Mpanzu ambao amekuwa akiuonyesha akiwa na AS Vita nadhani anaweza kucheza timu yoyote ya Tanzania na kufanya vizuri tu.

"Unajua mawinga wengi wa ukanda wetu wamekuwa na wakati mgumu wa kufungua ngome ya timu ambayo inakaa nyuma muda mrefu (kupaki basi). Sasa Mpanzu ana uwezo huo kwa sababu ni mbunifu, ana ujuzi mkubwa wa kuchezea mpira mguuni, kuna kipindi alikuwa akihusishwa na TP Mazembe, lakini ingekuwa ngumu kutokana na utamaduni uliopo baina ya klabu hizo mbili."

Katika eneo la winga ya kulia, ndani ya Simba hivi sasa anacheza Edwin Balua ambaye juzi dhidi ya Al Ahli Tripoli ilibidi aanzie benchi na nafasi yake kuchukuliwa na Kibu Denis, lakini baadaye aliingia na kufunga bao la tatu la ushindi kwa Simba.

Kocha Fadlu kwa namna ambavyo amekuwa akibadilisha watu mara kwa mara eneo hilo la winga ya kulia, ni wazi bado anatafuta mtu sahihi wa kumtumia, hivyo usajili wa Mpanzu ambaye ni pendekezo lake unatajwa huenda amepata suluhisho.

Fadlu hii siyo mara ya kwanza anauambia uongozi kumuongezea watu kikosini kutokana na waliopo kutoridhishwa nao, kwani alifanya hivyo dakika za mwisho Simba ikamshusha mshambuliaji Leonel Ateba ambaye leo hii anamuweka benchi Steven Mukwala. Lakini pia alisababisha kuondolewa kwa Freddy Michael.

ATAONGEZA NINI
Ukiachana na winga ya kulia anapocheza Balua na Kibu ambao wote walifunga wakati Simba ikiichapa Al Ahli Tripoli kwa Mkapa mabao 3-1, lakini Mpanzu anaweza kucheza winga ya kushoto anapotumika zaidi Joshua Mutale ambaye ameonekana kuwa kipenzi cha Fadlu.

Mutale ambaye amejiunga na Simba msimu huu, amefanikiwa kucheza mechi zote za Simba alipokuwa fiti, alikosekana siku ambayo alipata majeruhi, hivyo inaonyesha wazi Fadlu hayupo tayari kuona jamaa huyo akikaa benchi kirahisi.

Lakini ukiangalia tofauti ya uchezaji wa Mutale, Balua na Kibu, kwa Mpanzu anaonekana kuwa na uwezo mzuri katika umaliziaji na hapa anaongelewa na beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu 'Ninja' ambaye kwa sasa anaichezea FC Lupopo ya DR Congo.

"Nimecheza dhidi yake msimu uliopita, Mpanzu sio mchezaji machachari tu, bali ana uwezo wa kufunga. Naweza kusema alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu kwa AS Vita. Pia ni mzoefu pamoja na kuwa na umri mdogo," alisema Ninja, beki wa zamani wa Yanga.

Kulingana na kile ambacho wamekuwa wakikifanya Balua na Mutale, kuongezwa kwa Mpanzu kuna maana kwamba Fadlu atakuwa na wigo mpana wa machaguo kulingana na aina ya wapinzani ambao atakuwa akikabiliana nao, lakini pia itamrahishia kufanya mabadiliko ya mchezaji wakati mechi ikiendelea kama alivyofanya majuzi kumtoa Kibu aliyefunga bao la kwanza na kuingia Balua aliyekwenda kufunga bao la mwisho.

Kuna wakati makocha huhitaji mchezaji mwenye sifa za Mpanzu kukabiliana na timu ambazo zinakaa nyuma sana au Mutale kwa ajili ya kutumia mianya ambayo imekuwa ikiachwa wazi na wapinzani kutokana na kasi aliyonayo na hata Balua mwenye uwezo wa kuingia ndani na kuongeza idadi ya viungo.

Kama haitoshi, Mpanzu pia anaweza kutumika kama mshambuliaji wa pili akicheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho yaani namba 10 katika mfumo ambao Simba inaweza kuutumia wa 4-4-2. Katika nafasi hiyo, anaweza kumtingisha Jean Charles Ahoua, hivyo eneo la mbele wachezaji waliopo lazima wajipange.

Balua anatakiwa kuamka sasa na kuwa winga hatari licha ya kufunga mabao mawili ambapo moja ni Ligi Kuu na lingine Kombe la Shirikisho Afrika.

Ndani ya uwanja, Balua bado hajafanikiwa sana kuwa mtu hatari akiwa na nafasi ya kuanza na sasa amekuwa pia akitokea benchi. Lakini pia Kibu naye inabidi aongeze umakini wa kutumia nafasi ili kuilinda nafasi yake la sivyo Mpanzu atawakilisha benchi wote.

HAWA WANACHOMOKA?
Mtihani mwingine kwa Simba ni nani atampisha Mpanzu kwenye kikosi hicho, lakini mpaka sasa kuna mastaa wawili mmoja wao atang'oka kumpisha winga huyo.

Simba inaweza kutumia nafasi ya kwanza ya kipa Ayoub Lakred ambaye kama atakuwa hajapona mpaka dirisha dogo linafunguliwa itakula kwake.

Simba haitakuwa na nafasi ya kujiuliza sana kwa Lakred wakati huu ambao Moussa Camara akiwa ameanza kwa moto mkali ndani ya timu hiyo akifanya mageuzi makubwa ndani ya kikosi hicho.

Nyuma ya Camara kuna Aishi Manula ambaye licha ya kurudi kwa kishindo, lakini bado amelazimika kusubiri nafasi yake ikichukuliwa na kipa huyo raia wa Guinea.

Mbali na Lakred, raia wa Morocco, mtu wa pili ambaye anaweza kupisha ni Mkongomani Fabrice Ngoma ambaye amepoteza nafasi kabisa kikosi cha kwanza.

ANAANZIA HAPA
Mpanzu hataweza kuichezea Simba kwa sasa kutokana na kuchelewa dirisha la usajili, ambapo Wekundu hao watamuongeza kwenye dirisha dogo litakalofunguliwa katikati ya Desemba, mwaka huu, atakapoanza kucheza mashidano yote.

Wakati usajili wa dirisha dogo ukitarajiwa kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu, Simba itakuwa na nafasi ya kuliongeza jina la Mpanzu na hapo ndipo ataanza kucheza mechi za mashindano kwani atakuwa na leseni kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kanuni za CAF zinaruhusu mchezaji atakayetumika kwenye michuano wanayoisimamia lazima awe na leseni inayomuonyesha anacheza ligi ya nchi gani.

Kutokana na hilo, Simba italazimika kutomtumia Mpanzu katika mechi zote za hatua ya makundi ambazo zitaanza kuchezwa kuanzia Oktoba hadi Desemba 15, kwa mujibu wa kalenda ya mashindano ya CAF.

Mchezaji huyo atakapoanza kutumika, kocha Fadlu ataamua kubadilisha mwenyewe hesabu zake za muundo wa winga huyo ambaye anaweza kucheza winga zote mbili na mshambuliaji wa pili.