NADO #1 - Asimulia msoto wake katika soka
MWONEKANO wa sura ya staa wa Azam FC, Iddy Seleman ‘Nado’ unaweza ukakudanganya na kuamini kama alikuwa mpenda dini fulani hivi kama Mkristo, basi utamuweka kwenye kundi la walokole au iwapo Mwislamu - utadhani ni mwenye imani kali.
Nyuma ya upole wa sura, maneno kutoka kinywa chake kuwa ya kistaarabu, huku kwa mbali akiwa na kigugumizi, lakini anamshangaza anayemhoji baada yakufichua mambo mazito aliyowahi kufanya na kama ni mwoga unaweza ukatimua mbio licha ya udogo wa umbo lake. Shukrani kwa soka ambalo limeokoa maisha yake na kuwa mtu muhimu katika taifa na familia yake, vinginevyo kutokana na maisha aliyopitia wakati akisaka nafasi ya kutoboa kimaisha pengine hivi sasa unavyosoma andiko hili angekuwa gerezani ama jina lake lingesahaulika kwenye uso wa dunia kama walivyotutoka wapendwa wetu wengine.
Je unataka kujua amefichua nini? Kitu ambacho hajawahi kufumbua mdomo wake kukiongea sehemu yoyote, fuatana na gazeti lako la Mwanaspoti linalotumia muda wake mwingi kufuatilia habari za wachezaji na kuzichambua kwa kina, ili msomaji kupata taarifa sahihi za michezo na burudani na zilizojaa mafunzo.
Nado ni mchezaji mkarimu, asiyependa kumkwaza mtu hata kama atamuongelesha kitu asichokipenda. Staa huyu hujipa subira ya kujibu kwani kwa hekima ya uso wake unaweza kukuonyesha baadhi ya vitu kwamba umemkosea.
Februari 17, 2021 Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit maarufu kama Zaka za Kazi alitoa kibali kwa Mwanaspoti kwenda Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mahojiano ya ana kwa ana na Nado ambaye siku chache nyuma alikuwa ametoka kuuwasha moto kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba.
Huko ndipo tulipobaini kuwa winga huyo ambaye amepitia mengi, ikiwemo kujihusisha na wizi anaweza kuwa mfano kwa vijana wengine wanaotokea kwenye maisha ya hali ya chini kuamini kupitia ndoto zao, huku wakichukulia changamoto kuwa ni fursa. Baada ya kufika Chamazi tulipata nafasi ya kuonana naye na kumweleza nini kilitupeleka, ambapo aliufurahia ugeni wetu.
Alipenda kutufahamu, utambulisho ukachukua nafasi yake, kisha akahoji kwanini yeye na sio mchezaji mwingine ambapo tulimpa ufafanuzi na mara moja mahojiano yakaanza.
KIWANGO DHIDI YA SIMBA
Nado anasema siku zote amekuwa akiamini katika uwezo wake. “(Dhidi ya Simba) tulienda mapumziko tukiwa nyuma kwa bao 1-0, tuliamini wakati tukiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kuwa bado mchezo upo upande wetu licha ya kuwa nyuma. Tulirejea na nguvu mpya, ndio maana tulisawazisha na kuwatangulia lakini bahati ikawa upande wao wa kusawazisha,” anasema.
“Bao la kusawazisha nililomfunga (Aishi) Manula ni moja ya mabao yangu bora kuwahi kufunga kwenye ligi kwa sababu nilikuwa winga ya kulia na nilifunga kwa mguu wa kushoto, nimezoeleka kutumia mguu wa kulia ila watu hawajui kuwa kama mpira ukikaa vizuri mguuni naweza kupiga mashuti hata kwa mguu niliofungia.”
“Sikupiga kwa bahati mbaya nilijiona nipo kwenye nafasi nzuri na sikuwa na chaguo lingine, kwa kiasi kikubwa bao liliongeza morali kwa timu ndio maana tukapata bao la pili ambalo nalo nilihusika kwa kutoa asisti,” anasema Nado mwenye mabao manne katika ligi.
ETIENNE AMPA SHAVU
Miongoni mwa makocha ambao Nado anawaheshimu na wamekuwa na mchango mkubwa kwenye maisha yake ya soka ni pamoja na Etienne Ndayiragije, anayedai kuwa wakati akiwa Mbeya City alikuwa akikutana na kocha huyo akiwa na timu pinzani, lakini hakuwa akisita kumpongeza kwa kiwango ambacho alikuwa akikionyesha.
“Karibu mara zote alikuwa akinipongeza kuwa nacheza vizuri huku akinitaka kuongeza juhudi zaidi, nakumbuka kwamba alikuwa akiifundisha Mbao kipindi hicho na hata alipokuwa KMC. Nilikuwa nikijisikia poa kwa sababu kwangu halikuwa jambo dogo kocha wa timu pinzani kukubali uwezo wangu na nilikuwa nikimsikiliza na kuongeza juhudi,” anasema.
Baada ya kocha huyo kupata shavu la kujiunga na Azam alipendekeza kuletewa Nado ambaye mkataba wake Mbeya City ulikuwa umemalizika.
Nado anasema alipigiwa simu na aliyekuwa meneja wa timu hiyo, Philippo Alando na kuelezwa kuwa wanamtaka.
Kwa kuwa ilikuwa ndoto yake kupata nafasi ya kuichezea timu kubwa baada ya kuwa Mbeya City kwa misimu miwili na kufunga mabao 11, yakiwemo 10 ya msimu wake huo wa mwisho (2018/19) kwenye ligi. “Chapu kwa haraka nilikuja Dar na yalifanyika mazungumzo ya kujiunga na Azam, nilifurahi sana kwa sababu niliona ni hatua kwenye soka langu.
“Unajua baada ya mkataba kumalizika nilikuwa na mawazo kuwa huenda ningepata timu ya kawaida, kwa hiyo lazima nimshukuru Etienne kwa nafasi kubwa ambayo alinipa, nilipambana ili kuonyesha thamani yangu, lakini kwa bahati nzuri akapata nafasi na kuwa kocha wa timu ya taifa sikukaa naye sana Azam ila nilifurahi kufanya naye kazi.”
JUKUMU LA KITAIFA
Kutoka kuwa mtu wa chini ambaye hakuwa na mbele wala nyuma, Etienne aliamini kupitia Nado ambaye ukimwona ana umbo la kawaida, lakini shughuli yake akiwa na mpira ni nzito, uwezo wake wa kushambulia kupitia pembeni ulimsukuma kocha huyo na kuamini kuwa ana uwezo wa kulisaidia taifa hivyo alimwita Taifa Stars.
“Nilivyopata nafasi ya kuwa mchezaji wa Azam nilikuwa na matumaini kuwa ipo siku naweza kuitwa timu ya taifa. Kweli bwana haikuchukua muda mrefu niliitwa na Ettienne, ilikuwa ni kwa ajili ya kuwania nafasi ya kushiriki mashindano ya Chan ambayo yamechezwa mwaka huu, kipindi hicho ilikuwa mwaka 2019,” anasema.
“Ilikuwa ni hatua muhimu kwenye soka langu kwa sababu niliheshimiwiwa kwa kupewa jukumu zito la kulitumikia taifa, nashukuru Mungu kwa kushirikiana na wenzangu tulipambana na kuwaondoa Kenya ambao tulicheza nao. Baada ya kutoka nao suluhu kwenye michezo miwili, nyumbani na ugenini tukashinda kwa penalti,” anasema.
UTAMU WA LIGI
Nado anasema kwamba aliuonja utamu wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu wa 2013/14 akiwa na Ashanti United ya Dar es Salaam ambayo msimu huo ilishuka daraja na ilikuwa mchezo dhidi ya Yanga ambao kikosi chao kilikuwa kimesheheni mastaa kama vile Saimon Msuva, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Mbuyu Twite.
“Nilivyoingia (uwanjani) nilikuwa natetemeka na kocha alivyonipa nafasi alisema nikigusa mpira tu natakiwa kuachia kwa haraka, nilipokuwa nagusa mpira wachezaji wenzangu walikuwa wakinisogelea kwa haraka na kuutaka mpira kwa sababu walijua kuwa mimi bado mdogo na nahitaji msaada wao ili kukuza kujiamini kwangu.
“Baadaye nikaona mbona kawaida, maana Yanga walikuwa na watu hasa kule nyuma, nikaanza kukokota kidogo mpira halafu naachia, nilifurahi sana kucheza ligi kwa mara ya kwanza na ilikuwa mzunguko wa pili na baada ya mechi nakumbuka nilikuwa nikipongezwa kwa kazi nzuri ambayo niliifanya, hata wachezaji wa Yanga walinikubali,” anasema.
Katika mzunguko huo wa pili ambao Nado alianza kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu, anasema alifunga mabao matatu lakini hayakutosha kuinusuru timu hiyo kushuka daraja baada ya kuzidiwa pointi moja na JKT Mgambo ambao walimaliza msimu wakiwa juu kwa pointi 25. Chama la Nado lilijikuta likishuka daraja likiwa na pointi 25 sambamba na JKT Oljoro iliyomaliza na pointi 19 huku Rhino Rangers wakiburuza mkia na pointi 16.
“Ule mwanga ambao nilikuwa nikiuona wa kupata vihela vya hapa na pale ulianza kufifia taratibu na kurejea kwenye maisha ambayo nilikumbana nayo kwa kipindi kirefu baada ya kuondokewa na mama, nilicheza Daraja la Kwanza lakini hakukuwa na pesa Ashanti ndipo nilipojiingiza kwenye ndondo ili kupata pesa za kujikimu.”
MSOTO WA KUTOBOA
Nado ni kijana ambaye amepata malezi ya mzazi mmoja ambaye ni mama, hakuweka jina lake wazi, lakini Mungu ampumzishe mahala pema peponi na ndiye aliyekuwa kichwa cha familia iliyokuwa na dada zake wawili pamoja na bibi yao, ambapo walielezwa kuwa baba yake alizingua.
Ule uchangamfu wake usoni baada ya kufika mbali kimazungumzo ulipotea na simanzi ikamtawala, hivyo tuliishia hapo upande wa baba yake. Maana hakujisikia poa kumuongelea, lakini aliendelea kuongelea vile ambavyo mama yake alikuwa shujaa kwenye familia akipambana na kuwa na gari ambalo walilifanya kuwa la abiria na kuwa kitega uchumi chao.
“Mama alikuwa akinisapoti wakati akiwa hai na hicho ndio kilikuwa kipindi napambana kutoka kimpira, maisha nilikuwa nikiishi mazuri kwa sababu mambo yalikuwa mazuri nyumbani, nilipata kila nilichokuwa nataka, sikuwa nawaza sana kuhusu pesa kwa sababu nilikuwa naamini ukifika wakati wangu kila kitu kitakaa sawa,” anasema “Nilikuwa nacheza timu yangu ya mtaani ambayo ilikuwa ikifundishwa wakati huo na makocha wawili wa kike - mmoja wao ni Fatuma Omari ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa wa KMC na timu ilikuwa ipo Kimara na ndio watu ambao walinipekea Ashanti kufanya majaribio na nikapata nafasi ya kuwa hapo na kuanza maisha yangu ya mpira,” anasema.
Nado amepitia ngazi mbalimbali ya timu za vijana za Ashanti kabla ya kuwa timu kubwa. Alianzia chini akiwa na Hassan Kabunda ambaye anafanya vizuri akiwa na KMC, lakini bahati mbaya mama yake alitanguliwa mbele za haki kabla ya hata kumshuhudia akipokea mshahara wake wa kwanza kwenye soka.
MAISHA BILA MAMA
Baada ya kuondoka kwa mama aliyekuwa nguzo ya familia, Nado anasema ndipo alipokumbana na ugumu wa maisha kwani kila kitu kilikuwa tofauti na vile ambavyo ilikuwa awali. “Hata upatikanaji wa chakula ukaanza kuwa changamoto, Nikawa mtu wa kutoka asubuhi na kurudi jioni kama ndege vile, ndipo nilipoanza kujichanganya na makundi ya mtaani ili kubangaiza na kupata chochote,” anasema.
ITAENDELEA KESHO