Nabi: Njooni mhesabu mabao

Sunday June 20 2021
nabi pic
By Charles Abel

KOCHA Nasreddin Nabi amewaita mashabiki wa Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kuhesabu mabao, wakati chama lake litakapowakaribisha vibonde wa Ligi Kuu Bara, Mwadui katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo.

Matokeo ya ushindi tena mnono ndio yanayosubiriwa kwa hamu mashabiki wa Yanga katika mchezo huo utakaopigwa saa 1:00 usiku, huku kocha Nabi akisisitiza atawapa shoo kali bila kujali kama wapinzani wao ni dhaifu kiasi gani, muhimu wake ni kuona wanazoa alama tatu zote usiku wa leo.

Ubovu wa safu ya ulinzi ya Mwadui iliyoruhusu jumla ya mabao 60 katika mechi 31 za Ligi Kuu msimu huu unaonekana unaweza kuwa fursa nzuri kwa safu ya ushambuliaji ya Yanga kuendeleza kile ilichokifanya katika mechi uliopita dhidi ya Ruvu Shooting ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Katika mechi ya juzi dhidi ya Ruvu, Yanga iliupiga mwingi na kuwapa burudani mashabiki wake, licha ya dakika za mwisho mambo yalikaribia kuharibika, lakini kwa mchezo wa leo Yanga imeahidi kumaliza mapema ili kujiweka katika nafazi nzuri ya kubanana na watani wao na kuwakimbia Azam.

Mchezo wa leo ni muhimu zaidi kwa Yanga kuliko Mwadui, kwani inahitaji kuendelea kuipa presha Simba katika mbio za ubingwa kuliko Mwadui ambayo haina cha kupoteza kwani tayari imeshashuka daraja mapema huku ikiwa na rekodi mbovu kuliko timu zote katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

Kama Yanga itashinda leo itafikisha 67 na kufanya isalie nafasi yake ya pili, ikizidi kuikimbia Azam ambayo juzi usiku iliishindilia Gwambina mabao 4-1 na kufikisha alama 63, nyuma na ilizonazo Yanga kwa sasa, lakini ikipoteza itakuwa imewapa nafasi Yanga kutangaza ubingwa mapema zaidi.

Advertisement

Mwadui katika mechi 10 zilizopita, imeibuka na ushindi mara moja tu na kutoka sare moja, ikipoteza michezo nane, imefunga mabao manne na kufungwa mabao 19, wakati Yanga katika mechi kama hizo imeshinda tano, sare tatu na kupoteza miwili, imefunga mabao 13 na imefungwa nane tu.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema anaupa uzito mkubwa mchezo huo wa leo licha ya nafasi iliyopo Mwadui, iliyotoka kufungwa nyumbani kwa mabao 3-1 na timu ya Mtibwa Sugar.

“Kwa sasa kila mchezo kwetu ni muhimu na tunahitaji kupata ushindi. Hakuna timu rahisi kwenye ligi hivyo kikubwa ni kuhakikisha tunacheza vizuri na kupata matokeo mazuri,” alisema Nabi.

Katika mchezo wao wa kwanza uliopigwa mjini Shinyanga, Mwadui ilichapika kwa mabao 5-0, hivyo leo watakuwa na kazi ya kufuta aibu hiyo, vinginevyo wanaweza kuhesabu mabao ya kutosha kama Yanga itacheza kwa kasi iliyoanza nao kwenye mchezo wao dhidi ya Ruvu.

Yanga katika mchezo wa leo itakuwa na mabadiliko langoni kwani Farouk Shikhalo huenda akaanza badala ya Metacha Mnata ambaye amesimamishwa kwa sababu ya utovu wa nidhamu, huku sehemu ya kikosi kilichoinyoa Ruvu mabao 3-2 kiliendelea kubaki kama kilivyo.

Mbali na mchezo huo wa usiku, mapema leo mchana katika Uwanja wa Karume, mjini Musoma Mara wenyeji Biashara United wataikaribisha JKT Tanzania, huku maafande wakiwa na kazi ya kutafuta ushindi ili kuepuka kushuka daraja na wenyeji wao wakitaka kujihakikishia nafasi ya nne.

Mjini Bukoba jioni kwenye Uwanja wa Kaitaba, nako kutakuwa na kibarua kingine wakati wenyeji Kagera Sugaritaikaribisha Ihefu, huku timu zote zikipambana kuepuka kushuka daraja, huku ligi yenyewe ikiwa ukingoni kabisa.

Advertisement
​