Mzamiru, Mo Ibrahim washindwe wenyewe

Muktasari:
Mzamiru Yassin, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, Said Ndemla na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyekuwa majeruhi wamepewa mchongo kama wataamua kukaza mbele ya Aussems lazima kitaeleweka, la sivyo itakuwa imekula kwao.
UKISIKIA zali ndilo hili. Nyota waliokuwa hawapati namba katika kikosi cha kwanza cha Kocha Mfaransa, Pierre Lechantre alipokuwa akiinoa Simba, sasa wana nafasi ya kurekebisha mambo chini ya Mbelgiji, Patrick Aussems.
Mzamiru Yassin, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, Said Ndemla na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyekuwa majeruhi wamepewa mchongo kama wataamua kukaza mbele ya Aussems lazima kitaeleweka, la sivyo itakuwa imekula kwao.
Kiungo mkongwe wa Kagera Sugar, George Kavila amevitazama viwango vya Ndemla, Mzamiru, Mo na Tshabalala na kukiri kwamba jamaa ni mafundi, ila lazima waongeze juhudi ili waweze kunoga uwanjani na wawe na mtazamo wa mbele wasiishie kushangiliwa na mashabiki wa timu hiyo.
“Ni wachezaji wazuri hata kama hawakuwa na nafasi ndani ya kikosi cha Lachantre, ila naamini watakuwa na nafasi kwa kocha mgeni kama wataamua kumshawishi kabla Ligi Kuu Bara haijaanza rasmi Agosti 22,” alisema Kavila.
Naye nyota wa zamani wa timu hiyo, Mussa Hassan Mgosi alimzungumzia Mzamiru na kudai ni mchezaji mzuri kwani anajua kutumia nguvu, kujituma na nidhamu ya kazi.
“Mzamiru ni mchezaji mzuri, ajitume kwa bidii naamini atakuwa yupo vizuri katika msimu huu pia, ajiwekee malengo ya mbele ndipo anapokuwa na maajabu zaidi, ” alisema.