Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MTASUBIRI SANA: Yanga yatwaa ubingwa Tanzania bara

Mashabiki wa Yanga wakishangilia baada ya timu yao kuifunga Polisi Morogoro na kunyakuwa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara 25. Yanga ilishinda 4-1. Picha na Said Khamis   

Muktasari:

Yanga ilipata ushindi wake wa nane mfululizo baada ya kuichapa Polisi Moro mabao 4-1 huku Mfungaji Bora wa msimu uliopita, Amissi Tambwe akifunga ‘hat-trick’ ya nne ndani ya misimu miwili tangu atue nchini akitokea Burundi.

SIMBA na Azam bado zinaviziana katika kuwania nafasi ya pili, lakini Yanga ndio Mabingwa Wapya wa Tanzania baada ya jana kutangazwa rasmi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga ilipata ushindi wake wa nane mfululizo baada ya kuichapa Polisi Moro mabao 4-1 huku Mfungaji Bora wa msimu uliopita, Amissi Tambwe akifunga ‘hat-trick’ ya nne ndani ya misimu miwili tangu atue nchini akitokea Burundi.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa alifunga hat-trick mbili msimu uliopita akiwa na Simba na jana aliongeza nyingine ya pili akiwa na Yanga na kuweka rekodi ya aina yake katika Ligi Kuu ya Tanzania sambamba na kuiwezesha Yanga kutwaa taji la 25 la Ligi Kuu tangu mwaka 1965.

Watani zao Simba ndiyo wanaofuata katika orodha ya timu zilizotwaa mara nyingi ubingwa wa ligi, ikifanya hivyo mara 18 na kufuatiwa na Mtibwa Sugar mara mbili.

Hilo lilikuwa taji la tatu kwa Yanga ndani ya misimu mitano na katika kunogesha ushindi huo mashabiki wa Yanga walishangilia ubingwa kwa kurusha mafataki na kunyanyua kombe bandia, huku wachezaji na benchi la ufundi wakivaa fulana zilizoandikwa Yanga Bingwa 2014-2015.

Katika pambano hilo la jana Polisi walionyesha upinzani dakika 45 za kwanza, ingawa waliruhusu bao dakika tano kabla ya mapumziko lililofungwa na Tambwe kwa shuti akimalizia krosi tamu ya Simon Msuva.

Kipindi cha pili kilianza kwa Polisi kuonyesha uhai na kutaka kurejesha bao, kabla Tambwe hajawakata maini alipoandika bao la pili dakika ya 53, akimalizia shuti la Msuva, lililookolewa na kipa wa Polisi, Abdul Ibad.

Dakika tano baadaye kipa Deo Munishi ‘Dida’ alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti la karibu la James Ambrose aliyewahadaa mabeki wa Yanga na kubaki uso kwa uso na Dida.

Tambwe aliendelea kuiadhibu Polisi kwa kufunga bao lake la tatu katika mchezo huo na la 14 katika msimu huu kwa kuunganisha kwa kichwa krosi ya Msuva aliyeng’ara mno jana.

Wakati Polisi wakijiuliza namna ya kurejesha mabao hayo ili kujipa matumaini ya kubaki katika ligi ya msimu ujao, walishtukia wakipachikwa bao la nne kupitia kwa Msuva aliyefunga katika dakika ya 66 akimalizia pasi murua ya Mrisho Ngassa.

Bao hilo liliwafanya wachezaji wa Polisi kumzonga mwamuzi Zakaria Jacob kwa madai mfungaji alikuwa ameotea, lakini mwamuzi alishikilia msimamo wake na mchezo kuendelea.

Polisi walijifariji kwa kupata bao la kufutia machozi lililofungwa dakika ya 84 na Bantu Admin kwa shuti kali la umbali wa mita 30, bao ambalo halikuweza kuwaepusha na kipigo, hadi mwisho wa mchezo Yanga walikuwa wababe kwa mabao 4-1.

Kwa matokeo hayo Yanga imejikusanyia pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote ikiwavua taji Azam, huku ikiwa na rekodi na kufunga mabao mengi, 51 na ikiruhusu mabao 15 tu katlangoni mwake na wakiwa wamesaliwa na mechi mbili kabla ya kumaliza msimu.

Kocha mkuu wa Yanga, Hans Pluijm alisema amejisikia faraja kubwa kuiwezesha timu yake kutwaa taji hilo, lakini kwa sasa wanaelekeza nguvu zao katika mechi ya marudiano dhidi ya Etoile du Sahel katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa ugenini mwishoni wa wiki hii.

YANGA: Deo Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Said Juma, Msuva/Hussein Javu, Haruna Niyonzima/Nizar Khalfan, Tambwe/Jerry Tegete, Ngassa na Kpah Sherman.

POLISI MORO: Abdul Ibad, Ally Teru, Hassan Mganga, Meshack Abel, Laban Kambole, Anafi Seleman, Admin Bantu, Said Mkangu, Said Bahanuzi/ Nicholas Kabipe, Seleman Kassim na James Ambrose/Mussa Mohammed.