Mo Dewji alipa mishahara Simba ili waiue Asec

RAIS wa heshima wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ juzi aliwamwagia mkwanja wachezaji wa kikosi hicho mchana wa Jumatano alipowatembelea kambini kwao.

Bilionea huyo baada ya kikao cha dakika kadhaa na wachezaji, kwanza aliwalipa wachezaji na benchi la ufundi mishahara yao ya mwezi Januari kila mmoja.

Wachezaji wa Simba baada ya hapo walipokea bonasi ya mechi nne walizoshinda awali dhidi ya Azam, Dar City, Tanzania Prisons na Mbeya Kwanza.

Mechi ya Azam walipewa bonasi ya Sh50 milioni wakati Dar City, Prisons na Mbeya Kwanza hizo kila moja ilikuwa Sh20 milioni kwa maana hiyo mara tatu ni Sh60 milioni ukijumlisha na ile ya Azam walivuta jumla ya Sh110 milioni.

Bonasi hizo ukiondoa mechi ya Azam, nyingine zilizobaki wachezaji wanagawana tofauti mchezaji aliyecheza hata dakika moja anapata Sh400,000 aliyekuwa benchi na hakucheza Sh200,000 wakati wale wa jukwaani si zaidi ya Sh100,000. Wachezaji hao wa Simba mbali ya kuongezewa mzuka walielezwa kabla ya mechi ya Mimosas wataahidiwa bonasi nyingine kama watashinda wataichukua kabla ya kwenda Niger katika mechi ya USGN.

Februari 17, kikosi cha Simba kitaondoka nchini kwenda Niger katika mchezo wa pili hatua ya makundi kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USGN na baada ya hapo hawatarejea nchini wataunganisha huko huko kwenda Morocco.

Baada ya mambo yote hayo, Mo Dewji alisema atakuwepo uwanjani kwenye mchezo dhidi ya Mimosas na anawaomba mashabiki wa timu hiyo wajitokeze kwa wingi.

“Nimekuja kambini kukutana na wachezaji na viongozi kuwapa hamasa, unajua kwa nini Simba imekuwa kati ya klabu kumi bora Afrika ni kutokana na kushindana katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu bahati mbaya tumeteleza,” alisema Mo Dewji na kuongeza;

“Tupo katika kombe la Shirikisho Afrika lazima tujipange kwani ni mashindano ya kweli lakini bado tunakazi ngumu kwenye ligi na lazima tuwe na malengo makubwa.”

Mo Dewji alitumia muda mwingi kuwaeleza wachezaji, benchi la ufundi na stafu wengine thamani ya klabu hiyo. Aliwaambia wanakazi kubwa ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kusahau matokeo mabaya waliyopata katika michezo iliyopita ila wanapaswa kuyachukulia kama funzo na kufanya vizuri michezo ijayo na lisiwatokee tena.

Aliwaeleza wachezaji na benchi la ufundi pointi walizoachwa na vinara wa ligi si nyingi kama kwa pamoja kila mmoja atakuwa na lengo la kupambana kushinda kila mechi iliyokuwa mbele yao. Mo Dewji baada ya hilo aliwambia wachezaji malengo mkubwa ya Simba yalikuwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika ila imetokea bahati mbaya wameondolewa sasa nguvu zao zote wazihamishie kwenye Shirikisho Afrika.

Aliwaeleza wachezaji wanatakiwa kupambana mpaka tone la mwisho ili kufanya vizuri katika mechi ya Jumapili dhidi ya Asec Mimosas na si hiyo bali zote za hatua ya makundi ili kuvuka na kwenda hatua za mbele zaidi ikiwezekana kuchuku ubingwa.

Baada ya hapo Mo Dewji aliwaambia wachezaji na benchi la ufundi viongozi wapo pamoja nao katika kila kitu wanafanya na kuwa tayari kuwapatia kila kitu ili kutimiza yale malengo ya timu na kuhakikisha hadhi ya Simba inabaki palepale ndani na nje ya nchi. Nini maoni yako kuhusiana na habari hii; Tutumie; 0782-707 579.